Matatizo Hayakuui — Mwitikio Wako Ndiyo Huamua Hatima Yako...

Upo hapo ulipo leo, na unapitia hali unazopitia, kwa kiasi kikubwa kama matokeo ya mwitikio wako mwenyewe dhidi ya changamoto mbalimbali ulizokutana nazo njiani.

Watu wengi hudhani matatizo ndiyo yanayoamua hatima ya maisha yao, kumbe si matatizo yenyewe—bali mwitikio wao dhidi ya matatizo hayo.

Kwa kuwa  matatizo ni sehemu ya maisha ya MTU, basi swali la msingi si kama utakumbana na changamoto, bali ni namna gani utaitikia changamoto hiyo.

Mwitikio wako leo, ndiyo unaandika hadithi ya kesho yako.

Ukweli usiopingika ni kwamba: Mwitikio chanya huzaa matokeo chanya. Mwitikio hasi huzaa matokeo hasi.

Kanuni ya maisha inasema: “Matendo yako ni mwitikio wa mawazo yako.”

Na matendo yako ndiyo huamua matokeo unayopata.

Kwa hiyo, ikiwa hutabadilisha namna unavyoitikia matatizo, usitarajie mabadiliko ya matokeo katika maisha yako.

Hebu sasa tuangalie aina nne za miitikio ya watu wanapokumbana na matatizo, miitikio ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa chanzo cha kusuasua kwa watu wengi maishani.

1. Kulidharau Tatizo"

Hili ni kundi la watu wanaoishi kwa usemi usemao: “Liwalo na liwe.”

Watu hawa huona wazi kuwa kuna kitu hakiko sawa katika maisha yao—kipato ni kidogo, mahusiano hayana mwelekeo, au maisha hayana utulivu—lakini bado huchagua kupuuza tatizo wakiamini kuwa kupuuza ni suluhisho.

Lakini jiulize: Vipi kama “liwalo” halitakuwa jema? Vipi kama kupuuza kutazalisha matokeo mabaya zaidi? Ni nani atakayebeba gharama za matokeo hayo kama si wewe mwenyewe?

Kupuuza tatizo hakuliondoi. Kupuuza hulifanya tatizo likue kimya kimya hadi liwe janga.

Unaona unapata kipato cha chini lakini hufanyi mabadiliko.

Unaona mahusiano yako hayana mwelekeo lakini huchukui hatua.

Unaona unateseka kiroho, kiakili na kimwili lakini unaendelea kuahirisha maamuzi.

Ukweli ni huu: Tatizo lisilokabiliwa leo, hulazimisha kulipia gharama kubwa zaidi kesho.

2. Kulaumu Wengine

Hili ni kundi la watu waliobobea katika kulaumu:
wazazi, ndugu, waajiri, jamii, serikali—na hata Mungu.

Swali la msingi ni hili: Ni lawama zipi zimewahi kubadilisha uhalisia wa maisha ya mtu?

Hakuna kiwango cha lawama kinachoweza kutatua tatizo.

Ndiyo, huenda hukulelewa katika mazingira bora.
Ndiyo, huenda ulipata mwajiri asiyekuthamini.
Ndiyo, huenda mfumo una mapungufu.

Lakini ukweli mchungu ni kwamba: Sehemu kubwa ya matatizo yetu yanahusiana moja kwa moja na maamuzi yetu wenyewe.

Kulaumu hakubadili hali. Kuwajibika ndiko kunakobadili mwelekeo.

Cha kusikitisha zaidi, baadhi ya watu wamefikia hatua ya kumbebesha Mungu lawama: hawapewi pesa, hawapewi wake au waume, hawapewi mafanikio.

Lakini ukweli ni huu: Ulilikuta dunia ipo. Ulilikuta maisha yapo. Ulilikuta rasilimali zipo.

Kile kinachokosekana mara nyingi si neema—
ni uelewa, uamuzi, na uwajibikaji binafsi.

3. Kuwekeza Nguvu Kwenye Tatizo Badala ya Chanzo

Hawa ni watu wanaopambana na matokeo, badala ya kushughulikia chanzo.

Ni muhimu kufahamu kuwa: Kila tatizo lina sababu. Hakuna matokeo yasiyo na kichocheo chake.

Unapopambana na umaskini bila kurekebisha fikra za uhaba na matumizi yasiyo sahihi, unapoteza nguvu.

Unapopambana na hali ngumu bila kurekebisha mtazamo wako, unapambana na kivuli.

Umaskini ni zao la fikra.
Hali ngumu ni zao la mtazamo.
Matokeo mabaya ni zao la mifumo mibovu ya ndani.

Chanzo kikubwa cha matatizo mengi yanayotukumba ni: Ujinga wa kiroho. Ujinga wa kujitambua. Ujinga wa masuala ya fedha. Ujinga wa mahusiano na ndoa.

Suluhisho si kupambana na tatizo kama tatizo—
suluhisho ni kurudi kwenye chanzo chake.

4. Kulihofia Tatizo

Je, umewahi kuona tatizo likitatuliwa kwa kulihofia? Jibu ni hapana.

Hofu huua ujasiri, huua maamuzi, na huua maendeleo.

Mtu huanza kudhani amepata amani kwa kulikimbia tatizo, ilhali tatizo bado lipo palepale.

Mahusiano yakivunjika, unaogopa kuanza upya.
Uwekezaji ukishindikana, unaogopa kujaribu tena.

Lakini ukweli ni huu: Maisha hayapimwi kwa kuepuka makosa, bali kwa uwezo wa kujifunza, kurekebisha, na kusonga mbele.

Hofu haitatui tatizo. Hulikuza.

Tatizo si adui wako. Mwitikio wako ndiyo unaoweza kuwa adui au rafiki yako.

Ukibadilisha mwitikio wako: mawazo hubadilika, matendo hubadilika na matokeo hubadilika.

Na hapo ndipo maisha yako huanza kubadilika kwa kweli.

Ahsante sana kwa kuwa mwanafamilia wa masomo haya ya kujenga Utambuzi.

Ukitaka kujifunza Zaidi usisite kuwasiliana NAMI.

Ndimi Mbulwa King'ung'e
Founder – King Mentorship Program
Mwalimu | Mwandishi | Muelimishaji wa Maendeleo Binafsi
Life Coach & Consultant

📲 WhatsApp: 0744 284 329 / 0773 284 329
🌐 Blog: kingmentorshipprogram.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...