“Gereza Lisiloonekana: Jinsi Picha Uliyojijengea Inavyoamua Ukubwa wa Maisha Yako...”



Kuna gereza moja ambalo watu wengi wanaishi ndani yake maisha yao yote bila hata kutambua kuwa wamefungwa. 

Gereza hilo halina kuta, halina minyororo, halina walinzi wanaolinda milango yake. 

Ni gereza lisiloonekana, lakini lina nguvu kuliko magereza mengi tunayoyaona. Gereza hilo linaitwa picha uliyojijengea kuhusu wewe mwenyewe.

Ndani ya akili yako kuna taswira fulani kuhusu wewe ni nani, unaweza nini, na una thamani kiasi gani katika dunia hii. 

Taswira hiyo ndiyo inayoamua ukubwa au udogo wa maisha yako, hata kabla hujajaribu kufanya jambo lolote.

Kila mtu hubeba picha fulani moyoni mwake kuhusu yeye mwenyewe. Picha hiyo si lazima iwe sahihi, lakini huwa na nguvu ya ajabu sana. 

Ndani yake kuna majibu ya maswali mengi ambayo mara nyingi hatujiulizi kwa sauti: Je, mimi ni mtu mwenye uwezo au mtu wa kawaida tu? 

Je, ninaweza kufikia mambo makubwa au maisha yangu yataishia kwenye mipaka midogo? 

Je, nina hadhi ya kusikilizwa na kuthaminiwa au mimi ni mtu ambaye lazima akubali kila anachopewa na dunia? 

Maswali haya yanaonekana kama hayana maana, lakini majibu yake yanakuwa msingi wa maamuzi mengi tunayofanya kila siku.

Watu wengi hudhani kwamba maisha yao yanaamuliwa na mazingira waliyozaliwa, elimu waliyoipata, au bahati waliyo nayo. 

Lakini kwa kiwango kikubwa zaidi, maisha ya mtu huanza kuamuliwa na namna anavyojiona ndani yake mwenyewe. 

Akili ya MTU ina tabia ya kulinda picha aliyojijengea kuhusu nafsi yake. 

Kama mtu anaamini ndani yake kuwa yeye ni mdogo au hana uwezo mkubwa, akili yake itaanza polepole kutafuta sababu za kuthibitisha imani hiyo. 

Ataanza kuona vikwazo kila mahali, ataogopa kuchukua hatua kubwa, na hata fursa zitakapokuja mbele yake atazikwepa bila kujua kwa sababu ndani yake tayari anaamini kuwa mambo makubwa si yake.

Kwa upande mwingine, mtu anayejijengea picha ya mtu mwenye uwezo, mwenye thamani, na mwenye kusudi kubwa maishani huanza kuishi kwa mtazamo tofauti kabisa. 

Hii haimaanishi kuwa anakuwa na maisha rahisi zaidi kuliko wengine, bali ina maana kuwa anakutana na changamoto kwa mtazamo tofauti. 

Anapokutana na ugumu haumaanishi kwake kuwa hawezi; badala yake anaona kama ni sehemu ya safari ya kukua. 

Ndani yake kuna imani ya kimya kimya inayomwambia kuwa anaweza kujifunza, anaweza kubadilika, na anaweza kufikia kiwango kikubwa zaidi kuliko alichokuwa jana.

Mwandishi mashuhuri wa maendeleo binafsi Brian Tracy aliwahi kusema ukweli mzito sana: “Huwezi kwenda mbali zaidi ya pale ulipoishia kujiona.”

 Usemi huu unaonekana rahisi, lakini ndani yake kuna kanuni moja ya msingi sana kuhusu maisha ya MTU. 

Kiwango cha maisha unachokubali ndani ya nafsi yako huwa kama dari ya kioo juu ya kichwa chako. 

Unaweza kufanya juhudi nyingi, unaweza kufanya kazi kwa bidii sana, lakini kama ndani yako bado unajiona kuwa mtu wa kiwango fulani tu, hatua zako nyingi zitaishia kurudi kwenye kiwango hicho hicho.

Ndiyo maana mara nyingi tunaona watu wenye uwezo mkubwa lakini wanaishi maisha madogo kuliko uwezo wao halisi. 

Tatizo mara nyingi si ukosefu wa akili, vipaji, au fursa. Tatizo huwa ni picha waliyoijenga ndani yao kuhusu wao ni nani. 

Kama mtu ameishi miaka mingi akiamini kuwa yeye si mtu wa mafanikio makubwa, hata akipewa nafasi kubwa anaweza kuanza kujiharibia mwenyewe bila kujua. 

Ataanza kusita, ataogopa kufanya maamuzi makubwa, au ataacha kabisa kujaribu kwa sababu ndani yake kuna sauti inayomwambia kuwa yeye si mtu wa kiwango hicho.

Lakini historia ya maisha ya Watu inaonyesha jambo moja la kuvutia sana: mtu anapobadilisha picha yake ya ndani, maisha yake ya nje huanza kubadilika polepole. 

Hii ndiyo sababu watu wengine huanza safari ya mafanikio si kwa kubadilisha mazingira yao kwanza, bali kwa kubadilisha namna wanavyojiona. 

Wanajifunza kujithamini zaidi, wanaanza kuamini uwezo wao, na wanaanza kujiona kama watu wanaoweza kuchangia kitu kikubwa katika dunia. 

Kadiri picha hiyo mpya inavyozidi kuwa wazi ndani yao, ndivyo tabia zao, maamuzi yao, na hata mwelekeo wa maisha yao unavyoanza kubadilika.

Ni muhimu kuelewa kuwa matendo yako mengi katika maisha ni kivuli cha jinsi unavyojiona. 

Mahusiano unayokubali, mipaka unayoweka au kushindwa kuweka, ndoto unazothubutu kufuatilia, na hata kiwango cha mapato unachokubali mara nyingi vinaendana sana na picha uliyojijengea ndani yako. 

Kama ndani yako unaamini una thamani ndogo, utaanza kuvumilia mambo ambayo mtu anayejithamini asingevumilia. 

Kama ndani yako unaamini unaweza kufikia mambo makubwa, utaanza kuchukua hatua ambazo watu wengi wanaogopa kuchukua.

Kwa lugha rahisi sana, ulimwengu wa nje unaakisi ulimwengu wa ndani. Kabla maisha hayajabadilika nje, mara nyingi mabadiliko huanza kimya kimya ndani ya fikra za mtu. 

Picha mpya ya nafsi yake huanza kuota mizizi akilini mwake, na polepole picha hiyo huanza kuathiri kila anachofanya. 

Ndoto zake zinakuwa kubwa zaidi, ujasiri wake unaongezeka, na hatua zake zinaanza kuelekea kwenye maisha mapana zaidi.

Kwa hiyo swali muhimu ambalo kila mtu anapaswa kujiuliza si tu kuhusu ndoto zake, bali kuhusu picha anayojijengea ndani yake mwenyewe. 

Je, unajiona kama mtu wa kawaida anayesukumwa na mazingira, au unajiona kama mtu mwenye uwezo wa kuunda maisha yake kwa makusudi?

Je, ndani yako unaishi kama mshindi au kama mtu aliyekubali mipaka aliyowekewa na dunia? 

Kwa sababu ukweli mmoja unabaki palepale: maisha yako ya baadaye yatafuata kwa karibu sana picha unayoendelea kuijenga ndani yako leo. 

Ukibadilisha picha hiyo, taratibu utaanza kubadilisha mwelekeo mzima wa maisha yako. 

Mbulwa King'ung'e Founder King Mentorship Program

Mawasiliano:0744284339

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...