MIMI NI NANI? — Mapinduzi ya Ndani Dhidi ya Mfumo
Fikiria umeletwa duniani ukiwa mzima, kamili, ukiwa na uwepo wako halisi. Ukapewa jina kabla hujajijua.
Watu wakakuita kwa jina hilo kwa miaka mingi, wakalizoea, wakalithamini au wakalidharau—lakini hakuna aliyeketi nawe kukuuliza: Wewe ni nani?
Ukalelewa katika jamii iliyokutambua kwa jina, si kwa kiini chako. Ukavishwa utambulisho kabla hujaunda utambuzi. Ukapewa maelekezo kabla hujapewa nafasi ya kujitambua.
Ukaingizwa katika imani au mtazamo fulani wa kiitikadi uliokueleza wewe ni mkosefu, bila kukuonyesha kosa lako ni lipi.
Ukaanza kubeba mzigo wa hukumu usiyoielewa. Hukujua ulikuwa nani; ukajua tu ulipaswa kuwa nani.
Ukaenda shule. Nako hukuelezwa wewe ni nani. Uliandaliwa uwe “Fulani”. Ulipewa mwelekeo uliopimwa kwa alama, ukawekwa kwenye mizani ya ufaulu na kushindwa.
Ukaambiwa una akili au huna. Ukaambiwa una uwezo au huna. Ukaanza kuamini hukumu za nje kuliko sauti ya ndani.
Ulikosea jambo usilolielewa, ukaadhibiwa. Ukahukumiwa kwa vigezo usivyovitengeneza. Ukapewa majina yasiyo yako. Ukabeba fedheha isiyozaliwa ndani yako bali iliyotengenezwa na matarajio ya wengine.
Ukakomaa. Ukahitimu. Ukafika chuo. Ukatengenezwa kwa miaka mingi uwe mtu fulani. Lakini ulipotoka, soko halikukutambua. Mtaa haukukujua.
Ulichosomea hakikuzaa; kilikuacha katikati ya matarajio na uhalisia. Ukagundua kitu cha kutisha: yule mtu uliyetengenezwa uwe hana mahali pa kusimama.
Ukatafuta kazi. Ukapata. Mshahara mdogo. Unafanya kazi si kwa sababu unaishi wito wako, bali kwa sababu mfumo unahitaji uendelee kuzunguka ndani yake. Ndani yako kuna sauti isiyonyamaza: Kuna kitu hakipo sawa.
Unajaribu kupambana, lakini hamasa inakauka. Maisha hayaendi kwa mtiririko. Unafanya kazi bila furaha.
Unatimiza wajibu bila utimilifu. Hapo ndipo mgogoro mkubwa unaanza—mgogoro wa nafsi.
Mtu wa ndani anampinga mtu wa nje.
Mtu wa nje ni yule uliyetengenezwa uwe.
Mtu wa ndani ndiye wewe halisi.
Hapa ndipo mapinduzi huanza.
Jiulize kwa uaminifu usio na hofu:
Kama ungevua vyeti vyote, kama ungevua majina yote, kama ungeondoa hukumu zote za jamii, kama ungekaa kimya mbele ya maisha bila kelele za mfumo—ungekuwa nani?
Usijiulize unaitwa nani. Hilo ni swali la uso.
Jiulize wewe ni nani. Hilo ni swali la kiini.
Fikiria wewe ndiye MTU wa kwanza. Hakuna mtaala. Hakuna alama. Hakuna soko la ajira. Hakuna matarajio ya familia. Ni wewe na maisha. Ni wewe na dunia. Ni wewe na asili.
Ungechagua kuishi vipi? Ungekuwa mtu wa aina gani? Ungejenga nini? Ungetumikia nini? Ungeamini nini kuhusu uwezo wako?
Ukweli ambao wengi wanaogopa kuusikia ni huu: kila mmoja wetu alizaliwa akiwa na ukubwa ndani yake. Ukubwa huo haukutegemea cheti. Haukuhitaji kibali cha mfumo. Lakini ulididimizwa.
Ulifunzwa utake ruhusa ya kuwa vile ulivyo. Ulifundishwa kufuata njia zilizochongwa na wengine hata kama hazikufaa.
Waliotengeneza mifumo wanajua kitu kimoja: mtu halisi akijitambua hawezi kudhibitiwa kwa urahisi. Mtu anayejijua haishi kwa hofu. Haishi kwa kulinganisha. Haishi kwa kushindana na kivuli chake mwenyewe. Anaishi kwa kusudi.
Ndiyo maana safari ya kujitambua ni ya hatari kwa mfumo, lakini ni ya ukombozi kwa nafsi.
Katika falsafa ya King Mentorship Program, hatutoi majibu mepesi. Hakuna anayekuambia wewe ni nani. Hakuna anayekuchorea ramani ya maisha yako.
Tunakupa kitu hatari zaidi—maswali. Maswali yanayokuvua tabaka moja baada ya jingine. Maswali yanayokurudisha kwenye chanzo. Maswali yanayokulazimisha kukutana na wewe bila kinga.
Kwa sababu ukweli ni huu: hakuna mfumo utakaokuokoa dhidi ya upotevu wa nafsi kama wewe mwenyewe hujachagua kujitafuta.
Unaweza kuamua kuishi kwa maoni ya watu wengine.
Unaweza kuamua kufuata njia zilizotengenezwa tayari.
Unaweza kuendelea kuwa yule uliyetengenezwa uwe.
Lakini pia unaweza kusimama. Unaweza kuuliza. Unaweza kuvunja ukimya wa ndani. Unaweza kusema: Nataka kujua mimi ni nani kabla sijajaribu kuwa chochote.
Hilo ni jukumu lako. Siyo la jamii. Siyo la shule. Siyo la ajira. Ni lako.
Na siku unapoanza kuishi kwa utambuzi wa wewe halisi, kazi haitakuwa gereza. Mshahara hautakuwa kipimo cha thamani yako. Soko halitakuwa hakimu wa uwezo wako. Utatumia mfumo bila mfumo kukutumia.
Leo usiache swali hili likupite.
Usiishie kujiita jina lako.
Usiishie kujitambulisha kwa cheti chako.
Simama mbele ya maisha na uulize kwa uthabiti:
Mimi ni nani?
Kwa sababu ndani ya jibu hilo ndipo kuna uhuru wako. Ndipo kuna ukubwa wako. Ndipo kuna maisha yako halisi.
Ndimi Mbulwa King'ung'e - Founder King Mentorship Program.
Mawasiliano:0744284329
Comments
Post a Comment