“Kifo: Mlango wa Uhai, Sio Hukumu...”


Leo ninazungumza nanyi kuhusu jambo ambalo limekuwa likitawala maisha ya viumbe vyote tangu mwanzo wa uumbaji: KIFO.

Na kabla sijaanza kwenda mbali zaidi, hebu tuanze kwa swali rahisi lakini zito: Kama kifo ni matokeo ya dhambi, kwa nini ndiyo kinachotumika kama njia ya kuingia Ufalme wa Mbinguni?

 Je, huo Ufalme ni wa wema au waovu? Kama ni wa wema, iweje waingie kupitia njia inayodaiwa kuwa ovu? 

Na kama ni ufalme wa waovu, basi kwa mantiki hiyo, kifo kingekuwa njia sahihi, ijapokuwa kifo chenyewe si matokeo ya dhambi.

Haya maswali ya msingi yamewafanya wengi wafikiri juu juu, bila kuingia kwenye uhalisia wa maisha na kiini cha uumbaji.

Kwanza, tuweke wazi: kifo ni sehemu ya mfumo wa uishi.

Ni mlolongo wa asili, sheria ya uumbaji ambayo kila kiumbe hupitia. 

Hata kabla ya simulizi za “tunda kuliwa,” viumbe waliishi na walikufa. 

Taratibu za JADI zinaonyesha wazi kwamba MTU wa kwanza, alikufa zaidi ya miaka milioni 11 iliyopita. 

Lakini simulizi la kuliwa kwa tunda linazungumzia historia ya takribani miaka 7,000 tu. 

Sasa kama binadamu ambaye aliishi mamilioni ya miaka kabla ya hiyo simulizi alikufa, wewe unafikiri kifo chake kilikuwa matokeo ya nini?

Najua utakutana na watu ambao watakimbilia majibu mepesi. Mimi sijakurupuka leo. Nina elimu ya kiroho, elimu ya kiutu, elimu ya maisha na elimu ya darasani pia.

 Kwa hiyo ninachokisema sio mawazo mepesi, ni uchambuzi wa kina wenye ukweli ndani yake.

Ukisoma Mwanzo 4:16 kwa macho yasiyofungwa, utaona jambo ambalo wengi hawataki kuliona: Adamu hakuwa mwanzo wa watu wote wa kibayolojia.

Kaini alitoroka akaenda NODI na akakutana na watu. Hata akajenga mji. Ni wazi kulikuwa na jamii nyingine. 

Hawa nao waliishi na walikufa. Sasa swali linabaki: *kifo chao kiliwapeleka wapi? Ufalmeni? Au wapi?*

Hata yule nyoka, ambaye wengi wamejaa hamaki kumwamini kuwa muongo, alisema: “mkila hamtakufa.”

Na kweli hawakufa siku ile. Sasa kama asingesema hivyo, ninyi mnaodai mtu anaingia Ufalme kutokana na kifo mnaweza kuniambia, mngeingia vipi huko kama nyoka asingedanya na ule uongo wake kupelekea kifo? 

Na mbona mnakemea kifo, mnakilaani, wakati mnadai kwamba, ndicho kinachomwezesha mtu kufikia uzima wa milele? 

Au kwa ufupi, mnafahamu kabisa kwamba kifo ni mwiba, halafu mnakitumia kama ngazi ya mbinguni.

Na mbona mnahusisha kifo na shetani? Kwani shetani na Mungu wanategemeana? 

Kama mnaamini kifo ndicho kinachompeleka mtu kwa Mungu, lakini wakati huohuo mnasema kifo ni kazi ya shetani, basi kwa mafundisho yenu yanamaanisha Mungu na shetani wanafanya kazi kwa ushirikiano. Je, si ajabu hii? 

Kwa nini mnalaani kifo kama hamuamini kwamba ni sehemu ya safari ya kwenda kwenye maisha ya roho? 

Kwa nini mnalia wakati mnatambua kwamba huo ni mlango wa kwenda kwenye uzima ulio bora zaidi? 

Kwa nini mnasema kifo hakina huruma, wakati ndicho mnachodai ni barabara pekee ya kuelekea kwa Muumba?

Elimu ya kuishi imenifundisha kwamba kifo ni mfumo wa mpito. Hakipo kwa binadamu tu. 

Kipo kwa kila kiumbe, kuanzia nguruwe mnaowageuza kitimoto hadi viume vinavyoishi kwenye bahari za kina kirefu. 

Kuishi kimwili ni jukumu. Wewe ni sayari ya viumbe vingine. 

Ndani yako wanakaa maelfu ya viumbe wadogo, wanakutegemea uwalishe, uwape mazingira bora, uwanyweshe, na uubebe mwili kama nyumba yao. 

Kama vile ambavyo dunia inakuhudumia wewe, ndivyo ambavyo wewe unavyohudumia viumbe walioko ndani yako.

Mwili uliumbwa uishi, uwe na majukumu, uchoke, na hatimaye uache kazi katika uzee wake. 

Kifo cha mwili si adhabu, ni kukoma kwa majukumu.

Baada ya hapo, kiumbe kinaingia kwenye mfumo wa pili wa uishi: maisha ya kiroho. 

Huko hakuna masumbufu ya mwili, hakuna mzigo wa majukumu, hakuna kutunza viumbe wengine.

Kila roho inarudi katika hali yake ya asili: uhai, sio uzima. Uzima ni wa mwili, uhai ni wa roho.

Ndiyo maana kuishi kimwili kuna maumivu, kuna mkazo, kuna changamoto, kuna majukumu mazito. 

Baada ya jukumu lako kuisha—ndipo kifo kinafungua mlango wa safari mpya. 

Na ikitokea kiumbe kimekufa kabla ya uzee wake, mara nyingi ni kutokana na bahati mbaya, elimu ndogo ya kutunza mwili, mazingira mabovu, au kushambuliwa na viumbe wengine wabaya, au hata kutolewa sadaka na viumbe wa ulimwenguni wakiwemo watu na majini.

Sasa nyinyi wenye hoja kwamba kifo ni matokeo ya dhambi, hoja yenu iko wapi? 

Dhambi yenyewe iko wapi? Mmeambiwa dhambi zilichukuliwa. Kama dhambi zilichukuliwa, kwa nini mnaendelea kufa kama kuku? 

Au labda zilichukuliwa baadhi, zingine zikaachwa? Uhalisia ndiyo huu: hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kifo cha mwili na dhambi.

Wengi wenu hamjawahi kuasi dhidi ya Mungu kwa sababu hamna hata taarifa sahihi kuhusu Mungu. 

Mnachojua ni simulizi, si nadharia. Ndiyo maana uchambuzi wenu unakuwa mdogo. Mnafikiria kwa imani, si kwa maarifa. Ndio maana hata maswali ya msingi yanakuwa magumu.

Nitamaliza kwa ukweli huu muhimu: mtu huwa hafi. Mwili una uzima, ndiyo maana hufa. 

Roho ina uhai, ndiyo maana haiwezi kufa. Kwa hiyo tafuteni ukweli juu ya maisha ya kiroho - si mnakuja kufa kihasara na kuishia kuwa mizimu isiyo na faida.

Kifupi, kifo ni mfumo wa uumbaji, na ni kila kwa kiumbe kinachoishi kwa jukumu. 

Hakuna elimu ngumu kama elimu ya kuishi, hii elimu inapita elimu ya darasani, elimu ya cheo, na elimu nyingi za kidunia. Ni elimu ya ndani ya uumbaji. Ni elimu ya kuelewa kusudi la uishi.

Wa kuitwa: Mbulwa king’ung’e.

Mawasiliano: 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...