“Jamii Isiyohojiwa Haiwezi Kukua...”
Kisha kuna neno jamii. Tunalitaja kwa urahisi, tunaliishi kila siku na tunalirithi bila kulichunguza kwa kina.
Ukweli ni kwamba jamii imekuwa kama kioo cha kujitazamia; imekuwa kipimo cha tabia, dira ya maamuzi, na mara nyingi chanzo cha utambulisho wetu.
Lakini swali ambalo halijaulizwa kwa ujasiri wa kutosha ni hili: je, kioo hicho kinaonyesha ukweli, au kinaonyesha mazoea yaliyozoeleka?
Kwa sababu si kila kinachoonekana kuwa cha kawaida ni sahihi, na si kila kinachofuatwa na wengi ni cha kweli.
Kwa tafsiri rahisi, jamii ni mkusanyiko wa watu wenye miongozo fulani ya kuishi — mila, desturi, imani na taratibu walizokubaliana kuzifuata.
Lakini kukubaliana hakumaanishi kuwa ni sahihi. Wingi haugeuzi makosa kuwa ukweli. Mapokeo hayageuzi desturi kuwa uhalali wa milele.
Tatizo si kuwa sehemu ya jamii; tatizo ni kuacha kufikiri kwa sababu tu jamii imekwisha kufikiri kwa niaba yako.
Watu wengi huzaliwa ndani ya mfumo, hukua ndani yake, na huondoka duniani bila hata siku moja kuuchambua. Wameishi kwa kufuata, si kwa kuelewa.
Jamii nyingi zimejengwa juu ya mapokeo yasiyohojiwa. Ukienda kinyume nayo unaonekana msaliti. Ukiishi tofauti unaonekana mchawi.
Ukiwa huna shauku ya kufuata makundi unaonekana una tatizo. Lakini ukweli hauhitaji kura ya maoni ili uwe ukweli.
Je, kwa sababu jamii inaamini kitu basi ni lazima kiwe sahihi? Je, kwa sababu wengi wanafanya jambo basi lina uhalali wa kimaadili?
Kama jamii itaamini katika kafara ya mzaliwa wa kwanza, je, wingi wao utabadilisha uovu kuwa wema?
Kama jamii itaishi kwa hofu na kuitangaza kama imani, je, hofu hiyo inageuka kuwa hekima? Hapa ndipo tunapaswa kusimama na kujiuliza: tunafuata ukweli, au tunafuata umati?
Ukweli mchungu ni kwamba jamii nyingi hazitawaliwi na hoja; zinatawaliwa na hofu. Hofu ya kutengwa. Hofu ya kuitwa tofauti. Hofu ya kuonekana mpinzani wa mila.
Hofu ya kuambiwa unakwenda kinyume na Mungu. Watu huishi kwa kutishiwa zaidi kuliko kuelimishwa.
Huambiwa waogope kuliko kufikiri. Leo ugonjwa unahusishwa na shetani, wanakesha kumkemea, kesho kifo kinaitwa mapenzi ya Mungu ya kwamba kampenda zaidi.
Hakuna mchanganuo wa kina; ni majibu ya haraka kwa akili zisizohoji. Lakini jamii isiyohoji haiwezi kukua. Inabaki kuzunguka kwenye duara la mapokeo yasiyochunguzwa, ikijirudia kizazi hadi kizazi bila mwelekeo mpya.
Hata hivyo, jamii si adui. Jamii ni chombo. Swali si kama uwe sehemu yake; swali ni unachangia ubora gani ndani yake.
Jichunguze. Angalia mwenendo wako. Angalia ujuzi wako. Angalia kiwango chako cha udadisi. Angalia namna unavyotumia akili yako. Angalia mchango wako halisi.
Halafu jifanye mpo watu milioni sitini wenye kiwango chako cha fikra, maamuzi na ufahamu.
Jamii hiyo itakuwa ya namna gani? Kama hamna umoja wa kiutu bali makundi ya kiitikadi, kama hamna upendo bali mashindano ya nani yuko sahihi, kama hamna uchambuzi bali ushabiki wa mapokeo, je, jamii hiyo itastahili kuitwa mwongozo wa kuishi?
Hapo ndipo ukweli unapoanza kuonekana: ubora wa jamii unaanzia ndani ya mtu mmoja mmoja.
Mabadiliko ya kweli hayawezi kuanzia kwenye kelele za umati. Hayaanzi kwenye mikutano mikubwa wala kwenye namba nyingi.
Yanaanza pale mtu mmoja anapoamua kujitambua. Unapoanza kujitambua, unagundua wewe ni nani, unaamini nini, na unasimama wapi.
Hapo ndipo unapoacha kuwa zao la jamii na kuanza kuwa mbunifu wa jamii. Siyo kila kilichorithiwa kinapaswa kuendelezwa.
Baadhi ya mifumo ilijengwa kwa mazingira ya zamani yasiyolingana na uhalisia wa sasa. Kuendelea kuifuata bila uchambuzi ni kuabudu historia badala ya kujenga kesho.
Nayaandika haya si kwa sababu sitaki kuwa sehemu ya jamii, bali kwa sababu nasimama kujenga jamii yenye umoja wa kiutu, si ushirikiano wa kundi; jamii isiyojengwa juu ya hofu bali juu ya uelewa; jamii isiyogawanywa na matabaka ya kiakili bali inayothamini fikra huru zenye uwajibikaji.
Ujenzi huu hauanzi kwa kubadili watu wengi; unaanza kwa kuvua utambulisho wa kijamii uliokujenga bila ruhusa yako na kujenga upya utambulisho wa kujitambua.
Hapo ndipo jamii mpya inaanza kuzaliwa — si kwa mapinduzi ya ghafla, bali kwa mabadiliko ya ndani.
Na kama umefika hapa na kuna kitu ndani yako kimeanza kutikisika, kama umeanza kuona kuwa kuishi kwa mapokeo si lazima zaidi ya kuishi kwa usahihi, basi huu si mwisho wa kusoma — huu ni mwanzo wa kuchukua hatua.
Usirudi kuwa yule wa jana. Chagua kujitambua. Chagua kufikiri kwa kina. Chagua kujenga jamii bora kuanzia ndani yako.
Kama uko tayari kuvua utambulisho wa kuishi kwa mazoea na kuvaa utambulisho wa kuishi kwa usahihi, basi jiunge na mchakato wa kujengwa upya kupitia King Mentorship Program.
Hii si harakati ya kupinga jamii kwa hasira; ni harakati ya kuijenga upya kwa ufahamu.
Jamii mpya haitaanza kesho kwa kelele za wengi. Itaanza leo, pale wewe mmoja utakapoamua kusimama katika usahihi wako na kuwa chanzo cha mwelekeo mpya.
Ndimi Mbulwa King'ung'e. Founder wa King Mentorship Program.
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment