“SISI SOTE NI NDUGU WA DAMU: Ukweli Uliopotea wa Utu wa watu...”
Ndugu zangu...
Leo ninaandika makala hii si kwa hasira, wala si kwa lawama.
Ninaandika kwa tafakari.
Nilitulia. Nikawaza. Nikajiuliza swali moja gumu, lakini la msingi: Kwa nini sisi watu tunafanyiana ubaya, ilhali sote ni kitu kimoja?
Ninajua, na nina uthibitisho thabiti; kwa hiyo ninalisema hili bila woga wala kuyumba: sisi sote ni ndugu.
Si ndugu kwa sababu tunaishi jirani.
Si ndugu kwa sababu tumezaliwa katika familia au ukoo mmoja.
Sisi ni ndugu wa damu, kwa sababu tunatokea katika chanzo kimoja.
Hapa nazungumzia chanzo cha Utu—uwepo wa MTU wa kwanza, mwanamume wa kwanza na mwanamke wa kwanza, na uzao wao uliopo hapa duniani leo.
Tatizo kubwa si kwamba undugu huu haupo. Tatizo ni kwamba hatujafundishwa kuujua.
Tumezoeshwa kufikiri kwamba ndugu ni yule uliyezaliwa naye familia moja. Ndugu ni yule wa ukoo wako.
Ndugu ni yule wa kabila lako. Ndugu ni yule wa dini yako. Ndugu ni yule anayefanana na wewe kwa jina, imani au mwonekano.
Ikitokea MTU hana jina la ukoo kama lako, si wa eneo lako, hana imani yako, hajazaliwa katika taifa LAKO au hajazaliwa kama wewe—basi huyo tunaambiwa si ndugu yako.
Leo nawahoji: ndugu ni nani hasa?
Je, ninyi wote si ndugu? Au ni kwa sababu mlikengeushwa utu wenu, mkasahaulishwa chanzo chenu?
Leo nikikuuliza unitajie uzao wa MTU wa kwanza—yule aliyezalisha watu wote hadi kufika wewe hapo ulipo—huwezi kujibu.
Si kwa sababu hutaki kujua, bali kwa sababu hujawahi kuhimiza nafsi yako kujua. Umeridhika kuishi kwenye hoja ndogo, kwenye mafundisho ya mafumbo.
Kuna msemo wa kale usemao: fumbo mfumbie mjinga, mwerevu ataling’amua. Bado upo kwenye mafumbo?
Kama hukujua, basi fahamu leo: maisha ni mwendelezo, na wewe ni sehemu ya mwendelezo wa uzao wa MTU wa kwanza. Hukumea kama uyoga.
MTU huyu wa kwanza hakuwa na kabila, hakuwa na dini, hakuwa na jina la ukoo, hakuwa na taifa. Yeye ndiye chanzo halisi cha ninyi nyote kupatikana.
MTU wa kwanza alikuwa na rangi nyeusi kutokana na sababu za kuumbwa kwake. Lakini hilo halimaanishi alikuwa Mwafrika, kwa maana “Afrika” ni jina la baadaye—ni ubatizo wa uliofanywa na watu wa ulaya. Hapo kale bara hili liliitwa Arikas.
Mwanamke wa kwanza alikuwa na rangi ya kati, ya manjano hafifu—kile ambacho leo baadhi wanakiita albinism.
Hapo ndipo chanzo cha watu weupe kilipoanzia, huku mwanaume akiwa chimbuko la rangi nyeusi.
Ndiyo maana ukiona wahindi weusi, usishangae—hao ni uzao wa MTU wa kwanza. Ukiona watu weusi waliozaliwa asilia katika baadhi ya maeneo ya Ulaya, kabla hata ya mwingiliano wa bara la Afrika, tambua hawa ni masalia ya mwanzo wa uzao wa MTU wa kwanza.
Taratibu za JADI zinadokeza kuwa, MTU wa kwanza alizaa watoto 168. Aliwazaa katika mabara yote saba, kwa kila bara katika nchi 12 za asili, kwa uzao wa mapacha 12—kiume na kike.
Watoto hawa waliishi chini ya malezi yake kwa muda mrefu, wakifundishwa kuishi kiutu, kuthaminiana, na kumtii Mungu mwenye vyote kwa kumsalia kila asubuhi na jioni.
Walikuwa wakizungumza lugha ya Kibantu, na lugha hiyo ndiyo ikawa msingi wa uzao wao wote katika mabara yote.
Hadi sasa, lugha ya Kibantu inabakia kuwa chimbuko cha lugha zote unazozijua duniani.
Hii si tu historia ya maneno; ni ushuhuda wa undugu, mwendelezo wa kiutu, na alama ya chanzo kimoja cha watu.
Katika hatua za mwanzo kabisa za uhai wa watu, watoto wa tumbo moja—pacha wa kiume na wa kike—waliendelea kuoana ili kuendeleza uzao.
Kwa maana hiyo, mapacha waliozaliwa pamoja ndiyo waliokuwa mhimili wa kuendeleza uzao wa watu.
Hili halikuonekana kosa katika muktadha wa wakati huo, kwa sababu lengo halikuwa maadili ya baadaye, bali kueneza uhai na kuhakikisha mwendelezo wa kizazi cha MTU.
Baadaye, hekima ya wazee ikaona yafaa watu waendelee kuoana nje ya familia zao za karibu.
Sio kwa sababu hawakuwa ndugu wa damu, bali ili jamii ziingiliane—koo kwa koo, jamii kwa jamii—na kudumisha umoja wa kiutu.
Hapo ndipo majina ya ukoo, makabila na maeneo yalipoanza. Si kwa lengo la kuwagawa watu, bali kwa ajili ya utambulisho: nani alikaa wapi, nani alianza wapi, nani alizaa wapi.
Majina haya hayakutoka kwa Mungu. Yalitokana na mababu zenu—wale wale mnaowashutumu leo kwa majina ya uchawi na laana.
Nasisitiza tena: ninyi nyote ni uzao wa MTU wa kwanza na mke wake.
Usichanganye ninachosema na simulizi la Adam na Eva. Hao ni wazawa wa mbali sana wa MTU wa kwanza na mke wake.
Ninazungumzia historia ya takribani miaka milioni 11 iliyopita, kwa mtazamo wa UWEPO wa kiumbe MTU hapa duniani.
Kwa maana hiyo, ninyi wote ni ndugu. Si ndugu wa kujuana, bali ndugu wa damu.
Lakini mmegeuzana matumizi.
Mwanaume anajivunia kuwalala wanawake wengi, asijue anawakandamiza dada zake wa damu waliopaswa kulindwa na kuthaminiwa.
Mwanamke anajivunia kuwachuna wanaume, asijue hao ni kaka zake wa damu, lakini akili yake imekengeushwa.
MTU anajivunia kujeruhi, kuumiza, hata kuua kwa ajili ya kazi, cheo, madaraka au maslahi. Hajiulizi kwamba anayemwangamiza ni ndugu yake wa damu kabisa.
Je, huu ni ufahari au ni upumbavu?
Ukitaka uthibitisho kwamba sisi sote ni ndugu, angalia pale MTU mwenzako anapopata shida ghafla—moyo wako unaumia.
Ukiona MTU akigongwa mbele yako, hata kama humjui, hata kama unasema ni mchawi—bado unaumia.
Kumbuka matukio ya tarehe 29 Oktoba. Ni nani hakuhisi maumivu? Uliumia, kwa sababu walioumia walikuwa watu kama wewe—sehemu ya uzao wa MTU wa kwanza kama wewe.
Anaandika Mbulwa King’ung’e, mjenzi wa jamii ya kiutu nchini Tanzania.
Mtu aliyejitolea kusema ukweli ambao hakuna mzungu wala muarabu aliyewahi kusema, wala atasema.
Anaibua historia, falsafa, na undugu wa damu bila woga, bila kufungwa na dini, kabila au rangi.
Anaibua ukweli ambao wengine wanazama kwa hofu, wengine wanaukwepa kwa tamaa, na wengine wanalia kwa uchungu.
Leo, yeye anakualika wewe—msomaji, hadhira, mtu wa kawaida—usikubali kudanganywa, usikubali kufungwa na hoja ndogo.
Usikubali kudhani kuwa rangi, kabila, dini au jina lako la ukoo linakutenganisha na ndugu zako wa damu.
Kwa sauti thabiti na moyo wazi, Mbulwa King’ung’e anasema: “Kila mtu unayemwona, kila kiumbe unayemkumbuka—ni ndugu yako wa damu. Haijalishi umejua au hujui.”
Nawapenda sana ndugu zangu nyote kwa MOYO Wangu wote.
Mbarikiwe na ya Mungu mwenye vyote.
Ndimi Mbulwa King'ung'e
Mawasiliano: 0744 284 329
Comments
Post a Comment