USIISHI KWA SABABU ZA WENGINE KAMA HUJAZIELEWA SABABU ZAKO


Anayekusukuma ufanye jambo fulani mara nyingi huwa hakuambii kwa upendo, bali kwa kutaka kukuona ukifanana na wengine.

Anajisitiri nyuma ya neno ushauri, ili siku ukiharibikiwa, akae pembeni akucheke kimya kimya.

Utasikia wakisema: “Umri umeenda, oa/olewa—unasubiri nini?”

“Wenzako wa umri wako wamejenga, wana familia, wana maisha—na wewe je?”

Wanaposema hivyo, hawajui jambo moja muhimu sana: kila MTU ana sababu zake za kuishi, na sababu hizo hazifanani.

Tofauti hizo si kasoro—ndizo zinazokamilisha uhai wa sisi Watu.

Sababu za UWEPO wangu si sawa na zako.

Ninachokifanya mimi hapa si kila MTU anaweza kufanya.

Na hilo lina maana moja tu: zipo sababu maalumu zinazonizunguka zinazonilazimisha nifanye ninachofanya.

Nimesoma na wenzangu shule ya msingi, hawafanyi ninachokifanya.
Sekondari—hawafanyi.
Advance—hawafanyi.
Chuo—hawafanyi.
Wafanyakazi wenzangu—hawafanyi.
Hata tunaokaa nao—hawafanyi.

Kiufupi, wananishangaa.
Wamebaki midomo wazi.
Wananiona si MTU wa kawaida.

Kuna mambo nikiyasema yanawatikisa watu, hadi viongozi wakubwa.

Kwa nini? Kwa sababu nipo ndani ya sababu zinazonizunguka. Ndiyo maana nayasimamia haya.

Hili ni jambo langu.
Nikiliacha nikafuata mashauri ya Fulani, natoka nje ya sababu za uwepo wangu.

Sasa jiulize: Wewe unayemshinikiza mwenzako afanye jambo fulani kwa sababu wengine wamefanya — unajua sababu zinazomzunguka MTU huyo?

Na wewe unayeshinikizwa na kila MTU — je, utaendelea kuishi kama bendera inayofuata upepo?

Unajua sababu za UWEPO wako?

Ulishawahi kutafakari kwa kina: ni sababu zipi zipo nyuma ya pazia za kila jambo linalotokea katika maisha yako?

Kuna wakati maisha yanahitaji utulivu wa NDANI, wakati wa kujinyamazisha, wakati wa kujisikiliza WEWE, si kuwasikiliza wengine hadi ujisahau mwenyewe.

Hakuna hali inayomtokea MTU bila sababu.
Kila hali unayopitia ina mizizi yake, ina chanzo chake, ina maana yake.

Ndiyo maana si busara kukurupuka, wala kuishi kwa shinikizo la watu, bila kujifunza kwanza.

Ngoja nikuoneshe uelewe zaidi: Kuna Watu hawaolewi si kwa sababu hawataki, bali kwa sababu wako kwenye vifungo vya kiroho.

Huyu asipotulia, ajifunze, ajue chanzo cha hali yake, hata ukimshinikiza vipi, si rahisi kufanikiwa kuolewa.

Kuna Watu kila mahusiano yao yanavunjika, kila ndoa inaishia maumivu, kwa sababu kuna roho zinazowavuruga.

Huyu usimshinikize wala usimcheke—bila elimu ya sababu, ataendelea kuanguka.

Kuna Watu hawafanikiwi kwenye biashara zao,
si kwa kukosa juhudi, bali kwa sababu kuna roho zinazovuruga mafanikio yao.

Kila biashara wanayoanzisha inaanguka. Huyu hatakiwi kulaumiwa, bali kusaidiwa kuelewa sababu zinazomrudisha nyuma.

Nimeandika makala hii si kwa ajili ya kuwashambulia watu, bali kukufundisha wewe unayewacheka wenzako, unaowaona kama wamechelewa, kama wapo nyuma ya wakati.

Unawanyooshea vidole, wakati huna elimu ya kiroho, hujui kwa nini mambo yanatokea, wala hujui sababu zinazovuruga maisha ya watu.

Usitoe shinikizo.
Usimcheke MTU.
Yaelewe maisha kwanza.

Ukianza kuyaelewa maisha, utaacha maisha ya lawama, utaacha maisha ya kejeli, utaacha kujifanya unajua kila kitu.

Na ndipo utaelewa kwa nini ninaandika kuhusu:
Utambuzi binafsi, ukombozi wa fikra, na masuala ya kiroho.

Nafanya haya yote kwa sababu nimeyaelewa MAISHA kwa ujumla wake na kwa undani wake.

Usimcheke MTU wakati wewe mwenyewe hujui kwa nini MAISHA yapo wala hujui kwa nini unaishi.

Usiingie kwenye huu mtego.

Wakuitwa: Mbulwa King’ung’e
Mawasiliano: 0744 284 329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...