UHAI, ROHO, NA MUNGU: TOFAUTI AMBAZO HUJAFUNDISHWA...
Aliyekufundisha kuhusu roho, mara nyingi hajui alichokufundisha. Ndiyo maana hata roho za wafu zimeitwa Mungu.
Hapa duniani kuna wanaosema. Na kuna wanaojua wanachokisema.
Kuna wanaofumba. Na kuna wanaojua kufumbua.
Ndiyo maana nimesimama hapa. Si kwa makelele, si kwa mabishano, bali kwa ufumbuzi.
Nitafumbua mafumbo mliyofumbiwa—ikiwemo mafumbo ya kiimani. Kwa sababu Mungu hakupi imani ili akufumbe; imani ya kweli hufungua, huangaza, na huweka wazi.
Miongoni mwa masomo yanayochanganya watu wengi duniani ni somo la Roho.
Limezungukwa na hofu, tafsiri za kurithi, na unyenyekevu usiohojiwa. Ndiyo maana nitaanza taratibu. Usikimbie. Utaelewa tu.
Roho si dhana nyepesi. Roho si hadithi. Roho si jina la kumtukuza Mungu. Roho ni mionzi mikali sana, isiyoweza kutathminika katika hali ya kawaida ya kimaabara. Ni nguvu iliyo nje ya mizani ya macho, lakini si nje ya athari zake.
Mionzi hii huingizwa katika mwili wa kiumbe pale kiumbe hicho kikiwa bado tumboni—kwa wakati mahsusi wa mimba. Si kwa bahati, si kwa hisia, bali kwa mpangilio.
Kwa kiumbe MTU, mionzi ya roho huingizwa mwilini mama akiwa na mimba ya takribani miezi mitatu, au siku tisini.
Roho iko katika mithili ya umeme. Inapoingia ndani ya nafsi, nafsi hupata uhai. Ndiyo maana uhai ni wa roho—haufi. Na uzima ni wa mwili—ndiyo maana mwili hufa.
Hapo ndipo nafsi hupokea uhai. Kabla ya hapo kuna mwili unaojengeka; baada ya hapo kuna kiumbe anayeishi.
Mwili hufa roho ikitoka. Roho ikiwapo, mwili huishi. Huu ni msingi wa kuanza kuelewa, si hitimisho.
Roho hizi ziliandaliwa na Mungu mwenyewe kwa ajili ya viumbe vyake vyote. Lakini hapa ni lazima nifafanue jambo moja lililopotoshwa sana: Mungu si Roho.
Mungu haishi kwa maana ya kuhuishwa. Hana mwili kwa sababu yeye si kiumbe. Yeye yuko nje ya uhai anaouanzisha. Bali alizifanya roho ziwe nyenzo za kuwezesha viumbe alivyoviumba kuishi.
Kila kiumbe kiliumbwa na mwili, kisha kupewa roho, ndipo kikapata uwezo wa KUISHI.
Roho hizi hufungwa na muujiza wa Mungu unaoitwa alotro jabaz kwa lugha ya Kibantu, na kwa Kiswahili huitwa Siri Kuu ya Uficho Mkuu. Si kila siri hufichwa ili isijulikane; nyingine hufichwa ili ilindwe dhidi ya wasio tayari.
Roho huingizwa mwilini mwa kiumbe kwa ajili ya kazi kubwa mbili—hakuna ya tatu:
Kwanza, uchanganuzi. Hapa ndipo kiumbe hupata uwezo wa kufikiri, kupima, kulinganisha, na kutofautisha lipi ni jema na lipi ni baya.
Huu si uwezo wa dini, ni uwezo wa roho. Ndiyo maana hata asiye na imani anajua baya ni baya.
Pili, kunukuu. Roho hurekodi. Hurekodi kila tendo, kila chaguo, kila mwelekeo wa maisha ya kiumbe wakati wa uhai wake. Hakuna tendo linalopotea.
Kumbukumbu hizi hubaki hata baada ya mwili kufa. Ndiyo maana hukumu ipo—lakini siyo ya moto kama mlivyofundishwa. Hukumu ni ya kumbukumbu. Kila roho huhukumiwa kwa kadiri ya kile ilichonukuu yenyewe.
Kwa hiyo, hakuna malaika wala mtu anayeandika matendo yako kwenye kitabu cha nje kinachoitwa “kitabu cha uzima.” Huo ni mfano uliotumika kufundisha watu wasio tayari kufikiri kwa kina. Rekodi halisi iko ndani ya roho yenyewe.
Hata malaika wenyewe watahukumiwa kwa ya kwao na upumbavu wao.
Mungu aliviumba viumbe kwa jinsia ili vizaane. Na kila jinsia hupokea roho kutoka makao tofauti. Hitajiano la kimwili lipo kwa sababu ya utofauti wa roho, si kwa tamaa pekee.
Roho za kiume huhifadhiwa katika makao yanayoitwa bozgada mahalalya.
Roho za kike huhifadhiwa katika makao yanayoitwa kobil Antoni.
Angalizo: Roho hizi ni safi, hazina kumbukumbu wala rekodi yoyote kabla ya kuingizwa katika kiumbe.
Na hili halihusu binadamu pekee—bali viumbe vyote vilivyobeba uhai hupokea roho kutoka hayo makao mawili.
Baada ya kiumbe kufa—iwe ni malaika, jini, mtu, mnyama au mdudu—roho hutoka na kuelekea anga mbili tofauti kulingana na rekodi ya maisha yake.
Kiumbe kilichohitimisha maisha katika mema huingia anga iitwayo zugril galayo. Hapa huhifadhiwa roho za viumbe vyote vilivyohitimisha mema katika kuishi.
Kiumbe kilichohitimisha maisha katika mabaya huingia anga iitwayo maalumu nunu. Hapa huhifadhiwa roho za viumbe vilivyohitimisha mabaya katika kuishi.
Roho hubaki kama ilivyoakisi kile ilichorekodi na kukiishi. Roho ya kiutu hubaki na sifa ya kiutu.
Iliyonakili mema hubaki na kumbukumbu njema. Iliyonakili mabaya hubaki na kumbukumbu mbaya.
Roho hizi zina uwezekano wa kurudi hapa duniani na kuendeleza maono yao kupitia viumbe walio hai kimwili.
Si kwa bahati, si kwa kuchezea watu, bali kwa mvuto wa yale waliyoyaacha. Hapa ndipo lugha ya watu kuwa vyombo vya roho ikaanza. Kimungu hii ni fasaha, lakini Roho hizo siyo za Mungu.
Roho za kiutu zilizohitimisha mema huitwa mizimu. Sasa jiulize: unapofundishwa ukemee mzimu, je mzimu ni nini? Na wewe ukifa—ikiwa umehitimisha mema—utakuwa nani?
Roho za kiutu zilizohitimisha mabaya huitwa mizuka. Na mtu anayejishikiza katika mabaya huku akidai anamcha Mungu bila kujua, anaweza kufa na kuishia hapo.
Sasa jiulize kwa uaminifu: kama roho za viumbe wenzenu mmeziita Mungu, mnafikiri kweli mtamjua Mungu ni nani?
Roho ya kiumbe mwenzako inapokuja kukusemesha kwa matashi yake iliyorekodi wakati wa uhai wake—hiyo si Mungu. Ni kiumbe kama wewe, bila mwili.
Wewe unayesema Mungu ni roho, nenda ukatafute kwanza roho ni nini, na yeye ni roho ipi.
Ninayasema haya si kwa kubembeleza, bali kwa kufungua. Nitawaambia yale mnayopaswa kujua—yale ambayo hakuna muarabu wala mzungu aliyewahi kusema, wala atakayesema.
Ndimi Mbulwa King'ung'e
Mawasiliano: 0744 285 329
Comments
Post a Comment