“Kurudi Nyumbani: Safari ya Kuvunja Minyororo ya Fikra...”


Kuna watu wanaishi maisha ya kulaumu kila kitu. Wengine wanamlaumu Mungu. Wengine wanawalaumu wazazi, serikali, mfumo wa elimu, au bahati. 

Lakini ukweli mchungu ni huu: wengi wao si wavivu wala si watu wasio na uwezo. Ni zao la kile walichofundishwa tangu mwanzo.

Alipozaliwa, hakufundishwa kujitambua. Hakufundishwa kuuliza, “Mimi ni nani? Nimekuja kufanya nini?”

Badala yake, alipewa majibu tayari yaliyopikwa kabla hajajua hata kuhoji. Akaambiwa chanzo cha uhai ndicho kinapanga mustakabali wake.

Akaambiwa riziki yake imeandikwa. Akaambiwa kuna nguvu inayoweza kumpa yeye au kumnyima na kumpa mwingine.

Polepole, bila yeye kujua, akaanza kuishi kwa hofu. Hofu ya kukosea. Hofu ya kuuliza. Hofu ya kuwa tofauti. 

Akaambiwa makosa ni dhambi. Akaambiwa kuuliza ni kukosa imani. Akaambiwa kufikiri tofauti ni uasi. Na hapo ndipo alipoanza kupoteza sauti yake ya ndani.

Akaingia kwenye jamii ambayo yenyewe haijawahi kusimama kujiuliza maana ya maisha. Jamii inayorudia tu kile ilichorithi. 

Ikamwambia awe fulani. Awe kama fulani. Aishi kama fulani. Hakuna aliyemuuliza yeye anataka nini. Hakuna aliyemuuliza ana kipaji gani. Hakuna aliyemuuliza moyo wake unavuta upande gani.

Mfumo wa elimu ukampokea, lakini haukumtambua. Ukamfundisha kukariri, si kufikiri. Ukamwandaa kuajiriwa, si kuunda ajira wala kujiajiri. 

Alipoleta wazo la tofauti, akaonekana msumbufu. Alipojaribu ubunifu, akaadhibiwa. Akaanza kuamini kana kwamba kuwa tofauti ni kosa.

Akaishi maisha ambayo si yake.

Ndani anaumia. Nje anatabasamu.

Akahitimu. Hakuna kazi. Anaambiwa ajiajiri, lakini hakuwahi kufundishwa namna ya kujiajiri.

Anaambiwa awe mbunifu, lakini ubunifu wake uliwahi kukataliwa. Anaambiwa awe kiongozi wa maisha yake, lakini hajawahi kufundishwa kujiongoza.

Kisha anajikuta analalamika. Anamlaumu Mungu. Anailaumu jamii. Anailaumu dunia.

Lakini subiri kidogo.

Huwezi kujihukumu kwa kitu ambacho hukujua. Huwezi kujilaumu kwa kitu ambacho ulifundishwa kimakosa tangu mwanzo. 

Si kosa lako kwamba uliishi kwenye mfumo uliokuficha wewe ni nani. Si kosa lako kwamba uliambiwa ufuate bila kuhoji.

Lakini sasa — inakuwa jukumu lako kuamka.

Kwa sababu kuna ukweli mmoja ambao haujawahi kuambiwa kwa uwazi: wewe ndiye kiongozi halisi wa maisha yako. 

Hakuna mfumo, hakuna jamii, hakuna taasisi yenye mamlaka ya mwisho juu ya mustakabali wako isipokuwa wewe mwenyewe.

Lakini ili uwe kiongozi wa kweli, lazima urudi nyumbani.

Na nyumbani si mahali. Ni wewe.

Ni pale unapokaa kimya na kuanza kusikiliza sauti yako ya ndani. Ni pale unapoacha kuishi kwa ramani za wengine na kuanza kuandika yako. 

Ni pale unapoamua kuhoji kila imani uliyopewa bila kuichunguza. Ni pale unapokubali kwamba makosa si dhambi — ni darasa.

Kuamka si kupinga kila kitu. Kuamka ni kutambua. Ni kujua unaamini nini na kwa nini. Ni kuchagua kwa ufahamu, si kwa kurithi. Ni kuishi kwa makusudi, si kwa mazoea.

Huu si wakati wa kulaumu tena.
Huu ni wakati wa kujirudisha kwako.

Kwa sababu dunia haihitaji nakala nyingine. Inahitaji wewe halisi. Dunia haihitaji watu wanaoishi kwa hofu. Inahitaji watu waliogundua sauti yao na wakaamua kuishi nayo.

Na hapo ndipo mabadiliko ya kweli huanza — si kwenye kelele, bali kwenye utambuzi.

King Mentorship Program si jukwaa la maneno matamu. Ni jukwaa la kuamsha fikra. 

Ni mahali pa kuvunja minyororo ya kiimani, kimawazo na kijamii. Ni mahali pa kumrudisha mtu kwenye uhalisia wake. Si kwa kumfundisha cha kufikiri, bali kwa kumfundisha jinsi ya kufikiri.

Kwa sababu mtu anapojitambua, hapotei tena. Hapangiwi tena. Haishi maisha ya kuigiza tena.

Anakuwa huru. Na uhuru wa kweli huanza ndani.

Karibu tuanze safari ya kurudi nyumbani — kwako.

Ndimi Mbulwa King'ung'e.
Mawasiliano: 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...