Usitafute Mtu Sahihi — Jenga Nafsi Itakayemvutia Mtu Sahihi
Mahusiano ni uwekezaji wa maisha. Kama ilivyo katika uwekezaji mwingine wenye akili, mtu hawekezi bila kufanya tathmini ya kina.
Kabla ya kuwekeza pesa katika biashara au mradi wowote, huchunguza mazingira, uwezekano wa mafanikio, hatari zinazoweza kujitokeza, na faida inayoweza kupatikana baadaye.
Lakini jambo la kushangaza ni kwamba wengi hutumia umakini mkubwa wanapowekeza fedha zao, lakini hutumia umakini mdogo sana wanapochagua mtu wa kushirikiana naye maisha.
Hapo ndipo matatizo mengi ya mahusiano huanzia.
Mahusiano yanapoanza bila ufahamu wa kina, mara nyingi hugeuka kuwa chanzo cha maumivu ya kihisia, migogoro isiyoisha, na wakati mwingine kuvunjika kwa ndoto ambazo watu walizijenga kwa matumaini makubwa.
Ukweli ni kwamba mahusiano bora hayajengwi kwa bahati.
Huinuliwa kwa ufahamu, ukomavu wa fikra, na uwezo wa mtu kujitambua kabla ya kuanza kumtafuta mwingine.
Kabla hata hujakutana na mtu sahihi, kuna nguvu moja inayofanya kazi kimya kimya ndani yako—na nguvu hiyo ni fikra zako.
Fikra zako huamua aina ya watu unaovutiwa nao, huamua aina ya watu wanaovutiwa na wewe, na huunda aina ya mahusiano utakayojenga.
Katika ulimwengu wa maendeleo binafsi kuna kanuni maarufu sana inayojulikana kama Kanuni ya Uvutano.
Kanuni hii inasema kwamba katika maisha, mara nyingi huvutia si kile unachokitaka kwa maneno, bali huvutia zaidi kile unachofanana nacho kwa kiwango cha fikra, tabia, na mtazamo wa maisha.
Hii ina maana kwamba ubora wa mtu utakayevutia mara nyingi huwa ni kioo kinachoakisi ubora wako mwenyewe.
Hivyo, kosa kubwa ambalo wengi hufanya ni kutumia muda mwingi kuorodhesha sifa wanazotaka kwa mtu, bila kuangalia kwa uaminifu wa kiwango cha mvuto wao binafsi.
Mwanamke anaweza kusema anataka mwanaume mwenye maono, mwenye mafanikio, mwenye adabu, mwenye thamani na mwenye uwezo wa kuongoza familia.
Mwanaume anaweza kusema anataka mwanamke mwenye thamani, mwenye akili, mwenye maadili, na mwenye uwezo wa kujenga familia yenye utulivu.
Lakini pamoja na orodha hizi za matamanio, kuna swali moja muhimu sana ambalo wengi hulikwepa:
“Ni mtu wa aina gani ambaye mtu ninayemtaka huvutiwa naye?”
Swali hili linaweza kubadilisha kabisa mtazamo wako kuhusu mahusiano.
Mwanamke anayetamani mwanaume mwenye maono makubwa anapaswa kuelewa kwamba wanaume wa aina hiyo huvutiwa na wanawake wenye mwelekeo wa maisha.
Mwanamke mwenye akili na upeo wa kufikiri huwavutia wanaume wenye maono, kwani mazungumzo yao yana kina na maisha yao yanaanza kujengwa juu ya msingi wa kuthaminiana kiakili.
Hii kanuni haimuhusu mwanamke pekee; inamhusu pia mwanaume.
Wanaume wengi hutamani kupata mwanamke bora, lakini wanawake wengi huvutiwa na mwanaume mwenye mwelekeo wa maisha, nidhamu binafsi, na uwezo wa kusimamia maisha yake kwa uthabiti.
Wanaume wanaojijenga kiakili na kimtazamo huwa na mvuto mkubwa zaidi kwa wanawake wenye ubora wa hali ya juu.
Kadiri mtu anavyojijenga kiakili, kitabia na kimtazamo, ndivyo anavyoongeza uwezekano wa kuvutia watu wenye ubora unaofanana na huo.
Kwa hiyo, kama unataka kuvutia mtu sahihi katika maisha yako, usianze kwa kumtafuta kwa haraka. Anza kwa kujijenga.
Jenga akili yako kwa maarifa.
Jenga tabia zako kwa nidhamu.
Jenga maisha yako kwa maono na mwelekeo unaoeleweka.
Kadiri unavyokua toleo bora zaidi la nafsi yako, ndivyo unavyoongeza uwezekano wa kukutana na mtu ambaye pia ameamua kujijenga kwa kiwango hicho.
Hii ndiyo kanuni isiyoonekana, lakini yenye nguvu Kubwa: watu hawavutii kile wanachokitaka kwa maneno pekee; huvutia kile wanachokuwa katika uhalisia wa maisha yao.
Na pale unapofikia hatua ya kuwa mtu sahihi, uwezekano wa kukutana na mtu sahihi huongezeka kwa kiwango kikubwa.
Hapo ndipo safari ya mahusiano yenye afya, thamani, na mafanikio ya pamoja huanza.
Ndimi Mbulwa King'ung'e
Founder, King Mentorship Program
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment