“Kuzaana Bila Utambuzi ni Mzigo, Siyo Baraka...”
Kisha kuna jambo linaloitwa kuzaana.
Kila kiumbe hupewa shauku ya kuleta nafsi nyingine duniani.
Hata hivyo, kuleta nafsi bila kuiandalia urithi wa Utambuzi Binafsi na misingi ya kiutu si baraka ni mzigo.
Ndiyo maana dunia ya leo imejaa mkanganyiko wa kimaadili, kifikra na kiutambulisho.
Si kwa sababu tumekuwa wengi kupita kiasi, bali kwa sababu tumezalisha maisha bila misingi—bila kujitambua, bila mizizi, bila dira.
Ieleweke wazi: kuzaana ni sehemu ya mfumo wa Mungu.
Hata viumbe visivyo sahihi huzaana, kwa sababu kuzaana ni mfumo, si uthibitisho wa hekima.
Tatizo si kuijaza Dunia. Shida ni kile unachozaa umekiandalia mazingira gani katika dunia iliyojaa vurugu, mkanganyiko na kupotea kwa misingi.
Je, unawajua nguruwe? Kondoo? Mbuzi?
Walipewa akili. Hakuna kiumbe ambacho Mungu aliumba bila akili. Kila kiumbe huumbwa na akili na hufundishwa kuhusu nafasi yake kupitia muujiza wa mfumo wa uhai.
Lakini kiumbe kinapojitenga na mwelekeo wake wa awali, huingia katika hali ya kupotoka—
si kwa sababu adhabu imelazimishwa, bali kwa sababu kimechagua matashi badala ya misingi.
Na kinapozalisha, vitoto hurithi mwelekeo huo huo.Ndiyo maana ni vigumu sana kwa viumbe hivyo kurudi kwenye akili waliyoumbwa nayo.
Sasa tuje kwa watu.
Kwa mtu, ujinga ni urithi kama ulivyo utajiri.
Hurithishwa kizazi hadi kizazi.
Wazazi huishi kwa mfumo fulani—uwe sahihi au si sahihi—na mtoto asipohoji, huuendeleza kama ulivyo.
Jamii inapokubaliana juu ya maadili fulani hata yasiyo sahihi, mtoto huyafuata bila kuyaelewa.
Na bila mtu wa kuuliza “kwa nini”, ni vigumu sana kwa waliomo gizani kutambua kuwa wako gizani.
Ndiyo maana tunaona watoto wakilazimishwa: kutii bila kuelewa, kuendana bila kujitambua na kuamini bila kuuliza.
Kuwa mzazi au kuzaa si uthibitisho wa kujua ukweli wa kuishi. Kuzaana ni mfumo tu.
Tumezaa, lakini hatujawapa watoto ukweli wa KUISHI.
Tumewaacha walelewe na mifumo ya elimu inayowaandaa kufanya kazi, si kujijua, inayowafundisha kuiga, si kujiuliza na inayowatenganisha na mizizi yao.
Kisha wakibadilika, tunawalaumu.
Tumewafundisha kupenda kila kitiu kilichotokea ulaya, tukawasahaulisha asili na hadhi yao.
Hatuna muda nao.
Wanapouliza, tunakasirika.
Wanapotafakari, tunawanyamazisha.
Tunawaadhibu, tunawakosoa, tunawapa majina yanayowavunja—tukidhani tunalea, kumbe tunafunga fahamu zao.
Tunawaacha muda mrefu peke yao.
Wanaanza kujipuuza, kujiona hawafai, kujikataa.
Matokeo yake ni kupotea kwa utambuzi binafsi.
Tumewakabidhi kwa mifumo isiyo na utu.
Kwa walezi wasiojali.
Kwa waelimishaji wasiouliza “kwa nini”.
Mifumo hii imekuwa si rafiki kwa mtoto.
Ndiyo maana tunaona watoto wetu wakipoteza mwelekeo, wakijitafuta bila kujijua, wakichukua njia za maumivu wakidhani wanatafuta maana.
Haya si matukio ya BAHATI Mbaya.
Ni dalili za: kukosekana kwa Utambuzi Binafsi na
kukosekana kwa misingi ya kiutu.
Kama jamii, kuna mahali tumekwama.
Maisha hayakupaswa kuwa hivi.
Ni kweli, kila MTU hupitia mapito.
Tatizo si mapito; tatizo ni kuruhusu mapito yale yale yarudi kwa nafsi tunazozileta duniani.
Ndiyo maana nilichagua kutooa mapema.
Nilichagua kwanza kuandaa mtaala wa familia yangu.
Kama mfumo haukunisaidia mimi nijijue,
utawezaje kuwasaidia watoto wangu?
Nikaona haiwezekani. Nilichagua kurekebisha kabla ya kuendeleza.
Siwarithishi mali. Nawarithisha misingi.
Kwa sababu hapa duniani hakuna kitu cha thamani kuliko misingi.
Jiulize: una misingi ipi? Au unataka mtoto wako aje kuishi maisha yako bila kuyaelewa?
Mimi si nabii. Na siamini katika unabii. Lakini ninaweza kusema kwa uhakika: mtoto asiye na misingi ana uwezekano mkubwa wa kupitia maisha magumu zaidi kuliko mzazi wake.
Ndiyo maana King Mentorship Program haikuanzishwa kwa pupa.
Ni juhudi ya makusudi ya kuandaa: wazazi wanaojitambua, walezi wenye uwajibikaji, jamii yenye fahamu na hatimaye, taifa linalojielewa.
Karibu uwe sehemu ya kujenga kizazi kinachojitambua.
Ndimi: Mbulwa King'ung'e
Mwanzilishi – King Mentorship Program
Mjenzi wa Fikra za Kiafrika!
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment