“Yule Unayemuona Ndani Ndiye Unayekuwa Nje..."



Hakuna mtu yeyote duniani mwenye mamlaka ya kupanga kiwango cha kujiona kwako isipokuwa wewe mwenyewe.

Na hakuna MTU atakayekufanya ujione dhaifu bila wewe kumpa ruhusa hiyo ndani ya fikra zako.

Ukweli mkubwa wa maisha ni huu: vile unavyojiona ndivyo unavyokuwa — na kwa kiwango fulani tayari umeshakuwa hivyo.

Maisha hufuata picha iliyopo ndani ya akili yako. Kama ambavyo huwezi kukipata kitu ambacho hujakiona, vivyo hivyo huwezi kuwa mtu ambaye hujamuona ndani yako. 

Maono ya ndani ndiyo yanayochora uhalisia wa nje. Mtu haendi mbali zaidi ya pale alipoishia kujiona, kwa sababu hapo ndipo hujenga ukomo wake wa kufikiri. 

Mara nyingi huo ukomo si halisi bali ni taswira iliyojengwa na mitazamo, mazingira au maneno aliyoyakubali kuyahifadhi akilini.

Kiwango cha kujiona ni kama ramani ya safari ya maisha. Inakuongoza kutoka ulipo sasa hadi pale unapojiona ukifika. 

Ndiyo maana kanuni ya msawazo wa akili husema kuwa uhalisia wa maisha yako ni kivuli cha picha iliyopo kwenye fahamu zako. 

Mtu hushindwa kwanza akilini kabla hajashindwa maishani, na hushinda kwanza ndani kabla hajashinda nje.

Unapojiona kuwa wa kawaida kupita kiasi, maisha yatakupa ukawaida. 

Unapojiona kuwa mtu wa thamani na mwenye uwezo, maisha huanza kukutengenezea mazingira yanayolingana na taswira hiyo.

Fikiria upo Kigoma na umepewa jukumu la kufika Mbeya. Kwa kuwa ni mgeni wa njia, unaamua kutafuta ramani. 

Lakini kwa bahati mbaya unapewa ramani ya Kigoma–Kagera badala ya Kigoma–Mbeya.

Unaifuata kwa uaminifu, unaweka juhudi, unatembea kwa bidii… na hatimaye unafika Kagera. 

Je, ulipotea kwa sababu ya kukosa uwezo au juhudi? Hapana. Ulipotea kwa sababu ya ramani isiyo sahihi.

Hivyo ndivyo wengi wetu tunavyoishi — tukifuata ramani za kujiona tulizopewa na hofu, historia, au maneno ya watu wengine. Tatizo si uwezo wetu; tatizo ni taswira tuliyokubali ndani yetu.

Ukweli ni kwamba sote tumeumbwa na uwezo mkubwa, lakini baadhi yetu hujiona wadogo kuliko tulivyo. 

Hapo ndipo tunaanza kuuza thamani ya maisha yetu kwa bei ya chini, tukidhani huo ndiyo ukweli wetu. Hakuna kizuizi kikubwa duniani kuliko kile unachojiwekea mwenyewe akilini.

Kila ukomo unaouona nje mara nyingi ni tafsiri ya ukomo uliouweka ndani. Badili unavyojiona, na mwelekeo wa maisha yako utaanza kubadilika kimya kimya.

Ni muhimu kujihadhari na lugha unayojitumia, kuchunguza picha uliyonayo kuhusu wewe mwenyewe, na kujifunza kujiona katika kiwango cha juu zaidi kuliko hali yako ya sasa. 

Tengeneza ramani mpya ya akili kabla hujataka maisha mapya, kwa sababu kiwango cha maisha yako ni kivuli cha kiwango cha mawazo yako.

Unachokubali ndani ndicho kitakachojidhihirisha nje.

Kwa hiyo, swali si kama unaweza kufika mbali. Swali ni: Je, unajiona ukifika mbali?

Mwisho wa safari yako hauanzi nje — unaanzia ndani. Ndiyo maana usemi huu hubeba uzito mkubwa sana: “Yule unayemuona ndiye unayekuwa.”

Ukijiona wa kawaida, utaishi ukawaida. Ukijiona wa aina yake na mwenye mafanikio, utaanza kutembea katika mwelekeo huo. 

Maisha hayawezi kumpa mtu zaidi ya kile ambacho akili yake imeruhusu. Badili picha ya ndani leo, na kesho yako itabadilika bila mapambano makubwa.

“Iwapo unatamani kujengwa upya kimtazamo na kuanza kuona maisha katika kiwango cha juu zaidi, wasiliana nami. Tayari nimefanikiwa kuwasaidia wengi kubadilisha fikra zao na kufungua milango ya mafanikio yao.”

Kuhusu Mwandishi: Emmanuel Samuel King’ung’e ni Founder wa King Mentorship Program, Mwalimu, Mwandishi na Muelimishaji katika eneo la Maendeleo Binafsi, Life Coach & Consultant.

Mawasiliano: WhatsApp +255744284329 / 0773284329

Blog: kingmentorshipprogram.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...