KUISHI BILA SURA MBILI...


Tatizo la MTU halijawahi kuwa dunia. Halijawahi kuwa mfumo. Halijawahi kuwa mazingira. 

Tatizo la MTU ni kukimbia ukweli wake mwenyewe.

Kwa sababu anaishi katika mgawanyiko wa ndani. Anasema kitu huku akijua kabisa haishi kile anachosema. 

Anakemea kwa sauti kubwa yale ambayo ndani yake anayapenda.

Hapo ndipo usanii unaanzia.

Msanii si lazima awe jukwaani. Msanii ni yule MTU anayejenga taswira ya maadili asiyoishi. Ni yule MTU anayekemea kwa sauti kubwa makosa yale yale anayoyaficha moyoni. 

Ni yule MTU anayehukumu wengine kwa ukali, si kwa sababu anachukia kosa, bali kwa sababu anataka kujiweka mbali na kivuli chake mwenyewe.

Mgawanyiko huu wa ndani ndio chanzo cha unafiki. Na unafiki hauanzi kwa kumdanganya mwingine — unaanzia pale unapojidanganya mwenyewe.

MTU anapokosea, mara nyingi hutafuta kitu cha kulaumu. Mazingira. Historia. Mfumo. Watu wengine. Bahati. 

Lakini mara chache sana hukaa kimya na kusema: nimechagua hivi kimakosa. Kukubali uchaguzi wako ni hatua ya kwanza ya kuwa mtu halisi.

Ukiondoa uwajibikaji binafsi, umeondoa utu. Kwa sababu utu haujengwi kwa matamanio, bali kwa maamuzi. 

Maamuzi yako yana uzito kwa sababu ni yako. Kama si yako, basi hata mafanikio yako si yako.

Huwezi kuchagua lawama ziwe za dunia halafu sifa ziwe zako. Ama ukubali nguvu ya kuchagua, ama ukubali kuwa wewe ni kivuli cha mazingira.

Watu wengi wanaishi kama waathirika wa kila kitu isipokuwa wao wenyewe. Lakini mtu halisi haishi kama mwathirika wa milele. 

Anaweza kukubali aliumizwa, lakini hakubali kuendelea kujificha nyuma ya maumivu. Anaweza kukubali alidanganywa, lakini hakubali kuendelea kuishi kwa lawama. Anaweza kukiri alikosea, bila kujenga falsafa ya kujitetea.

Uhalisia si ukamilifu. Uhalisia ni umoja wa ndani na nje. Unachosema ndicho unachoishi.
 
Unachokataa hadharani ndicho unachokataa gizani. Ukisema unaamini kitu, maisha yako yaonyeshe hivyo bila kushinikizwa. 

Kama bado huwezi kuishi kile unachosema, basi kuwa mkweli na sema bado niko safarini — si kujenga taswira ya uongo.

Kuna unafiki mwingine wa kimawazo unaoishi ndani ya jamii: kuikataa dunia huku ukiitegemea kwa kila pumzi. 

Wapo wanaosema maisha hayana maana, lakini wanapambana kuendelea kuishi. Wanapenda raha. Wanatafuta mafanikio. Wanahofia maumivu.

Wanapokaribia kupoteza uhai hushikilia kwa nguvu. Hili linaonesha ukweli mmoja tu — tatizo si dunia, tatizo ni mkanganyiko wa ndani.

Dunia ni uwanja wa maamuzi. Ni sehemu ambayo tabia inakuwa matokeo. Ni eneo ambalo fikra zako zinageuka historia yako. 

Ukiishi bila kuelewa jukumu lako ndani yake, utaanza kuilaumu kwa hali uliyoichagua mwenyewe.

Watu wengi wanaishi kwa kuiga. Wanaiga sauti, mitazamo, misimamo, hata hasira. Hawajawahi kukaa peke yao na kuuliza: mimi ni nani bila kelele za wengine? 

Kuiga kunarahisisha maisha, lakini kunafuta utu. Na pale utu unapofutika, usanii huanza kuonekana kama uhalisia.

Mtu halisi ni yule anayethubutu kujiona bila mapambo. Anayethubutu kukubali mapungufu yake bila kuyageuza kuwa falsafa ya kujitetea.

Anayejenga tabia kabla ya kujenga taswira. Anayejua kuwa thamani ya kweli haitokani na maneno yake, bali na uthabiti wa maisha yake.

Jamii yenye wasanii wengi huwa na kelele nyingi lakini mabadiliko machache. Watu huzungumza sana kuhusu maadili, lakini hawabadiliki. 

Lakini jamii yenye watu halisi huanza kimya kimya. Kila mmoja anaanza na nafsi yake. Hawajengei hadhira — wanajenga misingi.

Mwisho wa siku, historia ya mtu haipimwi kwa alichokemea, bali kwa alichoishi. 

Haipimwi kwa alichosema angefanya, bali kwa alichorudia kufanya hata pasipo kushuhudiwa.

Hapa ndipo uchaguzi wako ulipo.

Kuendelea kuwa msanii wa maadili, au kuwa mtu halisi anayebeba uzito wa maamuzi yake.

Mission ya King Mentorship Program ni moja: kujenga watu wanaolingana ndani na nje. Watu wanaoweza kusimama bila kuvaa sura mbili. Watu ambao ukweli wao hauhitaji ulinzi wa maneno mengi.

Swali halijabadilika, na halitaisha kwa kizazi hiki:

Wewe ni msanii — au ni mtu halisi?

Ndimi Mbulwa King'ung'e founder wa King Mentorship Program.

Mawasiliano: 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...