“Thamani Haipimwi na Dunia, Inajengwa Ndani Yako...”

Watu wamekuwa wakisema maneno yanayoumiza kama vile, “Usioe mwanamke wa kabila fulani kwa sababu ni chawote,” au “Usiwe na mwanamke mzuri sana sababu hao hawatuli,” na wengine hata kusema, “Usihusiane na asiyeokoka, si mwaminifu.” 

Lakini kabla hatujakubaliana na misemo hiyo, ni muhimu kurudi nyuma kidogo...

Kabla dini hazijaja, kabla miiko ya leo haijatungwa, watu walikutwa wanaishi, wakipendana, wakiishi kwa adabu na makubaliano yao. 

Je, tuseme bibi zetu na mama zetu waliotupatia uzao huu walikuwa “chawote”? Hapana. 

Kwa sababu mtu si kabila lake, mtu si sura yake, mtu si uzuri wake, wala mtu si imani yake. 

Maadili ya mtu hubebwa na mtu mwenyewe.

Tabia ya mtu ni zao la malezi, mazingira, historia za ndani, imani anayoishi nayo, maumivu aliyoyapitia, mitazamo yake na hata maendeleo yake ya kiakili na kiroho - si kabila lake.

Sasa unatoa wapi ujasiri wa kumhukumu mtu kupitia kabila lake, sura yake, au imani yake, ilihali kila mmoja ametengenezwa na safari yake ya aina yake?

Uzuri haumaanishi tabia. Kabila halibebi maadili. Na dini peke yake haizai uaminifu. Kila mtu ana safari yake, ya ndani, ya uchungu, ya mafunzo na ya kukua - safari ambayo haiwezi kuonekana kwa macho ya mtu wa nje.

Niseme jambo moja kwa utulivu na upendo kwa yule ambaye mara nyingine amekuwa akitajwa kama “chawote”. 

Ninakuona. Ninakuthamini.. Na ninajua ndani yako kuna mtu ambaye angependa kueleweka kuliko kuhukumiwa. 

Huenda haujawa hivyo kwa sababu ya uzuri wako, wala kabila lako, wala imani yako. 

Inawezekana kabisa kuna siku uliumizwa na moyo wako ukajaribu kupona vibaya. 

Au labda ulikuwa ukitafuta kuthibitisha thamani yako kwa makosa ya watu waliokuzunguka.

Huenda ulimwengu haukukusikiliza, ukatafuta faraja ya muda mfupi. 

Au hujajifunza kujitambua vya kutosha na ukaingia njia ambazo hukuzipanga. 

Na yote haya hayakufanyi kuwa mtu mbaya - yanakufanya kuwa binadamu.

Lakini kuna ukweli ambao unapaswa kuufahamu kwa upole. 

Unapojitoa kupita kiasi kwa watu wengi, haimaanishi unathaminiwa zaidi; mara nyingi ina maana unajinyima thamani yako mwenyewe.

Fikiria big G ikiwa inaliwa na mtu mmoja, ladha yake hubaki. Lakini ikiliwa na watu kumi, haina thamani tena. 

Mfano huu si kejeli, ni mwanga wa kuona namna mtu anavyoweza kupoteza uzito wake binafsi anaporuhusu dunia imtumie kupita kiasi.

Ukweli ni kwamba wewe si mali ya umma. Wewe si zawadi ambayo kila mtu ana haki ya kuijaribu.

Wewe ni mtu mwenye thamani, mwenye utu, na mwenye uwezo wa kuishi maisha ya thamani. Thamani ya mtu huzaliwa kutokana na kujitunza, kujipenda na kujijua.

Bibi zetu hawakuwa wa kipekee, lakini walikuwa na misingi iliyowafanya walindwe na wathaminiwe. 

Na wewe unaweza kurudi kwenye misingi yako wakati wowote unapochagua. 

Kila siku mpya ni nafasi ya kujenga upya, ya kujirudishia utu wako na ya kubeba thamani inayokustahili.

Ninakuambia haya si kwa kukukosoa, bali kukukumbusha kwamba bado unaweza kutulia. Bado unaweza kubadilika. 

Bado unaweza kuwa mtu ambaye moyo wake unaeleweka, unaadabiwa na unathaminiwa. 

Na wakati utakapokutana na anayekupenda kwa dhati, ataona thamani yako ya ndani, si makosa ya jana wala hukumu za watu.

Usiwe mali ya umma. Jifunze kutulia. Jifunze kujitunza. Jifunze kujijali. 

Kwa sababu ndani yako kuna mtu mzuri anayeweza kung’aa zaidi kuliko unavyofikiri - na huo uzuri unaanza na wewe mwenyewe.

Ndimi Mbulwa King'ung'e 
Mawasiliano: 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...