“Tajo 12 za Uwepo Usioishi: Safari ya Kuibua Hekima ya Mungu...”
Nikisema “Amani ya ya Mungu idumu kwetu,” nawe huna budi kuitikia kimoyomoyo kwa kusema; “Idumu - na kwa wengine wote pia,”
Nimeanza kwa kulitaja Jina lake Mungu, Muumba wa viumbe vyote.
Yeye aliyefanya maisha kwa amani na wema, ingawa watu mara nyingi wamemvisha hadithi za uongo, na kumfanya awe mwandishi wa kila baya na kila maumivu yanayotokea duniani.
Kwa kuona jinsi jina lake linavyopotoshwa, nimeona nitoe hili somo, si kwa madai ya kutumwa, maana Mungu hana watumwa, bali kwa sababu Ukuu wake hausimami kwa imani zetu, bali kwa uhalisia wake usiotetereka.
Yeye alifanya maisha bila mashauriano yetu; akaandaa Mfumo ulioanzisha maisha na kutenda kazi Kubwa bila hitaji la ibada, maneno au sifa.
Tulizaliwa tukaukuta huo Mfumo.
Tutakufa tukiwa bado ndani ya huo Mfumo.
Na hata waliotupotosha wao wenyewe waliukuta mfumo, waliishi ndanimo na watauacha ukiendelea hadi mwisho wa uumbaji.
Tuliukuta. Tutaondoka. Lakini Mfumo huo utaendelea hadi ukomo wa dunia na pumzi ya mwisho ya uumbaji wake.
Na kwa kuwa wengi hawajui maadili na ukubwa wa jina “Mungu,” leo nitalifafanua si kwa hoja za mabishano, bali kwa mwanga unaotaka akili ya MTU ifikie utulivu wa kuelewa.
Maana kumpotosha Mungu ni kumpotosha MTU; kumwelewa Mungu ni kujielewa sisi wenyewe.
Asili ya Jina Mungu
Neno Mungu ni jina lililohifadhiwa Afrika ya kati, likitokea kwenye Maneno mawili ya lugha ya kibantu, ambayo ni; munu hungu (Mungu) ikimaanisha Mwenye Vyote.
Na hapa ndipo swali la msingi linakuja: Unayemwita Mungu, ana sifa za Mwenye Vyote, au ana tabia za kiumbe?
Maana kiumbe huhitaji, huchoka, huongea, huishi, hufa, huchukia, hupenda na hutetereka. Lakini Mwenye Vyote hafanani na haya.
Sasa ngoja nitoe tajo 12 zinazomtambulisha Mungu wa kweli, ili uzilinganisha na kile unachokiabudu:
1. Haonekani
2. Haongei
3. Sio mdogo
4. Sio mkubwa
5. Sio mfu
6. Sio hai
7. Sio mume
8. Sio mke
9. Sio mshiriki
10. Sio mmoja
11. Sio wengi
12. Sio kiumbe
Na huu ndiyo ufafanuzi wake...
1. Haonekani - Kwa kuwa hana rangi, hana umbo, hana mipaka. Kiumbe huonekana; Muumba hashikiki. Kama umemuona, lete ushuhuda.
2. Haongei - Hakuna Mungu mwingine wa kuzungumza naye. Sauti tunayoiita “ya Mungu” mara nyingi ni sauti ya roho za viumbe au nafsi zetu zenye huzuni na matumaini.
Ukisema ulinena naye, fafanua hapa mlizungumza nini.
3. Sio mkubwa - Siyo mkubwa kwa kuwa hana mwanzo. Uwepo usioanzia hauwezi kupimika.
Ukubwa na udogo ni viwango vya viumbe; si viwango vya Muumba. Ukisema uliona ukubwa wake, fafanua kwa kipimo gani.
4. Sio mdogo - kwa kuwa hana mwisho. Kama unajua kipimo chake, lete maelezo.
5. Sio mfu - “Mfu” ni mwisho wa maisha ya mwili. Mungu hana mwili, hana roho, hana mwanzo wala mwisho - kwa hiyo si “hai” wala “mfu”. Yuko katika hali isiyolingana na viumbe.
6. Sio hai - “Hai” ni hali inayotumika kwa viumbe wanaotumia roho. Mungu haishi kama viumbe, hatumii roho. Ukisikia roho inakusemesha, hiyo ni roho ya kiumbe, sio Mungu.
7. Sio mume" - Si bwana wala si mzazi. Cheo cha “bwana” ni chetu sisi viumbe, haha, ukiniita Bwana Mbulwa si kosa... “Mume” na “mke” ni nafasi za viumbe wanaozaliana. Mungu hazaliwi, hazai, hana jinsia.
8. Sio mke - Sio bibi, sio mzaliwa. Mungu mwenye mama au kuzaliwa, lazima atafakariwe upya.
Mungu mwenye mama, baba, au mtoto ni kiumbe anayeitwa Mungu kwa utamaduni, si mwenye vyote halisi.
9. Sio mshiriki
Hana watumwa, hana wajumbe, hana waliotumwa kama wahudumu wa uwepo wake.
Ukisema ulitumwa, eleza mlikutana wapi kwenye uumbaji ulioukuta tayari.
10. Sio mmoja
Hawezi kuhesabika kama kitu miongoni mwa viumbe. Hahesabiki. “Huyu mmoja” ama “wale wengi” ni lugha ya viumbe.
11. Sio wengi - Haidadiki, hana idadi. Ndiyo maana wachamungu wa asili hawana neno “miungu.” Mungu yuko nje ya idadi.
12. Sio kiumbe - Kwa kuwa yeye kaumba kwa uwezo na Nguvu Zake. Mungu mwenye mikono, miguu, macho, kiti, eneo au hasira - huyo ni kiumbe aliyebadilishwa kuwa wa kuabudiwa.
Ukitumia akili iliyokuzwa na mama na baba, utaona: Kwa ukubwa wa dunia, jua, mwezi, anga, bahari, mwanga na giza - kuna kiumbe gani kingeumba haya bila kuwa zaidi ya uumbaji?
Kuishi bila kujua ukweli wa Mungu, na kujifunga katika tamaduni zilizojitengeneza baada ya mfumo kuwekwa, ni safari ndefu ya upotevu.
Mungu hana dini, hana kabila, hana taifa, hana watumwa.
Yeye ni UWEPO - usioishi, asiyeanza, asiyekwisha; alifanya vinavyoishi na visivyoishi bila kutegemea shukrani wala sifa.
Uwepo huu haujui hasira, haujui wivu, haujui chuki, haujui furaha, kwa sababu hisia ni za viumbe.
Mungu yuko nje ya ulimwengu wa hisia kama vile mwanga uko nje ya kivuli.
Uwepo wa Mungu hauko kwenye mbegu za maneno, bali kwa utulivu wa kuelewa: Kwamba Yeye ni Mwenye Vyote - na sisi ni wapitiaji wa mfumo ule ule aliouanzisha.
Nasi tubarikiwe na Mungu Mwenye Vyote.
Sende Esupriy Dewo Ochi
Ndimi Mbulwa King'ung'e
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment