Aliyekuahidi Connection Ameondolewa Kwenye Mfumo, Jiinue Ustahili Kuunganishwa Na Wengine...
Leo nimechukua muda wangu kuandika jambo ambalo limekuwa likiwatesa wengi kimya kimya:
Connection. Nafasi. Fursa. Milango ya kupanda ngazi.
Ni ukweli ulio thabiti, kila siku tunasikia malalamiko: “Nimehangaika lakini sifanikiwi,” “Nimeahidiwa connection lakini imegoma,” “Hakuna anayeniona.”
Kwa BAHATI Mbaya hata wale watu waliokuahidi connection, nafasi, msaada au mlango fulani wa mafanikio, leo hawapo tena kwenye mfumo.
Hiyo haitakiwi kukukatisha tamaa; inapaswa kukutia akili.
Kwa sababu connection ya kweli haitegemei mtu, mfumo au huruma. Connection ya kweli inategemea thamani yako.
Kwa mantiki hiyo kabla ya kuuliza “nani atanisaidia?”
Jiulize kwa uaminifu: Nimekuwa mtu wa aina ipi kiasi cha mtu kuniona na kusema -“huyu namchukua”?
Hii si hoja ya kujilaumu. Ni hoja ya kujiamsha.
Kwa sababu hakuna connection ya kudumu inayojengwa juu ya mtu asiyejiinua.
Hebu tazama maisha yako kwa jicho la mtu mzima:
Fikra zako zinajenga au zinabomoa?
Mtindo wako wa maisha unavutia au unafukuza fursa?
Tabia zako zinaendana na mtu wa hadhi au bado unatembea kwenye udogo wa fikra za jana?
Watu wengi hulalamika kwamba “connection zimegoma,” lakini ukweli ni mmoja: hakuna kiongozi, mfanyabiashara wala taasisi itakayokuchukua kama hujajijenga.
Hakuna mtu anayehatarisha mfumo wake kwa kumweka ndani mtu asiyejitambua, asiyejitawala, na asiyeweza kubeba majukumu ya kiwango kikubwa.
Hakuna anayetaka kumuinua mtu ambaye hajiamini, haeleweki, au hajajijenga.
Ninasema haya si kwa sababu mimi ni mwandishi wa kukurupuka, hapana.
Nayasema kwa msingi wa uthibitisho thabiti, uzoefu uliojengwa kwenye kazi, watu, mifumo, na matokeo halisi.
Ndiyo maana, hata katika dunia ya leo, tunarejea kanuni ile ile isiyowahi kupoteza uzito wake -
Kanuni ya Uvutano.
Na Kanuni hii inasema wazi kabisa: Unavuta kile kinacholingana na ubora uliojijengea.
Si kile unachotamani. Si kile unacholilia. Si kile unachodai. Bali kile unachokuwa.
Unapovuta watu dhaifu, tambua kuwa kuna kitu kilichodorora ndani yako.
Unapovuta watu wazito, ujue kuwa tayari umeingia kwenye kiwango kingine cha uwezekano.
Hapa ndipo watu wengi wanajiumiza bila kujua:
Wanataka connection kubwa, lakini wanaishi maisha madogo.
Wanataka nafasi za juu, lakini wanafikiri kwa kiwango cha chini. Wanataka kuonekana, lakini hawajitoi kujengwa.
Siku hizi connection haitolewi kwa huruma - inapelekwa sehemu yenye thamani.
Hatutoi connection kwa mtu wa kutumia TV kuliko vitabu.
Hatutoi connection kwa mtu anayekimbilia kutafuta ndoa kuliko kujenga akili.
Hatutoi connection kwa mtu anayekurupuka maishani kama anayekimbiza kivuli chake.
Na hata kwenye taifa, maendeleo hayaji kwa bahati. Taifa linainuliwa na watu walioamua kujiinua kwanza.
Ujenzi wa mtu ni ujenzi wa taifa. Mtu dhaifu anazalisha taifa dhaifu. Mtu mwenye fikra kubwa anachangia taifa kubwa.
Connection inaanzia ndani yako kabla haijafika kutoka nje.
Kama maisha yako ni mzunguko wa kazini–nyumbani–TV–kulala–kuamka,
unatarajia connection gani toka kwa nani?
Ikiwa huna personal development, huna high earning skills, huna mtazamo wa karne hii mpya, bado umejifunga kwenye msemo wa “Wakati wa Mungu utafika”— basi jiulize: Ni kwa namna gani watu wakubwa wakutafute?
Hatuwapi connection watu ambao hata wao hawawezi kujiamini kuwa tayari.
Hatuwapi connection watu wenye roho ya kuombewa kila kitu lakini wasioweza kujijenga hata katika kimo cha ndani.
Connection ya kiwango cha juu inahitaji mtu wa kiwango cha juu.
Watu wakubwa huvuta watu wakubwa. Fursa kubwa huvuta watu waliokua.
Na mifumo mikubwa huwachukua waliowekeza kwenye ubora, sio waliokaa wakisubiri kuchukuliwa.
Hata mimi, kazi ninayoifanya, makala ninazoandika, na majukwaa ninayojenga—
si kwa sababu sina cha kufanya.
Ni kwa sababu hii ndiyo njia yangu ya kujitengenezea jina, weledi, thamani na mazingira ya kukutanisha mawazo na watu wazito.
Na ndiyo maana leo, ninakaa meza moja na watu ambao zamani ningeona kama ndoto.
Si kwa sababu waliniona—bali kwa sababu nilijenga kiwango cha kuniwezesha kuwa mtu wa kuonekana.
Ukikataa kujijenga, mfumo utakubadilisha kuwa chawa wa watu.
Ndio maana mnaona machawa wa vyama, wasanii wanaotumika, watu wa mitandaoni wanaopoteza utu kwa likes— si kwa sababu hawana uwezo,
ila kwa sababu hawakujenga nafasi yao ya kuunganishwa kwenye fursa safi.
Na connection mbaya ni adhabu.Imefanya wengine kuwa watumwa wa kingono, imewafanya wengine kuwa vinyago vya propaganda, imewafanya wengine kupoteza utu wao kwa tamaa ya kutambuliwa.
Ukitaka connection safi, jenga mtu safi NDANI mwako.
Ukitaka kuunganishwa, kuwa wa kuunganishwa.
Ukitaka kufunguliwa milango, kuwa mlango unaoweza kufunguliwa.
Ukitaka kuonekana, jenga kiwango ambacho hakiwezi kupuuzwa.
Hii ndiyo falsafa ya kimataifa ya mafanikio: Thamani yako inatangulia kabla jina lako halitajwa.
Na hata kwenye mentorship zangu—
simchukui kila mtu.
Connection ya kuwa mwanafunzi wangu haipewi kwa huruma.
Nikiangalia mtu nione hana msingi—namnyima.
Kwa sababu connection ya kweli inahitaji mtu tayari.
Wa kuitwa Mbulwa King’ung’e
Mawasiliano: 0744 284 329
Comments
Post a Comment