“Waonjaji Wamepoteza Ladha, Sasa Ni Wakati Wetu Wa Kuamka...”


Siku hizi mambo yamebadilika sana, kwani hata matunda nayo yamekuwa tayari kuonjwa na waonjaji kabla ya kuhifadhiwa kabatini. 

Inashangaza sana. Sijui tunaenda wapi kama hata matunda yanataka kuliwa kwanza ndipo yahifadhiwe…

Mimi mwenyewe nipo nashangaa TU naona ule usemi wetu unaosema; “mbuzi kafia kwa muuza supu, ukitimia...

... hahaha waone wanywa supu wanavyocheka.” Ni ujinga tu, lakini ndiyo hali halisi ya leo.

Eti matunda yanadai na yenyewe yanataka kuonjwa kwa sababu walaji nao siku hizi midomo yao haifanyi kazi, kana kwamba midomo ipo kwa ajili ya kuzungumza tu. 

Haya mambo hayatakaa sawa. Zamani waonjaji walikuwa wanahofia kuuziwa mbuzi kwenye gunia.

Ulikuwa unaweza ukanunua mbuzi, kumbe ule mfuko wa kuhifadhi upepo umetoboka au umeharibika. 

Sio kwamba waliumbwa hivyo na Mungu, hapana ni makosa ya mahesabu wakati wa kuonjwa. 

Upepo ulipojaa, puto likavimba, aliyesababisha puto akasema siwezi kulea, aliyebeba puto akasema; "wakati ulikuwa bado," katika harakati za kupunguza upepo mambo yakaharibika. Mwisho mtu anabaki kuwa “kopo”. 

Sina MAANA kwamba WOTE wapo kwa sababu ya hilo, ila matatizo mengi ni matokeo ya ujinga wa kutokujua...

Usifikiri nazungumza kwa masihara. Hapana. Nauliza: kwanini tumefika huku? Tunaelekea wapi? Kwanini tunaharibiana maisha? Kwanini tunakuwa sehemu ya uharibifu huo? Na kwanini tunakubali kuharibiwa?

Wazazi mko wapi? Wakemeaji mko wapi? Wokovu mnaoutangaza uko wapi?

Ni nani wanafanya haya? Wapagani? Hapana, ni sisi wenyewe!

Tuendelee tu, utanielewa.
Mwili una mahitaji yake kama vile njaa. Ukiwa na njaa husemi “njaa shindwa”, unakula. 

Kwa hiyo kwa nini mwili ukihisi mahitaji ya kihisia tunakemea na kutishia watu dhambi badala ya kuwapa misingi ya namna ya kuishi na kujidhibiti wakati huo?

Hisia kila mtu anazo.
Maneno ya “huyu ana pepo la ngono” yanatoka wapi, wakati mtu akiwa na njaa hamsemi ana “pepo la njaa”?

Ninachotaka kusema ni kwamba: muwape watoto na vijana wenu misingi.

Vijana wanaharibikiwa kimaisha. Hawana matumaini. Waonjwaji na waonjaji wote hawaamini kinachoendelea. Wamebaki tu midomo wazi.

Wazazi mko wapi? Amkeni.

Zamani mambo haya hayakuwepo.
Tunda halikuonjwa wala waonjaji hawakuonja bila ridhaa ya wazazi. Kulikuwa na misingi. Hawakuvuka mipaka hovyo.

Sasa hivi misingi imeharibika kuanzia shuleni.
Anayemfundisha mtoto wako ndiye mharibifu wa kwanza si wa kiume si wa kike. (Sina MAANA WALIMU wote wanafanya haya, WALIMU mnisamehe mimi ni mwalimu mwenzenu...  )

Na ajabu ni kwamba elimu wanayopewa haiwajengi, haiwapi thamani; inawapa tu karatasi inayoitwa cheti.

Kwenye imani nako, watu wamegeuzwa kuwa kondoo. Ijapokuwa watu ni watu; kondoo ni kondoo.

Waongoza kondoo wanawala wale kondoo wasiojielewa... (Tusameheane, sina maana ni wote, kila MTU nafsi yake imsute...)
 
Kondoo nazo zinamalizana makundi kwa makundi... (Enyi kondoo mnisamehe, mwandishi anafoka, basi nafsi yako ikusute😅...)

Mwisho wa siku wanaishia kusema: tulianguka, tutatudu, tutaendelea…

Mashuleni huko, damu ni moto. Vijana wanamalizana.

Wasanii nao hawajatuacha salama - wanaharibu watoto wetu. Kila mahali uharibifu umejaa.

Zamani elimu haikuwa ndefu kama ya leo, lakini ilitoa misingi.

Sina maana kwamba turudi huko, hapana.
Tujulize tu: tunafeli wapi?

Binti alipofikisha miaka 15 aliruhusiwa kuolewa.
Sisemii tufanye hivyo leo.

Ninachotaka ni ufanye mahesabu: kutoka miaka 15 hadi 30 - leo mtoto anaishije huku tunakemea tu bila kumpa mwongozo?

Kijana wa kiume alikuwa anaweza kuoa akiwa na miaka 18.

Alikuwa na uwezo wa kumudu familia.
Na hawakunua viwanja, walikuwa wanapewa maeneo na kuanza kuishi.

Sasa fikiria: kama wao walianza kwenye umri huo, hawa vijana wa leo wanaishije tunaposema tu “wakemeeeni!” bila kuwasaidia? Jaribu kuvaa viatu vyao basi, vimekutosha?

Nimeandika kwa masihara ila MOYONI nina maumivu makali sana, vijana wetu wengi hawajitambui...

Na hata wasomi nao bado hawana Ukomavu wa kifikra, tunahitaji kuwapa vijana wetu Elimu ya maisha na si kuishia kuwapa elimu ya darasani tu...

Jamii tukubali: tumefeli.
Tujitathmini.
Tujirekebishe.

Kuonja wala kuonjwa hakufai.
Sikubaliani nalo.

Lakini tusikemee tu - tuwapende vijana. Tuwape misingi.

Hata mimi nawapenda sana.

Ndimi Mbulwa King’ung’e
Mawasiliano: 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...