Tatizo Sio Imani, Tatizo Ni Mfumo Unaoiunda...


Kuna nguvu kubwa sana ndani ya imani. Imani inaweza kumuinua MTU kutoka hali ya chini kabisa na kumpeleka kwenye kilele cha mafanikio. 

Lakini imani hiyo hiyo, ikifundishwa vibaya, inaweza kumfanya mtu abaki katika mzunguko wa utegemezi, hofu na kushindwa bila yeye mwenyewe kujua. 

Hapa ndipo watu wengi hukosea; wanadhani tatizo ni imani, kumbe tatizo ni mfumo wa mafundisho unaoongoza imani hiyo.

Lazima tukubali ukweli mmoja mzito: akili ya MTU hujengwa na kile anachofundishwa mara kwa mara. 

Ukimfundisha mtu kuhoji, atakuwa mtafiti. Ukimfundisha kuogopa, atakuwa mtiifu wa hofu. Ukimfundisha kusubiri, atakuwa mwathirika wa muda. 

Ukimfundisha kuwajibika, atakuwa mbunifu wa maisha yake mwenyewe. Hivyo basi, mafundisho si maneno tu; ni uhandisi wa fikra.

Kwa muda mrefu, kumekuwa na mifumo inayowafanya watu waamini kwamba utii ni bora kuliko ufahamu. 

Watu wanaelekezwa kupokea bila kuchunguza, kuamini bila kutafakari, na kufuata bila kuelewa. 

Hili linaonekana kama unyenyekevu, lakini kisaikolojia linazalisha utegemezi wa kiakili.

 MTU anayezuiwa kuuliza maswali polepole hupoteza uwezo wa kufikiri kwa kina. Na pale uwezo wa kufikiri unapodhoofika, hata maamuzi ya maisha yanakuwa dhaifu.

Hakuna ukuaji bila ufahamu. Hakuna mafanikio bila uwajibikaji. Hakuna mabadiliko bila hatua.

Hata kama mtu ana imani kubwa kiasi gani, kama hafundishwi kanuni za maisha, atabaki akizunguka kwenye mzunguko ule ule. 

Maisha yana misingi isiyobadilika: thamani huzaa matokeo, juhudi huzaa mavuno, nidhamu huzaa thamani, maarifa huzaa nguvu. Hakuna mfumo wa kiroho unaoweza kufuta kanuni hizi za asili.

Tatizo kubwa zaidi hutokea pale mtu anapoanza kumtegemea mtu mwenzake kuliko kanuni.

Historia inaonyesha kwamba kila jamii iliyojenga utamaduni wa kumwamini mtu zaidi ya ukweli huishia kuvunjika. 

MTU ana mipaka. MTU anakosea. MTU ana tamaa. Lakini ukweli haupindishwi na hisia. Ukiona watu wanaogopa kuuliza maswali juu ya maamuzi ya viongozi wao, ujue tayari mfumo umeanza kuwafanya wafuasi badala ya kuwafanya wanafikra.

Kuna pia aina ya mafundisho yanayojenga saikolojia ya kusubiri. Watu wanaaminishwa kwamba wakati wao bado haujafika, kwamba hawapaswi kuchukua hatua hadi ishara maalum itokee. 

Lakini muda hausubiri mtu, na maisha hayabadiliki kwa kusubiri. Maisha hubadilika kwa kujiandaa, kujifunza, kufanya na kurekebisha. 

Ukimfundisha mtu kusubiri badala ya kujiendeleza, unamnyima miaka ya mafanikio yake.

Nimeona watu wakiamini kwamba mafanikio ya kifedha ni tukio la ghafla, kwamba ustawi ni zawadi isiyohitaji mchakato. 

Lakini ukweli ni kwamba fedha hufuata thamani, na thamani hutokana na ujuzi, tabia na tija.

Hakuna neno linaloweza kuchukua nafasi ya kazi. Hakuna usemi unaoweza kuchukua nafasi ya uwezo. Ukimwambia mtu atapata bila kujenga, unamjengea ndoto isiyo na mizizi.

Pia kuna hatari ya kufundisha picha ya hofu badala ya picha ya ukuaji. Hofu ni njia rahisi ya kudhibiti, lakini si njia ya kujenga. 

MTU  anayesukumwa na hofu hawezi kuwa mbunifu, hawezi kuwa jasiri, na hawezi kubeba maono makubwa. Lakini MTU anayefundishwa kuwajibika, kujifunza na kuchambua huwa huru hata akiwa katikati ya changamoto.

King Mentorship Program haisimami upande wa dini wala dhidi ya dini. Inasimama upande wa ukuaji wa mtu. 

Inasimama upande wa akili iliyo huru. Inasimama upande wa uwajibikaji. Lengo si kubomoa imani ya mtu, bali kuondoa ukungu kwenye fikra zake.

Maana imani bila ufahamu hugeuka mzigo, lakini imani yenye ufahamu hugeuka nguvu.

Mtu anayekua kweli huonekana kwa matokeo. Maamuzi yake yanakuwa bora. Kazi yake inakuwa na tija. Lugha yake inakuwa na busara. Tabia yake inakuwa na uthabiti. 

Kama miaka inapita lakini hakuna ukuaji wa akili, hakuna ongezeko la thamani, hakuna maboresho ya maisha — basi kuna mahali mafundisho hayakujenga ipasavyo.

Huu si wakati wa kubishana; huu ni wakati wa kutafakari. Je, mafundisho unayopokea yanakuza uwezo wako au yanakuongezea utegemezi? 

Je, unafundishwa kufikiri au kufuata? Je, umejengwa kuwa mbunifu wa maisha yako au mtazamaji wa maisha ya wengine?

Mabadiliko ya kweli huanza pale mtu anapoacha kulaumu mfumo na kuanza kuchunguza fikra zake. 

Lakini uchunguzi huo hauwezekani kama mfumo wenyewe unazuia maswali. Ndiyo maana mapinduzi makubwa ya maisha huanza na mapinduzi ya fikra.

Na hapo ndipo uzito wa King Mentorship Program ulipo. Siyo programu ya maneno matamu. Siyo programu ya kuwapa watu matumaini ya hewa. 

Ni mfumo wa kukuza akili, kurekebisha mtazamo na kujenga mtu anayeweza kusimama peke yake, kufikiri kwa kina, kuchukua hatua kwa ujasiri na kuzalisha matokeo halisi.

Kwa sababu mwisho wa siku, lengo si kuwa na wafuasi wengi. Lengo ni kuwa na watu waliokomaa kiakili, waliotulia kimaamuzi na wenye uwezo wa kuathiri dunia yao kwa busara.

Sasa jiulize kwa uaminifu kabisa: Je, mafundisho uliyo nayo yanakufanya uwe bora kila mwaka, au yanakuweka mahali pamoja huku ukihisi uko salama?

Hapo ndipo jibu la safari yako linapoanzia.

Ndimi Mbulwa King'ung'e: Founder wa King Mentorship Program.

Mawasiliano: 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...