Mungu Hana Watetezi: Uongo wa Imani ya Kupandikizwa...

Nitawambia mambo ambayo hakuna Mzungu wala Muarabu aliyewahi kusema—wala atakayekuja kusema.

Kwa sababu wengi wenu mmelelewa kujua kwa maarifa ya kupandikizwa, mkasahau kabisa maarifa ya kwenu.

Mkakumbatia yaliyoletwa, mkayadharau yaliyokuwa.

Leo naendelea kuzungumzia ukweli kuhusu Mungu na uongo uliobebeshwa kumhusu.
Na nisikike vizuri hapa:

Nikimtaja Mungu, simtaji kutoka kwenye kitabu chochote cha tamaduni zilizoletwa. Namtaja kutoka chanzo cha utu.

Nalitaja lile jina ambalo hata waliokuja na vitabu walilikuta tayari lipo.

Sikulileta. Sikulifundishwa. Nililirithi.

Nataja jina ambalo wazee wangu, babu zangu, na vizazi vyangu walilitambua kabla ya maandishi, kabla ya tafsiri, kabla ya mipaka.

Waliliabudu si kwa woga, bali kwa ufahamu wa uhai.

Nataja lile jina lenye ukuu, jina lililokuwepo kabla ya majina, linalopita kila jina lililojitangaza kuwa Mungu, na kila jina lililofananishwa na Mungu.

Si jina la kutungwa. Si jina la kutafsiriwa. Si jina la kubishaniwa.

Ni jina la Chanzo cha uhai.  Ni jina linalotambulika na roho kabla ya akili kuingiliwa.

Majina mengine yalikuja baadaye—kama vivuli vya jina hili. Kama sauti zilizojaribu kuiga mwangwi wake.

Lakini hili halina mbadala. Halina mshindani.
Halihitaji mtetezi.

Kwa sababu halikai kwenye midomo ya watu—linakaa kwenye uhai wenyewe.

Vitabu vya kuletwa havina mzizi wa jina Mungu.
Ndiyo maana havina hoja moja.

Vimebaki kushindana, kutishiana, na kugombania mamlaka.

Kwa hiyo wewe baunsa wa Mungu, wewe mtetezi wa Mungu—kabla hujaendelea kutetea usichokijua, fahamu hili:

Mungu hana watetezi. Wala hahitaji viumbe alivyoviumba vibishane, viuane, vishindane au kunyongana kwa jina lake.

Akili ndogo hufurahia mashindano hayo, kwa kuita utumwa huo “imani,” wakati utu wao unaharibika.

Lakini akili kubwa hutambua; haya si ya Mungu.
Haya ni ushabiki uliopachikwa jina Mungu.

Katika kukua kwangu, nilipenda sana Uarikasi/Uafrika. Sio kwa jazba—bali kwa kiu ya ukweli.

Nilitaka kujua: ni nini kilikuwapo Arikas/Afrika kabla ya madaftari ya Asia na Ulaya kuwasili?"

Nilipopekua historia, nikakutana na jambo moja zito—na hata wewe litakushangaza.

Mkoloni aitwaye King Leopold II, mtawala wa kikoloni wa Congo kipindi hicho, aliandika barua kwa wamisionari na viongozi wa kidini kabla ya kuingia Afrika."
Katika barua hiyo aliwaonya wazi:

"Waafrika si wajinga. Wanaujua ukweli wa KUISHI. Wanaamini kuna Nguvu Kuu inayotawala maisha yote. Wanaiheshimu. Wanaitii. Wanaiita Mungu."

Lakini akaongeza: "Msifundishe ukweli. Kumbukeni hatuji kuokoa roho—tunakuja kujenga utajiri.

Usimfundishe "mnyama mweusi" kudadisi. Mfundishe kutii. Mfanye awe kondoo. 

Usimruhusu ahoji. Usimfundishe chochote kuhusu ardhi yake na rasilimali zake.

Msasahaulishe kabisa utajiri uliopo chini ya miguu yake.

Mtishie kwa kauli hii: “Heri walio maskini wa kiroho, kwa maana ufalme wa mbinguni ni wao.”

Jana nilizungumza kuhusu roho.
Na narudia hapa bila kuyumba: Hakuna roho maskini. Hakuna roho tajiri.

Roho zote hutengenezwa kwa muujiza mmoja wa Mungu. Na kila kilicho hai kina roho.

Kabla hujaanza kutetea maana za kuletwa, kuhusu ufalme wa Mbinguni, jibu swali moja rahisi:

Mbingu ni nini?

Kwako wewe, mbinguni ni angani. Huo ni uongo wa elimu ya kinajimu iliyopandikizwa ili usiujue ukweli.

Je, unajua kuwa mpaka sasa uko NDANI ya mbingu?

Sasa wewe unayesema “utaenda mbinguni,”
utaenda mbinguni ipi wakati mahitaji yako yote ya hapa duniani yanatoka kwenye mbingu?

Dunia yenyewe inategemea mbingu ili iishi.

Au hujui kwamba dunia ni kiumbe chenye uhai wake?

Unaishi juu ya kiumbe mwenzako—lakini hata hilo ulifundishwa kulisahau.

Mbingu yenyewe hutenda kazi kwa kutegemea mazingira maalum yanayoitwa Santigil,
ili iweze kutimiza jukumu lake la kuhudumia dunia na sayari nyingine.

Kwa maana mbingu si wingu tupu,
wala si anga hapo angani. Kitu kingine kabisa! 

Mbingu hutumikia. Dunia hupokea.
Na vyote viko ndani ya mpangilio mmoja wa Uhai.

Nikisema hujui, ukubali.
Nikisema unazungumza usivyovijua, ukubali.
Nikisema unakemea usivyovijua, ukubali.

Je, uliletwa duniani kukemea
mpaka mishipa ya shingo ikakamae?

Au unachezeshwa kiakili na mifumo isiyoonekana?

Nikimtaja Mungu, namtaja Mwenye vyote—
MunĂ» Hungu.

Simtaji God.
Simtaji Allah.
Simtaji Jehovah.
Sitaji cheo wala kiti.

Namtaja Mungu kama alivyonukuliwa na
Chanzo cha Utu — MTU wa kwanza.

Muafrika wa leo, tuliza kichwa. Pumzika.

Muarabu kakuletea maadili yake, kwa kusema hayo ndiyo ya Mungu—unakumbatia bila kuchunguza.

Mzungu kakuletea tamaduni zake, ukayapa kuwa hayo ndiyo ya Mungu—unakumbatia bila kuuliza.

Ndiyo maana leo mnavurugana. Hampatani.

Lakini ukweli ni mmoja: ninyi wote ni watu.
Ninyi wote ni ndugu.

Achaneni na mabaya ya kupandikizwa. Rudini kwenye utu wenu.

Narudia tena: nitasema mambo ambayo
hakuna kitabu cha tamaduni yoyote kilichowahi kuyaandika.

Yataingia akilini mwako kwa mantiki.
Ukubali au ukatae—yataingia TU.

Utaishi nayo muda mrefu, na siku moja akili yako itasema: “Huu ndio ukweli.”

Na hakuna ukweli unaozidi hapa.

Na kama wewe ni MTU unayetafuta ukweli wa KUISHI, sio vihela vya kichimvi, wala madaraka ya kichimvi, basi ukweli unaoutafuta ndiyo huu.

Sio kwa sababu mimi nimesema—bali kwa sababu akili yako itautambua, hata kama utausukuma mbali.

Na ni kweli pia: si wengi wanaoujua ukweli huu.
Si kwa sababu umefichwa, bali kwa sababu haupendwi na akili iliyofungwa.

Duniani kuna watu bilioni—lakini wachache sana
wanaothubutu kuacha kupokea na kuanza kujua.

Na mimi ni miongoni mwa hao wachache,
sio kwa cheo, sio kwa ubora wa damu, bali kwa uamuzi wa kuitii akili huru kuliko hofu ya kupandikizwa.

Ukweli huu hauombi uaminiwe. Unahitaji kutambuliwa.

Na utakapoutambua, hutahitaji mtu wa kukuambia— utajua tu.

Ndimi Mbulwa King’ung’e
Mawasiliano: 0744 284 329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...