USIKUBALI MADENI YAONGOZE MAISHA YAKO...



Kwa muda mrefu sana tumezoea kusikia msemo huu: “Usiogope kukopa, hata serikali inadaiwa… wewe ni nani usidaiwe?”

Ni msemo maarufu, wa kishujaa kwa kusikika -lakini kwa ndani unaumiza, hasa pale mtu anapozongwa na madeni na hana tena mwelekeo wa kifedha.

Ukweli mchungu ni huu: Wengi wamefikia hatua ya kukopa ili kulipa deni jingine, yaani mzunguko hatari unaowafanya waishi kama mateka wa madeni.

Unakuta umemuahidi mdeni wako kuwa kesho utamlipa. Lakini unajua wazi huna pesa. 

Presha inakuja, usingizi unapotea, na unachokifanya mwisho wa siku ni kukopa kwa mtu mwingine ili kufunika shimo moja na kufungua jingine.

Hii ni hatua mbaya sana katika maisha.
Inakugeuza kuwa mtumwa wa madeni, unafanya kazi si kwa ajili ya kujenga maisha yako, bali kulisha madeni. 

Ndipo ndoto zako zinakuwa mbali na ukuaji wa kiuchumi unadumaa.

Ukianza kufanya kazi ili kulipa madeni badala ya kujenga mustakabali, unakuwa umeingia kwenye aina fulani ya utumwa wa kisasa.

Kipato chako kinachoshikika kinaenda kwa wanaokudai, na hata ndoto zako zinakuwa mbali kwa sababu kila siku unaanza upya kwenye sifuri.

Kwa tafsiri fupi, Deni ni kutumia zaidi ya kipato chako.

Na hata kama hutumii zaidi ya unachopata, ukikosa mfuko wa dharura, tukio dogo tu linakubomoa na unalazimika kukopa. Hapo ndipo mtego wa madeni unapokuanz­ia.

Na ukweli ni kwamba dharura haziwezi kukosekana; zinaweza kugonga wakati wowote - hospitali ghafla, sherehe isiyopangwa, gari kuharibika, kukosa ada ya mtoto, au hata kupoteza chanzo cha kipato.

Na pale huna akiba… njia inayobaki ni kukopa.

Nakubali kabisa: kipato kinaweza kuwa kidogo.

Lakini mtu mwenye nidhamu ya kifedha, bajeti, na mpangilio anaweza kuishi ndani ya kiwango chake na kuendelea kusonga mbele.

Leo nakupa mbinu mbili rahisi lakini zenye nguvu zitakazokusaidia kuepuka madeni yasiyo ya lazima na kukupeleka kwenye uhuru wa kifedha.

1. Jua kiasi kinachohitajika na kigawanye kwa muda uliopo

Ili kuepuka kwenye madeni hususani katika kuwekeza au kufungua mradi fulani.

Anza kwa kujiuliza: “Nahitaji kiasi gani?”
“Nina muda gani kufikia kiasi hicho?”

Ukishajua, tengeneza mpango wa kuweka akiba kidogo kidogo kulingana na muda uliopo.

Mfano: Unataka kufikia mwezi Desemba 2026 uwe umekusanya 10,000,000/=*l kwa ajili ya mtaji wa biashara.

Hatua zako ziwe:

Jua muda uliobaki
Gawa lengo lako kwa idadi ya miezi au wiki
Amua kiasi utakachotenga mara kwa mara
KAA KWENYE MPANGO - bila kurudi nyuma

Ukifika muda uliojipangia, utakuwa tayari unacho unachokihitaji bila kuomba, bila kukopa, bila kuumiza kichwa.

2. Tenga asilimia ya kipato chako kulingana na muda wa lengo

Hii ni kanuni rahisi lakini yenye matokeo makubwa.

Tenga angalau 10% – 20% ya kipato chako kwa kila mapato unayopata.

Kwa mfano: Kodi yako ni 150,000 kila baada ya miezi 3.

Unaweza kufanya mojawapo:

A) Weka 5,000/= kila siku — ndani ya mwezi mmoja tayari unayo kodi.

B) Weka 2,000/= kila siku — ndani ya miezi 3 utakuwa umefikia 180,000/=, zaidi ya unachohitaji.

Tazama unavyouondoa kabisa uwezekano wa kukopa.

Ni nguvu ya mpangilio rahisi lakini wa kimkakati.

Matokeo yake? Hakuna hofu, hakuna kukopa, hakuna presha.

HITIMISHO
Hakuna atakayekusaidia kupanga maisha yako ya kifedha isipokuwa wewe.

Cho chote kitakachohitaji pesa, ikiwa ni ada, kodi, sherehe, dharura, biashara, au ustawi, ni Wajibu wako.

Na njia hizi mbili ndizo zinakuzuia kuishi maisha ya madeni yasiyoisha.

Ukizipuuza, uwezekano wa kuangukia kwenye madeni ni mkubwa.

Lakini ukizifuata kwa nidhamu, hakuna lengo utashindwa kufikia.

Tumia kanuni hizi leo — si kesho.
Jiokoe na jiandae kwa maisha yenye uhuru wa kifedha.

Ndimi,Mbulwa King'ung'e

Founder – King Mentorship Program

Kwa ushauri zaidi wasiliana NAMI: 0744 284 329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...