Kabla Hujaipa Dunia Lawama, Kagua Ridhio Zako...
Utasikia mtu akilalamika: “Maisha yangu yameharibiwa kwa sababu ya fulani…”
Lakini mara nyingi husahau kuwa, katika kile anachokiita kuharibiwa, yeye mwenyewe alichangia—kwa sababu aliweka ridhio yake.
Ni muhimu ieleweke: viumbe huishi kwa ridhio. Kila ridhio hukubalika pale pande mbili zinapokubali kufanya jambo fulani.
Ridhio hiyo ndiyo inayotoa kibali cha tukio kutokea.
Hili si suala la kijamii tu; hata kimungu ni fasaha. Kufanya jambo kwa kulazimisha, bila ridhio ya upande wa pili, ni kukengeuka katika haki—na hata kimungu, hauko sawa.
Ukikubali kumkopesha mtu fedha, halafu akakudhulumu, kabla hujalaumu tafakari: ridhio yako ndiyo iliyomfungulia mlango huo.
Ukikopa fedha kwa mtu, ukaweka ahadi ya kurudisha, kisha ukaanza kuleta kona nyingi wakati wa kulipa—hujaikiuka sheria ya mtu mwingine; umeenda kinyume na ridhio yako mwenyewe.
Ukikubali kuingia kwenye mahusiano na mtu, mkashiriki safari moja ya kihisia na kijamii, kisha mkaishia kuachana, usianzishe lawama za haraka.
Simama kwanza, tafakari ridhio yako, maamuzi yako, na mipaka uliyoiweka au uliyoshindwa kuiweka.
Usilaumu mwenendo mbovu wa serikali au tawala mbalimbali bila kujiuliza swali gumu lakini la lazima: ni nani aliwapa kibali cha uwepo wao?
Historia ya dunia inaonyesha wazi kuwa mifumo huishi kwa ridhio ya wale wanaoivumilia.
Usilaumu watu kwa kukuharibia mipango yako; tafakari kwanza ridhio yako iliyowafanya wawe sehemu ya maisha yako, ya ndoto zako, na ya maamuzi yako.
Usimlaumu hata yule shetani anayesingiziwa karibu kila jambo.
Jiulize kwa ujasiri: kwa nini basi ulimpa ridhio katika maisha yako?
Hakuna nguvu inayotawala maisha ya mtu bila ruhusa—ya wazi au ya kimya.
Hoja ninayojenga hapa ni moja, nzito na isiyoepukika: ukitaka kuishi bila utumwa wa lawama, chunga sana ridhio zako.
Kwa sababu pale unaporuhusu jambo fulani katika maisha yako, bila tahadhari na uwajibikaji, unageuka polepole kuwa mtumwa wa jambo hilo.
Hivyo basi, ili kuepuka utumwa wa lawama, jenga nidhamu ya kuchuja ridhio zako mwenyewe.
Ukitaka usilaumiwe, na ukitaka usiwalaumu watu, linda mipaka ya ridhaa zako.
Ridhio zako zina nguvu mbili: zinaweza kukupandisha uishi kiwango cha juu cha utu, uhuru na thamani—lakini pia, zikiachwa bila hekima, zinaweza kukuangusha kwa kiwango cha chini kabisa cha majuto.
Mwandishi asiyejitambua hulaumu dunia; mwandishi wa hadhi ya kimataifa hufundisha dunia kuwajibika.
Wakuitwa Mbulwa King’ung’e
Mawasiliano: 0744 284 329
Comments
Post a Comment