AFRIKA: KABLA YA AKILI PANDIKIZI, KABLA YA IMANI YA NGUVU, NA KUPOTEA KWA UTAMBULISHO...
Walikuja wakavikuta vya kwetu vikiwa timamu. Wakavivuruga. Wakaleta vya kwao. Vikatutoa kwenye mfumo wetu.
...Na leo—hatujijui!
Haya si maneno ya hisia. Ni mwanzo wa kukuleta kwenye ukweli.
Historia ipo wazi kabisa: bara la Afrika halijawahi kwenda kuharibu, kutawala, au kusababisha migogoro katika mabara mengine.
Afrika halikuwahi kuwa bara la uvamizi; lilikuwa - na bado ni—bara la uhai.
Lilijua mema ya kuishi. Lilijua ukweli wa kuishi. Lilijua umoja wa watu, upendo, undugu na uwiano kati ya watu, asili na Uungu.
Kwa maana hiyo, katika kuishi kwako leo, kama hujawahi kuyaelewa mema ya wazazi na mababu zako, na ukahisi walikuwa wapotevu au waliishi gizani, basi ujue fikra zako zilipinduliwa kabla hujazaliwa.
Mema ya wazee wetu hayakupotea yenyewe - yalipinduliwa kwa makusudi. Yakavunjwa.
Yakadharauliwa. Kisha yakapandikizwa akili nyingine na imani nyingine.
Hili halikufanyika kwa bahati mbaya. Lilifanyika kwa mkakati.
Mkakati ulikuwa mmoja: mkate mizizi, mabadilike kiakili, kisha muingizwe kwenye mifumo isiyo yenu.
Ndiyo maana mliingizwa kwenye mirabaa ya kibiashara kama wanunuzi, si watengenezaji.
Kwa sababu wanachokuuzia hakina mizizi yako, hivyo lazima uuziwe tu milele.
Leo hii mmegeuzwa kuwa watumwa wa kifikra.
Chenu hamna.
Mifumo ya maisha, elimu, uchumi, hata tafsiri ya Mungu, inaendeshwa na wageni, kimya kimya.
Elimu yenu inawapa vyeti, si maadili.
Inawapa taaluma, si utambuzi.
Inawapa utii, si uwezo wa kuhoji.
Ndiyo maana mnalalamika kukosa ajira.
Kwa sababu mmefundishwa kuwa watumiaji, si waundaji.
Mmefundishwa kutumikia mifumo, si kuunda maisha.
Mmefundishwa kuishi kwa ruhusa, si kwa uelewa.
Mnalalamika, lakini bado mnaendeleza mnyororo uleule uliowafunga.
Hamjui kwa nini maisha yapo.
Mmeaminishwa maisha ni:
Kusoma, kujua lugha za wengine, kupata cheti, kuajiriwa, kulipwa mshahara, kisha kufa.
Hiyo siyo MAANA ya uhai. Huo ni mzunguko wa matumizi.
Maisha yakiwapiga, mnageuka wachungaji, manabii, na walaghai wa kiroho—mkifuata miongozo ile ile iliyowapotosha, ikawatoa kwenye utu wenu; sasa mkiitumia kuwapotosha wengine.
Kila mtu anadai katumwa na Mungu. Ukimuuliza ametumwa kufanya nini—hakuna jibu jipya, zaidi ya kuendeleza mnyororo uleule wa kufunga fikra za watu.
Ukweli huu haupendwi, lakini hauwezi kupingwa: dini zote zililetwa Afrika kwa nguvu.
Na kama hujui, maelfu ya watu waliuawa wakati miongozo hiyo inaingizwa.
Hivyo swali haliepukiki: Kama huyo anayeitwa mfalme wa amani alikuwa analeta amani, kwa nini waliokuja kwa jina lake walitumia upanga, risasi na moto—hasa kwa wale waliopinga upotevu huo?
Huu si uzushi. Huu ni ukweli wa kihistoria.
Sijasema kwa jazba. Sijasema kwa kusikia. Maisha ya kipotevu yaliyovikwa ukweli nimeyaishi.
Siyasemi haya ili uache kila ulicho nacho.
Nayasema haya ili kuikosoa akili yako.
Kwa sababu akili—ikikosa kukosolewa—huwa gereza la mtu mwenyewe.
Hebu tafakari kwa uaminifu:
Majina ya koo za babu zenu mnaosema walikuwa wachawi au wapotevu—mmeyarithi, hamjayakataa.
Majina ya makabila ambayo mengine yalitokana na majina yao - mmeyakubali, mnayataja Kama yalivyo.
Majina ya maeneo mbalimbali waliyoyapa—mmeyakubali, mnayataja kama yalivyo.
Majina ya vitu vya asili—mmeyakuta, mmeyakubali.
Baadhi ya mila na desturi—hata kama kwa uchache—mmezikubali.
Lakini ile imani yao ya kweli, ile iliyowaunganisha na Uungu bila mpatanishi wa kibiashara—mmeikataa.
Mnakubalije kila kitu kingine, mkapinga kimoja tu?
Hamuoni kuwa tatizo si imani—ni akili iliyopandikizwa?
Nikikuuliza leo:
Kama jina Mungu lilikutwa likitumika Afrika kabla ya tafsiri za Ulaya, unalipinga vipi jina lililokutwa likiabudiwa na babu zako?
Unalifananisha vipi jina hilo la asili na tafsiri zilizokuja baadaye?
Ukweli ambao wengi hawapendAfrika haikumjua Mungu kwa kusimuliwa—ilimjua Mungu kwa uhalisia wake!
Waafrika walimtaja Mungu.
Walimsalia katika roho na katika kweli.
Walimheshimu kupitia Sala, si kupitia hofu.
Ni sawa na wewe leo uende China, ukakuta wanaabudu dragon.
Wewe humjui dragon huyo. Halafu uanze kuleta maadili yako, tafsiri zako, na mfumo wako.
Matokeo yake unaharibu maana halisi ya dragon kwa Wachina.
Hiki ndicho kilichotokea Afrika.
Ndiyo maana elimu yako inakusahaulisha wewe ni nani.
Ndiyo maana historia yako inakuambia zaidi Ulaya kuliko mizizi yako.
Ndiyo maana unafundishwa kupata kazi, lakini si kupata nafsi.
Wanajua walikubadilishia historia.Wanajua uwezo na nguvu za Mungu wa Afrika.
Hawataki uungane naye.
Wanataka uendelee kutaabika—bila utulivu wa nafsi, bila mizizi, bila mwelekeo.
Mimi si mzushi.
Nimewauliza watu wengi swali moja rahisi:
Mungu ni nini?
Wengi hawajui.
Sasa nikuulize wewe:
Mungu ni nini kwako?
Asili ya jina Mungu ni lugha gani?
Limetoka katika ardhi gani?
Haya si maswali ya kidini.
Ni maswali ya utambuzi.
Afrika haitaki wokovu wa kuazima.
Inataka kukumbuka ilichokuwa kabla ya kusahaulishwa.
Mbulwa King’ung’e
Mwandishi wa Ukombozi wa Akili na Utambuzi wa Kiafrika
Mawasiliano: 0744285329
Comments
Post a Comment