“Wewe Ni Nani Katika Mnyororo wa Tumaini la Maisha?”
Maisha yamejengwa juu ya kanuni moja kubwa: kusaidiana.
Hakuna kiumbe kinachoweza kuishi peke yake. Hakuna aliyejitosheleza.
Kila nafsi, kila uhai, kila pumzi, vyote vimefungamanishwa ili kuendeleza muendelezo wa uhai.
Na ifahamike kuwa, Mungu huwa haingilii maisha ya kiumbe moja kwa Moja, lakini mambo aliyoyaumba ndiyo yanashikamana kuendeleza maisha.
Huo ndiyo muujiza wake mkuu, muujiza wa mfumo, si muujiza wa upendeleo.
Muujiza unaohakikisha kwamba chochote kilicho hai kina nafasi katika dunia hii.
Kama mambo ya Mungu yanatupa msaada wa kuishi, maumbile yake, sheria zake, pumzi, ardhi, mvua na uhai, basi sisi watu tunapaswa kuwa mwendelezo wa msaada huo.
Mungu anatoa chanzo cha uhai, lakini wanadamu wanatoa muunganiko wa safari ya uhai. Yeye hatushiki mkono moja kwa moja, lakini ametupa uwezo wa kushikana sisi kwa sisi.
Hivyo msaada wa Mungu hutupa uhai; msaada wa watu hutupa matumaini. Mambo ya Mungu hutuwezesha kuishi, lakini watu ndio hutusaidia kuishi kwa maana.
Na ndiyo maana kiumbe kinapokosa msaada, kinapoteza matumaini.
Kwa sababu matumaini hayaji kutoka angani - yanatoka kwa viumbe vinavyoishi.
Ndiyo maana matumaini yote huwekezwa katika viumbe vinavyoishi.
Matumaini ni kivuli cha msaada: ukiondoa msaada, kivuli hupotea; ukipanga upya msaada, tumaini hurudi.
Hata ulimwengu wa biashara unatupa picha hiyo hiyo:
Mfanyabiashara anayeuza bidhaa, tumaini lake liko kwa mwenye kiwanda.
Mwenye kiwanda tumaini lake limo kwa anayezalisha malighafi.
Muuzaji tumaini lake limo kwa mteja.
Na mteja tumaini lake limo kwa muuzaji.
Na mnyororo huu unaendelea bila ukomo.
Hapo ndipo tunaona kuwa matumaini ni aina ya msaada, na msaada wenyewe upo katika namna mbili:
Msada wa bure, na msaada wa gharama.
Msaada wa bure hujengwa juu ya moyo; msaada wa gharama hujengwa juu ya kuendeleza huduma au fani ili iwafikie wengi zaidi.
Hapa ninachokupa ni msaada wa bure wa maarifa.
Lakini mtu akitaka kujiunga na King Mentorship Program, atapata msaada wa utambuzi binafsi kwa gharama fulani, ili taaluma, huduma, na hekima ifike kwa wengine zaidi ya mmoja.
Kwa maana kama fani haiungwi mkono, hutoweka.
Na kama huduma haitiliwi thamani, hufa.
Sasa fikiria: kama unachokifanya hakipokelewi, hakithaminiwi, wala hakiungwi mkono, utakuwa na tumaini la kweli?
Una bidhaa nzuri lakini huna wateja…
Una huduma nzuri lakini huna wanaokuthamini…
Una juhudi, lakini nguvu zako hazina mwitikio…
Kila unachojaribu kinaenda kinyume…
Ni ngumu sana kuwa na tumaini.
Na hii ndiyo changamoto inayoikumba dunia ya leo: watu wengi wamepoteza matumaini kwa sababu hawapati msaada, wa bure wala wa kugharamia.
Sina maana kwamba usimtegemee Mungu, lahasha!
Kila kiumbe kinamtegemea Mungu, si kwa msaada wa moja kwa moja, bali kwa sababu kinaishi ndani ya mfumo wake: mambo yake, ulimwengu wake, sheria zake.
Lakini swali kubwa ni hili: Je, wewe ni msaada kwa mwingine?
Je, wewe ni mke ambaye mume anaweza kuweka tumaini kwake?
Je, wewe ni mume ambaye mke anaweza kutegemea?
Je, wewe ni mfanyabiashara au mtoa huduma anayejenga tumaini la mteja?
Je, wewe ni mteja ambaye mtoa huduma anaweza kukutumainia?
Je, uwepo wako unaleta uzima, au uzito?
Maisha ni mfumo unaokamilika kwa mema.
Tumeumbwa kukamilishana, si kuumizana.
Tumetengenezwa kupeana tumaini, si kuondoleana nguvu.
Unapomaliza kuisoma makala hii, jiulize kwa uaminifu: Kuna mtu anayejivunia uwepo wako?
Au kuna mtu anayefifia kwa sababu ya wewe?
Kila mtu ni muhimu.
Kila mtu anapaswa kuwa tumaini kwa mwingine.
Na pale unapoanza kuwa kikwazo badala ya kuwa daraja, basi ndipo maisha yako yanapoanza kupoteza maana yake ya ndani…
Kwa hiyo jukumu letu ni kuwa daraja, sio kikwazo; kuwa tumaini, sio mzigo; kuwa mchango wa mwanga alioutoa Mungu, sio kivuli kinachouzuia.
Ndimi,
Mbulwa King’ung’e
Mawasiliano: 0744 284 329
Comments
Post a Comment