“Mazingira si Hatima: Mapinduzi ya Fikra Yanayoamua Wewe Ni Nani...”



Duniani, MTU huzaliwa akiwa hana lebo, hana mipaka, hana tafsiri juu ya yeye ni nani. 

Lakini kadri anavyokua, anaanza kupewa majina yasiyo rasmi: “wewe ni wa kawaida,” “wewe si wa kiwango hiki,” “ndoto hizi si za watu kama sisi.”

Maneno haya hayaji kwa kelele; huja kwa sauti za upendo, kwa ushauri, kwa maonyo, kwa mifumo ya malezi. 

Taratibu sana, mazingira huanza kumchora mtu upya. Si kwa nguvu ya mikono, bali kwa nguvu ya fikra. Na kabla hajagundua, anaanza kuishi ndani ya ramani ambayo hakuiunda.

Mazingira si kuta wala barabara; mazingira ni mkusanyiko wa imani, sauti, matarajio, na viwango visivyoandikwa vinavyomzunguka mtu kila siku.

Ndani ya mazingira ndipo tunajifunza nini kinawezekana na nini hakiwezekani. 

Ndani ya mazingira ndipo tunapimiwa thamani yetu kwa mizani ya wengine. 

Watu wawili wanaweza kuzaliwa siku moja, katika hospitali moja, chini ya anga lile lile, lakini wakakua katika viwango tofauti kabisa vya kujiamini, kuthubutu, na kufikiri—si kwa sababu ya tofauti ya akili walizozaliwa nazo, bali kwa sababu ya tafsiri walizofundishwa kuzikubali kuhusu wao wenyewe.

Ndipo tunapofika kwenye ukweli mgumu: wengi wetu hatuishi maisha yetu halisi; tunaishi tafsiri tulizopewa. 

Mwandishi Joseph Murphy katika kitabu chake The Power of Your Subconscious Mind alizungumzia nguvu ya heterosuggestion —pendekezo linalotoka kwa mtu mwingine na kupokelewa na akili ya ndani bila kuchunguzwa kwa kina. 

Kwa lugha nyepesi, kile unachoambiwa mara kwa mara, ukiamini, hugeuka kuwa ukweli wako wa ndani. 

Hivyo, maneno kama “huwezi,” “utashindwa,” au “hicho si kiwango chako” zinapopokelewa bila uchambuzi, hujenga dari isiyoonekana juu ya uwezo wako. 

Si kwa sababu uwezo wako umefikia mwisho, bali kwa sababu imani yako imewekewa kikomo.

Hatari ya mazingira si kwamba yanakuzuia moja kwa moja; hatari yake ni kwamba yanakufundisha ujizuie mwenyewe. 

Unaanza kujiwekea mipaka kabla hata hujajaribu. Unaanza kuogopa kabla hata hujathibitisha.

Unaanza kupunguza ndoto zako ili zisilete msuguano na waliokuzunguka. Taratibu, unakuwa salama—lakini si huru. 

Unakuwa mtulivu—lakini si kamili. Na ndani kabisa, kuna sauti ndogo inayokuambia unaweza zaidi, lakini sauti hiyo imefunikwa na kelele za miaka mingi za mapendekezo hasi.

Hapa ndipo falsafa ya King Mentorship Program inapoanza. Haianzi kwa kukuambia dunia ni ngumu; hilo tayari unalijua. 

Haianzi kwa kukuahidi mafanikio ya haraka; hilo ni soko la hamasa. Inaanza kwa swali la msingi: Je, fikra unazoishi nazo ni zako kweli, au ni mkusanyiko wa sauti za wengine? 

Kwa sababu kama msingi wa utambulisho wako umejengwa juu ya mapendekezo yasiyochambuliwa, basi hata mafanikio utakayopata yatakuwa na dari ya kisaikolojia.

Hutaweza kupaa juu ya kiwango cha imani uliyo nayo kuhusu wewe mwenyewe.

Mapinduzi ya kweli huanza pale unapokaa kimya na kuchunguza kwa uaminifu: ni imani gani kuhusu mimi nimebeba kwa miaka mingi? 

Nani aliniambia? Je, nilithibitisha kwa ushahidi, au nilikubali kwa unyonge wangu? Katika mchakato huo, unagundua kwamba baadhi ya “ukweli” uliokuwa unaishi nao haukuwa ukweli bali tafsiri za wengine—wengine waliokuwa na hofu zao, mipaka yao, na uzoefu wao binafsi. 

Na kwa sababu hukuchuja, ukaubeba mzigo wao kama utambulisho wako.

King Mentorship Program inasimama juu ya kanuni moja kubwa: mazingira yanaweza kukuathiri, lakini hayawezi kuamua hatima yako bila ridhaa yako ya ndani. 

Hivyo, hatua ya kwanza ya mapinduzi ni kutambua sauti zilizokujenga. Si kuwalaumu waliokulea, bali kuchambua kilichoingia ndani yako. 

Hatua ya pili ni kuchuja kwa ushahidi—kujiuliza kwa ujasiri, “Ni ushahidi gani wa kweli unaothibitisha kuwa mimi siwezi?” 

Mara nyingi, utagundua hakuna. Kulikuwa na maoni, si uthibitisho. Kulikuwa na hofu, si ukweli.

 Hatua ya tatu ni kujenga upya pendekezo la ndani—kuunda kauli mpya za utambulisho, si kama maneno ya kujifariji, bali kama mwelekeo wa kimkakati wa akili yako. Huu ni uhandisi wa fikra, si burudani ya hisia.

Kwa sababu mwisho wa siku, dunia haikuwekei mipaka; fikra zisizochunguzwa ndizo huweka mipaka. 

Unaweza kubadilisha mtaa, nchi, au kazi, lakini kama hujabadilisha tafsiri yako ya ndani, utaenda na dari yako popote utakapokwenda. 

Ndiyo maana mapinduzi ya kweli si ya nje; ni ya ndani. Ni pale unapochukua mamlaka ya kuchagua nini uamini kuhusu wewe mwenyewe. 

Ni pale unapoacha kuishi kwa idhini ya sauti za wengine na kuanza kuishi kwa ufahamu wa uwezo wako.

Hivyo swali si kama mazingira yamekuathiri; hilo halina mjadala. 

Swali ni kama utaendelea kuyapa mamlaka ya mwisho juu ya hatima yako. Siku unapoamua kuchunguza fikra zako kwa kina, kuzichuja, na kujenga upya utambulisho wako kwa makusudi, siku hiyo huzaliwa mara ya pili—si kimwili, bali kiakili. 

Na hapo ndipo MTU wa kawaida anaanza kuwa kiongozi wa nafsi yake.

Hapo ndipo safari ya kweli huanza.

Ndimi Mbulwa King'ung'e, Founder King Mentorship Program.

Mawasiliano: 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...