“Kazi Ni Mfumo, Kusudi Ni Sababu: Ukweli Usiofundishwa Shuleni...”


Hivi unafahamu kuwa watu wengi duniani wanafanya kazi au kushughulika na mambo ambayo hayana uhusiano wowote na kusudi la kuumbwa kwao?

Wanaamka kila asubuhi, wanafanya kazi kwa bidii, wanapokea mshahara, lakini ndani yao kuna ombwe lisiloelezeka. 

Furaha haikamiliki, na mara nyingi wanahisi kama kuna kitu kikubwa wanakikosa maishani mwao. 

Kazi ni muhimu, ni njia ya kuishi, ni mfumo unaowezesha mtu kulipa bili, kuendesha familia, au kujipatia adabu. 

Lakini tatizo linapokuja pale ambapo kazi hiyo haikidhi mwito wa ndani na kusudi halisi.

Hapa ndipo mtu anapopaswa kujiuliza: Je, kile ninachofanya kila siku kinanikamilisha kama MTU?

Kinaniletea furaha ya kweli na kinafanya maisha yangu kuwa baraka kwa wengine?

Haya si maswali ya kawaida. Ni maswali yanayogusa mzizi wa uwepo wako. 

Kwa sababu watu wengi wamefundishwa kutafuta kazi, kushikilia ajira, na kupima mafanikio kwa mshahara—lakini hawajawahi kufundishwa kutafuta kusudi.

Na hapa ndipo mkanganyiko mkubwa huanza. Kwa sababu kazi inaweza kukupa kipato, lakini ikashindwa kukupa maana ya kuishi. Inaweza kukuajiri, lakini ikakuibia uhuru wa nafsi yako.

Kwa tafsri nyepesi kazi ni shughuli yoyote halali anayofanya mtu ili kujipatia kipato. 

Ni mfumo ulioundwa ili kukuweka hai, kukuwezesha kumudu gharama za maisha, na kukusaidia kuishi ndani ya jamii.

Watu wengi wanaofanya kazi wana ujuzi wa kitaaluma, wana vyeti, wameajiriwa chini ya serikali, mtu au taasisi. 

Elimu hutumika kama kibali cha kuidhinishwa kufanya kazi fulani, na mara nyingi mshahara hupimwa kwa kiasi cha elimu, si thamani ya mtu.

Hata hivyo, ukweli mchungu ni huu: hata walioelimika sana huendelea kulipwa chini ya thamani yao halisi.

Tofauti pekee ni kwamba mtu asiye na elimu huuza nguvu zake, mtu aliyeelimika huuza akili na muda wake. Lakini wote wawili bado wapo ndani ya mfumo unaopima nafasi, si thamani.

Lakini hapa ndipo wengi huchanganya kazi na kusudi, na kuishi maisha ambayo si yao kwa kweli.

Ukiachilia mbali kuhusu kazi kuna kitu kinaitwa KUSUDI. Kwa tafsiri laini kusudi ni sababu kubwa iliyosababisha maisha yako yawepo hapa duniani. 

Ni lile jambo ambalo unasukumwa kulifanya kwa ndani, unalifanya kwa furaha bila kushinikizwa, unalifanya kwa uthabiti hata pasipo kulipwa.

Kusudi halitegemei cheti, halihitaji idhini ya mtu. Kusudi ni mwito wa ndani unaokutambulisha wewe ni nani hasa.

Na jambo muhimu sana kuelewa ni hili: kusudi si lazima likupe pesa, bali linakupa maana ya maisha.

Kwa sababu kusudi hutoa thamani, na kwa kuwa watu hubadilishana fedha na kile wanachokithamini, basi ni nadra sana mtu akaishi kusudi lake kikamilifu na asilipwe. 

Na kama halilipwi, mara nyingi ni uamuzi wa ndani wa mtu mwenyewe...

Binafsi, tangu nikiwa mdogo nilijikuta napenda sana kuandika na kuelimisha jamii. Nikiwa kidato cha pili tayari nilikuwa nikiandika mada mbalimbali—si kwa sababu ya shinikizo, bali kwa msukumo wa ndani.

Kadri nilivyokua, nikagundua ukweli mmoja muhimu: uelimishaji kupitia uandishi huenda ndiyo sababu ya kuwepo kwa maisha yangu.

Ni kitu ninachokifanya kila siku kwa furaha, kwa uthabiti, bila kulazimishwa. Ndipo nikagundua kuwa nimefanikiwa kuliishi kusudi langu na kuligeuza kuwa kama kazi. 

Leo ninapata kipato, ninatimiza kusudi langu, na wakati huohuo ninarahisisha maisha ya wengine.

Ukiliishi kusudi lako kwa uhalisia, kipato chako hakikadiriwi na mtu. Una uhuru wa kuongeza kipato muda wowote. 

Unaweza kulipwa hata bila kufanya kazi moja kwa moja, kupitia mifumo uliyojiandaa. Thamani yako halisi hujitokeza wazi, na unaepuka utumwa, manyanyaso na mateso ya kazini.

Kati ya haya mawili—kuendelea kufanya kazi iliyo nje ya kusudi lako, au kuanza safari ya kugeuza kusudi lako liwe kama kazi—kipi kinaakisi maisha unayotamani kuyaishi?

Kama makala hii imekufanya ujihoji, utafakari, au uone kuwa kuna zaidi ya mshahara na ajira, basi uko tayari kwa hatua inayofuata.

Nikaribishe inbox tuzungumze kwa undani kuhusu KUSUDI LA MAISHA YAKO. Majibu unayotafuta yanaweza kuwa karibu zaidi ya unavyodhani.

Ndimi  Mbulwa  King’ung’e
Founder – King Mentorship Program
Mwalimu | Mwandishi | Muelimishaji wa Jamii
Life Coach & Consultant – Maendeleo Binafsi

📲 WhatsApp: +255 744 284 329 / 0773 284 329
🌐 Blog: kingmentorshipprogram.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...