“Usimpakazie Mungu Ujinga Wako”
Utangulizi: Wakati Akili Inapolala, Utaahira Hutawala
Kuna nyakati unaposhabikia baadhi ya mambo kwa nguvu zote, ni lazima kwanza uweke akili pembeni - ndipo utaelewa kwanini upumbavu huishi kwa shangwe.
Ni kana kwamba, ili uendelee kushabikia upumbavu, unalazimika kuvaa utaahira.
Na katika baadhi ya nyakati, unapopewa mamlaka, ni kana kwamba unapaswa kuvua utu wako, kuuacha pembeni, kisha kuvaa unyama - halafu kwa ujasiri wa ajabu, ukamnukuu Mungu kama chanzo cha mamlaka hayo.
Huu ndio uso halisi wa mifumo mingi ya utawala duniani; mifumo isiyopangwa na Mungu, wala haitawahi kupangwa naye, kwa sababu ni zao la ubunifu wa Watu waliopofushwa na tamaa ya nguvu na kiu ya kutawala wengine.
Mifumo Isiyo ya Kimungu
Wazo la kugawa dunia lilianzia Ulaya, katika zama ambazo watu walianza kuingiliana na viumbe wa ulimwenguni - malaika na viumbe majini - waliowafundisha taaluma za mamlaka na utawala.
Kupitia elimu hiyo, walijenga dhana ya mamlaka na mipaka, wakaanzisha kanuni za kugawa ardhi kwa misingi ya nguvu, si udugu.
Huko huko Ulaya, walijaribu mfumo huo na kuuthibitisha.
Baada ya kuona unafanya kazi kwa manufaa yao, wakauleta barani Afrika kupitia mlango wa ukoloni.
Hapo ndipo mipaka ilipochorwa, ndugu wakatenganishwa, marafiki wakageuzwa maadui, na jamii zilizokuwa kitu kimoja zikapasuliwa kwa kalamu na ramani za wageni.
Ndipo mipaka ikaundwa - na hivyo Afrika ikawekwa ndani ya sanduku la uhasama, migogoro, vita na majeraha ya kiakili.
Hadi leo, Afrika bado inalipa gharama ya kugawanywa huku; bado tunapigana, bado tunalalamika, bado hatujawa huru kiakili.
Lakini je, haya yalikuwa mapenzi ya Mungu?
Kama kila jambo linapangwa na Mungu, basi ni nini lilikuwa lengo Lake katika mateso haya yote?
Ukoloni na Uongo wa “Mpango wa Mungu”
Ukoloni haukuwa wito wa kimungu. Haukuwa mpango wa wokovu, bali mpango wa utawala.
Wale waliokuja Afrika hawakuwa wametumwa na Mungu bali walitumia jina la mungu wao wa uongo kama kificho cha ulafi wa kujipatia mali na utajiri.
Walijenga misingi ya utawala kwa kuhalalisha uovu kwa jina la “uongozi wa kiroho.”
Hivyo, ikawa rahisi kwao kuwatawala watu kwa kuwapokonya akili na kuwapa imani potofu.
Hata leo, wengi wetu bado tunamini kwamba Mungu alipanga mataifa haya kugawanyika -lakini ukweli ni kwamba, tuligawanywa na Watu waliokuwa na agenda zao.
Mungu Haingilii Matashi ya Kiumbe
Mungu aliumba kiumbe chenye hiari. Na pale hiari inapopoteza mwelekeo, ndipo ubaya huzaliwa.
Kwa hiyo, ni kosa kubwa kumhusisha Mungu na matokeo ya uamuzi mbovu wa MTU.
Mungu hasukumi mtu kufanya maovu.
Anampa akili, dhamira, na uwezo wa kuchagua.
Lakini MTU anaposhindwa kutumia vyote hivyo, hubaki kuishi kwa matashi yake, akipotea ndani ya giza la ujinga wake mwenyewe.
Kwa hiyo, ni uongo mkubwa kusema kila jambo ni “mpango wa Mungu.”
Kuna mambo ni matokeo ya uzembe, ubinafsi, na tamaa ya wanadamu.
Ni rahisi kuishi ovyo na baadaye kusema, “Mungu alipanga.” Hapana. Mungu hajapanga ujinga.
Mungu hajawahi kuagiza watu waandamane, wafe kwa mabomu ya machozi, au wateswe kwa sababu ya haki.
Mungu hajawahi kuamuru utawala wa unyanyasaji.
Kila mfumo wa kikatili ni zao la
MTU aliyeamua kuishi nje ya kanuni za haki na upendo.
Afrika na Tabia ya Kupokea Bila Kuchuja
Afrika imepoteza uwezo wa kuchuja.
Tumepokea kila kitu - dini, elimu, mifumo ya utawala, hata tafsiri ya Mungu - bila kuuliza maswali.
Matokeo yake, kwa wengi wetu, Mungu amegeuka kuwa kiumbe wa mawazo yetu binafsi.
Tunamfanya awe kwa kadri ya uelewa wetu, si kwa asili yake.
Kwa baadhi ya watu, Mungu ni kama kitu cha kufinyangwa - anaweza kubadilishwa kulingana na utashi wa wale wenye mamlaka.
Hivyo ndivyo dini zimegawanyika: kila dhehebu linadai lina Mungu sahihi zaidi, kila kundi linadai lina njia ya kweli zaidi.
Lakini kama kweli Mungu ni mmoja, kwa nini tunaabudu tofauti?
Kwanini wale walio chini ya mwamvuli mmoja wa imani wanashindwana katika sala?
Je, tunamuabudu Mungu mmoja, au tunabudu tafsiri zetu binafsi za Mungu?
Hoja Kubwa: Mungu Si Kisingizio
Mungu ni hoja kubwa - hoja inayozidi mipaka ya akili na tamaduni.
Mungu si kisingizio cha ujinga, si pazia la maovu, si muhuri wa hila za kidini au kisiasa.
Watu wachache hufanya uovu, halafu wanasimama hadharani na kusema “Mungu ametupa nafasi hii.”
Lakini ukweli ni kwamba ni matokeo ya makubaliano yao, si mpango wa Mungu mwenye vyote.
Wengine wakipoteza mwelekeo wa maisha husema “ni majaribu ya Mungu.”
Lakini Mungu si mjaribu wa viumbe vyake; aliumba maisha kwa amani na wema.
Majaribu tunayoyaona mara nyingi ni matokeo ya uamuzi mbovu na maisha yasiyo na mwelekeo.
Kwa hiyo, tusimpakazie Mungu uongo.
Tukifanya upuuzi, tukikosea, tukiumiza wengine - tuseme tu ukweli kwamba ni makosa yetu.
Mungu hana sehemu katika ujinga wetu.
Kuhusu Kuishi na Maana ya Uhai
Mtu anaishi kwa matashi yake, si kwa amri ya siri kutoka juu.
Kila unachofanya ni matokeo ya uamuzi wako.
Kama utachagua hekima, utaishi kwa amani; kama utachagua ujinga, utavuna maumivu.
Kwa hiyo, usiweke jina la Mungu kwenye kila jambo lisilo na maana.
Mungu yupo nje ya ujinga, nje ya ulafi, nje ya ubinafsi.
Mungu aliumba maisha kwa mpangilio, ili kiumbe kiishi kwa haki, upendo, na uelewa.
Kama hujui kwa nini unaishi, utapoteza maana ya maisha.
Ndipo majengo yako, fahari zako, na mali zako zote zitaharibiwa kwa sekunde chache - kwa sababu hujajua kwanini upo.
Mwisho: Tafuteni Ukweli, Si Visingizio
Tafuteni ukweli, tafuteni umoja, tafuteni maana ya kuishi.
Mungu hatakiwi kuingizwa katika upumbavu wa Watu.
Mungu hana mipango mibaya; mabaya ni matokeo ya kuishi nje ya hekima yake.
Kwa hiyo, acha kumhusisha Mungu na ujinga.
Mungu alifanya maisha Kwa amani na wema.
Mungu ni chanzo cha uhai.
Mungu ni hoja kubwa sana - isiyo na nafasi ndani ya ujinga wa MTU.
🖋️ Wenu kijana mdogo,
Mbulwa King’ung’e
📞 0744 284 329
Comments
Post a Comment