“Unaishi Ulichotengenezwa Uwe, au Ulichoumbwa Kuwa?”


Moja ya ukweli mgumu ambao nimeujua kwa kina ni huu: watu wengi hawateseki kwa sababu hawana uwezo, wanateseka kwa sababu ya vita ya ndani wanayoishi nayo kila siku.

Si vita ya pesa, si vita ya mazingira, si vita ya kukosa elimu. Ni vita ya kiutambuzi—vita kati ya wewe halisi na wewe uliyotengenezwa uwe. 

Na mtu akishindwa vita hii, haijalishi ana shahada ngapi, kazi gani, au thamani kiasi gani, ndani yake hubaki mtupu.

Kabla hujaelekezwa usome nini, kabla hujaambiwa ufuate njia gani ya maisha, kabla hujaaminishwa mafanikio ni nini, kabla hujaambiwa uamini nini, kulikuwa na wewe halisi. 

Kulikuwa na mwelekeo wako wa asili, msukumo wako wa ndani, na sauti isiyoonekana iliyokuwa ikikuita kuelekea jambo fulani. 

Huo ndio wito wa ndani. Tatizo ni kwamba mara nyingi wito huo hauendani kabisa na kile ambacho mifumo ya elimu, dini, malezi na jamii imekutengeneza uwe. Ndipo mgongano huanza.

Mifumo inafanya kazi yake vizuri sana—inakupa mwelekeo, inakupa tafsiri, inakupa mipaka, inakupa matarajio. Lakini haikupi ruhusa ya kujitambua.

Inakutengeneza uwe kitu fulani na inatarajia ubaki hapo. Wakati mwingine kile unachotengenezwa kuwa hakifanani hata kidogo na wewe halisi.

Hapo ndipo mtu hujikuta anapambana kimya kimya, akiuliza maswali asiyothubutu kuyauliza hadharani: Je, nikae hapa kwa sababu ndiyo njia salama, au nifuatilie kile kinachonichoma ndani?

Je, nichague mshahara au nichague mwito wa ndani? Je, nikubali walivyonizoea au niwe tayari kuvunja picha waliyonijengea?

Watu wengi huogopa kuchagua wito wa ndani. Si kwa sababu hawauoni, bali kwa sababu gharama yake inaonekana kubwa.

Hukumu za watu zinaumiza, kuanzia upya kunaogopesha, na kuacha njia iliyozoeleka kunahitaji ujasiri ambao wachache huuthubutu.

Ndiyo maana watu wengi huishia kuishi maisha ambayo si yao. Wanafanya kazi, lakini hawana msukumo. Wanajituma, lakini hawana amani.

Wanapata kipato, lakini hawana maana. Wanacheka mbele za watu, lakini kwa siri wanajilaumu, wanajuta, na wanajishusha thamani yao wenyewe.

Hii huonekana hata kazini. Mtu anafanya kile alichotengenezwa afanye, lakini hakifanyi kwa uweledi wa ndani. 

Anaishi kwa kulazimika, si kwa mwito. Wengine hata wananyanyaswa na mabosi, wanapokea kipato cha chini kuliko uwezo wao, au wanafanya “vizuri” kwa macho ya jamii lakini wanajisikia wamekufa ndani. 

Haya si matukio ya bahati mbaya. Hizi ni dalili za mtu anayeishi nje ya wito wake wa ndani.

Niseme ukweli bila kujificha. Mimi ni mwalimu mtaalamu. Nimefundishwa na mfumo rasmi, na ningeweza kuendelea tu kufundisha kwa sababu ndiyo njia niliyotengenezwa nipitie. 

Lakini ndani yangu kulikuwa na maswali ambayo hayakuwa darasani, uelewa ambao haukuwa kwenye mitaala, na msukumo wa kuwasaidia watu wajijue wao ni nani kabla ya kuwaambia wafanye nini.

Ningeweza kupuuza sauti hiyo na kuishi maisha salama, lakini ningekuwa mwalimu mzuri huku nikiwa mtu aliyepotea ndani yake mwenyewe.

Ndiyo maana nikaanzisha King Mentorship Program. Sio kwa ajili ya umaarufu, bali kwa sababu niliamua kuifuata nafsi yangu halisi hata kama haikuwa njia iliyokuwa imezoeleka.

Kama leo unaona mambo hayaendi, kama unaamka asubuhi bila msukumo, kama unaanza kujiuliza kimya kimya kama uko sahihi ulipo, au kama umeanza hata kupoteza maana ya maisha, usijilaumu. 

Tatizo si wewe. Tatizo ni kwamba hukuwahi kufundishwa kujitambua.

Hakukuwa na mtu wa kukuuliza maswali sahihi, hakukuwa na mfumo wa kukuonesha tofauti kati ya kile ulichofundishwa uwe na kile ulichoumbwa uwe. 

Na bila utambuzi binafsi, mtu huishi maisha ya watu wengine bila hata kujua.

Ndiyo maana King Mentorship Program ipo. Haitakufanya uwe kila kitu wala kukupa ndoto bandia, lakini itakupa kitu ambacho ni hatari zaidi: maswali sahihi. 

Maswali yatakayokurudisha kwa wewe halisi, kwa uwezo wako, na kwa maana ya kuishi kwako.

Maswali ambayo yakishajibiwa kwa uaminifu, huwezi tena kuendelea kuishi maisha ya uongo.

Uamuzi sasa uko mikononi mwako. Unaweza kuendelea kuishi kama ulivyotengenezwa, au unaweza kuanza kuishi kama ulivyoumbwa. 

Lakini kumbuka hili—gharama ya kuishi nje ya wito wako hulipwa kwa maisha yako yote.

Kama unataka kuishi kwa maana, kuacha alama, na kubadilisha maisha yako pamoja na jamii yako, jiunge na kozi za King Mentorship Program sasa.

Mawasiliano: 0744 284 329.

Ndimi, Mbulwa King’ung’e

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...