JE, MAANA YA MAISHA IKO WAPI...?
Leo nilikuwa nimetulia chini ya mti wa mwembe, nikifurahia kivuli chake na upepo mwanana uliokuwa ukipita taratibu. Katika utulivu huo, akili yangu ilianza kutafakari kuhusu maisha.
Nikatazama hali ya binadamu—namna anavyohangaika, anavyoteseka, na anavyopambana na maisha yenyewe. Ndipo swali la msingi likazaliwa moyoni mwangu:
Maana halisi ya maisha iko wapi? Maisha yalianzaje? Kwa nini yapo?Je, yaliumbwa ili watu watumiane na kutesana?
Kwa sababu, kwa asilimia kubwa, hatufaidiani bali tunatesana, tunanyonyana na tunakandamizana badala ya kujengana.
Tunaishi kutetea hadhi tulizonazo, badala ya kujali, kuadabia, na kuthamini utu wa wengine.
Kabla sijapata jibu kamili, mawazo yangu yakahamia kwenye madaraka, vyeo, na fursa za kumiliki wengine. Nikajiuliza:
Je, maisha ni kuwa na madaraka makubwa, cheo na hadhi ya juu? Na kama ni hivyo, madaraka hayo yalianzaje, na kwa lengo gani hasa?
Kwa nini karibu kila sehemu ya dunia kuna mifumo ya kutawala, kusimamia na kudhibiti mawazo na fikra za watu hata kama ni nzuri?
Kisha nikatafakari kuhusu pesa.
Je, maisha ni kuwa na mali nyingi?
Kama si hivyo, kwa nini kwa sababu ya pesa tunafanya maovu, tunadhalilishana, tunaharibiana maisha, na wakati mwingine tunaua?
Nikajiuliza tena: Je, maisha ni kuwa na elimu kubwa, shahada nyingi na utaalamu wa hali ya juu?
Kama ndivyo, ni nani aliyeweka vigezo hivyo vya thamani ya maisha?
Na kwa nini basi, miongoni mwa wasomi wengi, bado kuna watu wasioelewa maana ya maisha zaidi ya taaluma walizosomea?
Je, maana halisi ya elimu tunayojivunia ni ipi hasa? Elimu ipo kwa ajili ya nini—kutengeneza wataalamu tu, au kuwafanya watu waelewe maisha yao?
Na tukirudi nyuma zaidi: Ni nani alikuwa mwalimu wa kwanza? Na ni nini hasa alichofundisha mwalimu huyo wa kwanza?
Nikajiuliza pia kuhusu umaskini na maisha magumu.
Je, maisha ni kuridhika na umaskini? Au kwanza tujiulize: umaskini ni nini hasa?
Na wale walioishi kabla ya kuanzishwa kwa pesa na mifumo ya kisasa ya maisha—je, tuseme walikuwa maskini? Au waliishi kwa kipimo tofauti cha thamani ya maisha?"
Huenda tatizo si umaskini wenyewe, bali ni sisi kushindwa kufikiri upya kuhusu kile tunachokiita utajiri.
Kadiri nilivyozidi kutafakari, nikaona wazi kuwa kuna mifumo iliyoundwa ili kusimamia maisha ya watu kwa njia ovu...
Nikajiuliza tena: Ni nani aliyeandaa mifumo inayosimamia na kutawala fikra za watu ulimwenguni kote?
Kwa sababu inaonekana kana kwamba tumeandaliwa kwa mfumo mmoja tu:
Soma ➡️ pata kazi ➡️ lipwa ➡️ endelea kuishi.
Swali likabaki: Je, kazi hizi ndizo maana halisi ya maisha yetu? Au tunazifanya kwa sababu tu tumetengenezewa tuzifanye?
Sikupata jibu.
Nikajiuliza zaidi:
Kama kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu Mungu—anayesemekana kuwa chanzo cha uhai—tutawezaje kuelewa kwa undani sababu ya kuwepo kwa maisha?
Dini moja inasema hiki. Nyingine inasema kile.
Asili, falsafa, na makundi mbalimbali yanatoa tafsiri zinazotofautiana.
Ni wapi basi tutapata ukweli wa pamoja kuhusu maana ya maisha?
Nikashuhudia hali ambapo mtu yuko tayari kumwangamiza mwenzake kwa sababu tu hawashiriki imani moja.
Nikajiuliza: Je, hilo ndilo lengo la maisha? Je, dini ipo kwa ajili ya kulinda uhai au kuuharibu?
Kama tunaweza kuharibu maisha ya wengine kwa jina la Mungu, basi tunapaswa kujiuliza kwa ujasiri:
Ni Mungu yupi anayegawanya watu katika makundi yanayoharibiana na yasiyopatana kwa hoja?
Na miongoni mwa makundi hayo, dini yake ni ipi ili tujue humo ndimo maana ya maisha ilipo?
Nikatazama mifumo ya elimu duniani.
Nikaona wazi kuwa watu wengi wanaandaliwa kuwa wataalamu, si waelewa wa maisha.
Swali likazidi kuwa zito:
Kama wote tunaandaliwa kuwa wataalamu wa kazi, ni nani atakayesimamia utu wa ninyi Watu?
Hapo ndipo nilipohisi uzito mkubwa moyoni.
Nilihuzunika...
Nikagundua kuwa tumefundishwa kuwa wakatili, kudhulumu, kukandamiza na kunyonya—si kwa sababu ni asili yetu, bali kwa sababu mifumo imetufundisha hivyo.
Tumetengenezwa kuwa wafanyakazi wa mifumo, badala ya kuwa walinzi wa utu wa Watu.
Ndipo nikajiuliza swali la mwisho:
Ni nani basi atakayewafundisha watu kuhusu maisha halisi, ikiwa wamejivika ubatili wakiuita ndiyo ukweli wa KUISHI?
Ndipo nafsi yangu ikaniambia: ni wewe. Kwa sababu una elimu ya MTU wa kwanza—elimu isiyotokana na vitabu pekee, bali na uelewa wa maisha yenyewe kama yalivyofanywa na Mungu mwenye vyote.
Na Ndiyo maana hadi unaandika makala hii: hakuna aliyesimama, hakuna aliyeliona hili.
Na sauti ya ndani ikasema tena: Wewe ndiye una wajibu. Simama. Nenda. Kawafundishe watu ukweli wa kuishi kiutu.
Kwa sababu ninyi watu mpo duniani ili kukamilishana, si kuharibiana.
Kwa MAANA hiyo, ukiujua utu wako, utaelewa utu wa mwenzako.
Ukielewa utu wa mwenzako, utauthamini.
Na ukiuthamini utu wa mwingine, utamtendea yale ambayo hata wewe uko tayari kutendewa.
Hakika, kujifahamu na kuelewa maisha ndio mwanzo wa kuishi kwa amani, wema, na kufurahia uwepo wetu duniani.
Mimi ni mwalimu wa maisha, na mwalimu wa mambo ya Mungu.
Ninafundisha kuhusu: Utambuzi binafsi. Ukweli wa maisha na elimu ya Mungu mwenye vyote.
Karibu ujumuike nami katika kudumisha utu wa Watu, hadi pale tutakaporejesha umoja wetu wa kuishi kiutu.
Ndimi, Mbulwa King'ung'e
Mawasiliano: 0744 284 329
Comments
Post a Comment