Tumefundishwa Kusawazisha Makosa, Siyo Kuishi Kwa Usahihi...
Ni ngumu sana kuishi kwa usahihi kama hatujitambui.
Na ni vigumu zaidi kujitambua kama hatujawahi kufundishwa sisi ni nani.
Ndiyo maana tumeishia kuishi kwa usawa badala ya usahihi.
Tunasawazisha mambo hata pale yasipostahili kusawazishwa.
Hata nikikufanyia ukatili, nitatafuta namna ya kuuhalalisha—kwangu ionekane ni sawa.
Lakini ukweli ni huu: Kile unachoona ni sawa, kinaweza kuwa si sawa kwa mwingine.
Angalia mahusiano ya mwanaume na mwanamke.
Mwanaume akichepuka, jamii inasema ni kawaida.
Mwanamke akichepuka, anahukumiwa, anaitwa malaya, anatengwa, hata kufukuzwa.
Lakini tukitumia mizani ya kiutu, tunagundua kuwa kuchepuka hakutakiwi kwa jinsia zote.
Tofauti ni kwamba tumejifunza kuhalalisha upande mmoja na kuadhibu mwingine.
Hapo ndipo tunapoanza kuishi kwenye ulimwengu wa uongo.
Ulimwengu ambao unawazalisha wanafiki wengi kuliko watu halisi.
Jaribu kuangalia watu 30 waliokuzunguka.
Ni wangapi unaowaona wamenyooka, wanaishi kwa ufasaha wa kiutu, hadi hata wewe unawakubali?
Mara nyingi hawazidi wawili.
Kwa nini? Kwa sababu tumelelewa kuhalalisha makosa, si kuyaacha.
Hatukufundishwa mizizi yetu. Hatukufundishwa kujielewa.
Na mtu asipojielewa, hawezi kuwaelewa wengine.
Ndiyo maana tumekuwa mizigo kwa wengine, vikwazo kwa wengine, na wakati mwingine minyororo ya akili kwa wengine.
Tunafunga fahamu za watu makusudi ili tujinufaishe.
Tunatumia ujinga wao—ambao sisi wenyewe tumeutengeneza kuwanyonya.
Tumewageuza watu kuwa bidhaa, na tunachowauzia hakijawasaidia.
Badala ya kupongezana kwa kuishi kwa usahihi, tunapongezana kwa kuendekeza usawa wa uongo.
Huenda maneno yangu yanaonekana magumu.
Lakini ukweli ni huu: Tusipojitambua sisi ni nani na kwanini tupo hapa duniani, tutaendelea kuishi kwa matashi yetu huku tukiumiza wengine.
Tutatumiana badala ya kufaidiana. Tutaishi kinafiki badala ya kiutu. Tutafanya unyama unaozidi hata wanyama wa porini.
Jiulize: Kama tuna elimu nyingi, waliosoma wengi—kwa nini ujinga unaongezeka?
Kwa nini maradhi, migogoro, chuki na mipasuko vinaongezeka?
Kama tuna dini na imani zinazotishia watu adhabu kali, kwa nini hao hao wanaoongoza na waongozwaji ndio wanaongoza kufanya maovu?
Sihukumu. Ninafafanua.
Tatizo ni kukosa mizizi. Ni kama mvuta sigara—anajaza moshi ndani, kitu kisicho na virutubisho, kinachomdhuru.
Watu hawahitaji kufanywa mashabiki wa makundi.
Wanahitaji kufundishwa kujielewa. Wao si kondoo. Ni watu.
Usimuuzie mtu elimu kwanza— mfundishe utambuzi binafsi.
Usimuuzie mtu imani— mpe mizizi.
Mfundishe ukweli kuhusu Mungu mwenye vyote, si michezo ya kiakili inayomzuia kufikiri na kuhoji.
Elimu inayomzuia mtu kutumia akili zake humfanya asijitambue.
Familia kupitia vipigo, kejeli, dharau, kunyanyasa na kutenga mtoto, humtoa kwenye utambuzi binafsi.
Jamii kupitia kuhalalisha upotevu humharibu mtoto kiutambuzi.
Elimu za mapokeo—hasa hizi za kumpima mtoto kwa ufaulu pekee—humfanya ajione mjinga, punguani, hana akili.
Dini za mapokeo nazo zimefifisha uwezo wa akili
kwa kuzuia kuhoji na kuficha asili ya mtu.
Sijisifu, lakini kupitia King Mentorship Program nimewacoach hadi viongozi wa kiroho.
Wengi walishangazwa na elimu ya Utambuzi Binafsi na wakakiri kuwa hii ni kila kitu.
Utambuzi binafsi si elimu ndogo. Ni zaidi ya elimu ya kawaida. Ni msingi wa maisha.
Ndiyo maana maono ya King Mentorship Program ni kujenga jamii inayojitambua, inayoweza kujiongoza, kujisimamia na kujitawala.
Huu si mwito wa fedha. Si mwito wa umaarufu.
Ni mwito wa kurejesha utu wa mtu na umoja wa watu.
Karibu uwe sehemu ya kujenga kizazi kinachojielewa.
Kinachoishi kwa usahihi, si kwa usawa.
Ndimi Mbulwa King’ung’e
Founder – King Mentorship Program
📞 Mawasiliano: 0744 284 329
Comments
Post a Comment