CHANZO CHA UHAI, UWEPO, NA KUSUDI LA MTU...

Kwa muda mrefu nimekuwa nikitafakari swali moja kubwa linalowakabili watu wote, bila kujali rangi, taifa, au dini: Kwanini tupo, na kwanini tuliumbwa?

Hili si swali la kawaida. Si swali la kujibiwa kwa sentensi nyepesi zisizo na mashiko au majibu ya kukariri. 

Ni swali zito linalomlazimu mtu kutuliza fikra, kuchunguza kwa kina kila hoja, kila andiko, na kila simulizi.

Linahitaji muda wa kusoma kwa makini, kutafiti kwa uangalifu, kutafakari kwa kina, na hatimaye kurudi na majibu yaliyo fasaha—si majibu ya kukariri au kurithiwa.

Ni swali linalodai ujasiri wa kuhoji yaliyozoeleka, pamoja na nidhamu ya kuchunguza hoja zote—za kidini, za kifalsafa, na za kiutu—bila woga, bila upendeleo.

Lengo la tafakuri hii lilikuwa moja tu: Kufahamu kusudi la uwepo wa watu kwa ujumla, na kusudi la kila mtu binafsi.

Tunaishi katika ulimwengu wenye msongamano wa hoja kiasi kwamba utu wa Watu umefifia. 

Leo, watu wako tayari kuumiza, kutawala, hata kuua wenzao, wakidai kuwa mamlaka yote wanayoyatekeleza yametoka kwa Mungu, na kwamba vitendo hivyo ni ushahidi wa kumtumikia Mungu.

Wengine wanaishi katika minyororo ya kifikra—wanateseka, wanatumikishwa, na wanaishi bila uhuru wa ndani.

Wengi hawajui: kwanini maisha yapo, kwanini kifo kipo, wala maisha ya kiroho ni nini na huishiwa vipi.

Badala yake, wamekubali kuishi ndani ya mifumo ya fikra waliyoikuta, bila kuhoji chanzo chake, uhalali wake, wala matokeo yake.

Ndipo nikaanza safari ya kuchunguza chanzo cha uhai chenyewe.

Chanzo hiki kinaelezewaje? Kipoje? Na kwa nini kiliamua kuumba maisha?

Nilitambua jambo moja muhimu: kuna dini nyingi, falsafa nyingi, na simulizi nyingi—lakini zote zinajaribu kuelezea chanzo kilekile kwa majina na mitazamo tofauti. 

Miongoni mwa majina hayo, lipo jina linaloweza kutumika kwa viumbe vyote vinavyoishi, si kwa watu pekee.

Majina mengine yanahusishwa na viumbe vilivyoumbwa na chanzo hicho, lakini baadaye vikajitwika nafasi ya kudai kuwa ndicho chanzo chenyewe. 

Ikumbukwe kwamba chanzo cha maisha hakihubiri wala hakijitangazi; kilifanya uumbaji bila kusema, bila kutangaza, bila kujieleza.

Majina mengine ni viumbe vilivyogeuzwa kuwa viabudiwa na viumbe wenzao. 

Mengine ni mifumo ya habari za uzushi kuhusu chanzo cha maisha, iliyoenezwa kutoka sayari moja hadi nyingine. 

Mengine ni miundo ya kiakili iliyobuniwa na watu, na mengine ni tafsiri zilizorithishwa kizazi hadi kizazi bila kuchunguzwa kwa kina.

Somo hili halilengi kubomoa imani, bali kurejesha. 

Kuna kuishi kiusawa, na kuna kuishi kiufasaha.

Huwezi kuishi kwa ufasaha bila kufahamu chanzo chako. Bila uelewa huo, maisha yanakuwa ni mfululizo wa kuiga, kuogopa, na kutii—bila maana ya ndani.

Kabla ya maisha kuwepo, kulikuwepo UWEPO.

Katika lugha ya Kibantu, Uwepo huu uliitwa “vradiens kimiadd.”

Haukuwa “Mungu” kama jina, kwa sababu jina hilo linahusiana na tendo la kuumba. Kabla ya uumbaji, hakukuwa na hitaji la jina.

Jina Mungu lilianza kutumika baada ya uumbaji, pale MTU wa kwanza alipoumbwa na mambo ya Mungu na baadae kufahamishwa kuhusu Jina Mungu kupitia choo-i.

MTU huyo alifundishwa na choo-i, yaani muujiza wa Mungu ambao hukisemesha kiumbe cha Kwanza TU kufanywa na mambo ya Mungu kwa kukipa elimu juu ya uwepo wake na jambo lililomhusu.

Baada ya uumbaji ndipo dhana ya “Mungu” ilipojitokeza—si kama kiumbe, bali kama Mwenye vyote. 

Huu ndio msingi wa neno Mungu katika mizizi ya lugha ya kiutu (Kibantu), likitokana na muunganiko wa maneno "munu hungu" yanayoashiria mmiliki wa vyote vilivyopo.

MTU wa kwanza alizungumza lugha ya Kibantu. 

Alizaa watoto 168 waliotawanyika katika mabara yote saba; katika kila bara, uzao wake uliendelea kupitia mapacha wa kiume na wa kike, akizaa katika nchi za asili kumi na mbili. 

Watoto hao walibaki katika maeneo hayo, wakiendeleza kizazi hadi watu wa leo kupatikana. 

Piganeni. Uaneni. Bishaneni. Vunjaneni. Nyonganeni. Ninyi wote ni ndugu. Sema nini hamjui chanzo chenu.

Hakuna aliyemea kama uyoga. Ninyi ni mwendelezo wa uzao wa MTU wa kwanza na mke wake.

Watu wa leo si tukio la bahati nasibu. Ni mwendelezo wa kizazi. Ni matokeo ya mchakato mrefu wa maisha unaoendelea.

Watoto wote walizungumza lugha ya Kibantu katika mabara yote saba. Hata Antarctica ilikuwa na watu—lakini sitafafanua hapa kilichotokea mpaka leo ikaonekana haina watu.

MTU wa kwanza aliwafundisha watoto wake kuhusu Mungu, na aliwafundisha sala aliyofundishwa kwa muujiza wa Mungu kupitia choo-i.

Sala hiyo ninayo, na sisi wachamungu halisi tunaitumia kila asubuhi na jioni. Ukihitaji, nitakutumia—lakini kwa sharti moja: unitumie sala ya MTU wako wa kwanza.

Haya ni mambo ya zaidi ya miaka milioni 12 iliyopita. Kwa hiyo wewe unayetegemea historia ya miaka 7,000 au 2,000, usianze kuomba rejea—kwa sababu kuandika na kuchapisha kulianza juzi tu.

Hata hivyo, MTU wa kwanza alifundishwa kuandika, kuhesabu, na kupanga muda. Ndiyo maana hesabu ya miaka ilianza kwake. 

Kwa mujibu wa kalenda ya jadi, tangu afe MTU wa kwanza, sasa tupo mwaka wa milioni kumi na moja na kuendelea.

Wewe unayeishi kwenye mwaka 2026, jiulize: Nani alibadili mfumo huu, na kwa nini?Je, hutaki kutuliza kichwa na kusikiliza?

Neno Mungu limetokana na lugha ya kiutu (Kibantu):munu + hungu = Mwenye vyote

Vyote ni vya Mungu. Wewe una vichache, kwa Mwenye vyote.

Hitimisho la SoMo la leo ni hili: Nenda ukatafute maana ya: God, Kyala, Jehovah, Allah, Baba, Roho, Bwana, Mfalme na majina mengine mlioupa huo UWEPO.

Uone kama yote yanamaanisha Mwenye vyote.

Utakapoanza kuelewa Mungu kutoka kwenye mzizi wa Chanzo cha Utu, utaanza kuelewa maisha.

Hapo ndipo migogoro ya kidini huanza kuyeyuka, kwa sababu chanzo ni kimoja, ila tafsiri ndizo nyingi.

Msishangae kwanini mnachanganyana—bado hamjamjua Mungu.

Nitawafundisha kuhusu Utu wenu.Nitawapa mambo ambayo hakuna mzungu wala muarabu aliyewahi kusema, wala atasema.

Kesho nitarudi na SoMo kuhusu Roho. Tutaelewana tu.😎😎

Ndimi Mbulwa King’ung’e. 

Mwalimu wa Maisha na Mambo ya Mungu. Founder, King Mentorship Program.

Mawasiliano: 0744 284 329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...