USUKANI WA MAISHA: Kutoka Lawama za Kiroho hadi Mapinduzi ya Uwajibikaji...
Kuna dhana ambayo imejengeka kwa nguvu katika jamii nyingi inayoitwa mapito ya maisha.
Kwa muda mrefu, dhana hii imefungwa moja kwa moja na Mungu kana kwamba kila ugumu, kila maumivu, kila kushindwa ni maandishi ya moja kwa moja yaliyokwisha kupangwa.
Lakini kuna swali la msingi ambalo halijawahi kuulizwa kwa uzito unaostahili: kama ulipewa akili, ulipewa utashi, ulipewa hiari ya kuishi isipokuwa tu uwe sahihi — bado unaongozwa au umepewa mamlaka?
Shida si kuongozwa. Shida ni kuambiwa unaongozwa huku ukiendelea kupambana kumuomba huyo anayesemekana anakuongoza akuokoe katika magumu.
Kama ndiye anayekuongoza, kwa nini akupeleke kwenye maumivu halafu akuache umuombe akutoe humo? Hapa ndipo mkanganyiko wa kiakili unapoanzia.
Kwa muda mrefu, MTU amekuwa akihamisha uwajibikaji wa maisha yake kwa nguvu za nje. Ugumu ukitokea, anasema ni mapito. Akiumia, anasema ameandikiwa. Akikosea, anatafuta chanzo nje yake.
Lakini hapohapo, huyo huyo ataomba mabadiliko. Ataomba afanikiwe. Ataomba apendwe. Ataomba apate ndoa bora. Ataomba atoke kwenye maumivu aliyodai yaliandikwa kwa ajili yake.
Kama kila kitu kimeandikwa, kwa nini ukiombee mabadiliko? Na kama kinaweza kubadilika, kiliandikwa vipi?
Zaidi ya hapo, kumekuwa na hoja ya kuhusisha maovu na kiumbe kingine — kwamba kuna nguvu inayomsukuma mtu kufanya makosa.
Lakini je, msukumo una nguvu kuliko uamuzi? Ni nani aliyesema “ndiyo” kabla ya tendo kufanyika? Ni nani aliyekubali?
Ukweli mgumu ni huu: MTU anapenda uhuru wa kuchagua, lakini hapendi uzito wa kuwajibika.
Hivyo basi, Mungu na shetani wamekuwa vibao vya kutupia lawama za kile ambacho kimsingi ni matokeo ya maamuzi ya MTU.
Kibaya zaidi, hakuna anayekaa chini na kujiuliza: kati ya hao wawili, nani anaendesha maisha yangu kwa vitendo?
Kama kweli unaongozwa kila hatua, kwa nini unahubiriwa ujirekebishe? Kama kuna dereva wa maisha yako, kwa nini unawajibishwa kwa maamuzi Yako?
Ukweli mmoja haukwepeki: si kila swali linahitaji kujibiwa kwa imani. Kuna maswali yanahitaji kufikiriwa kwa ujasiri.
Shuleni hukujibu hesabu kwa imani. Ulijifunza kanuni, ukafanya mazoezi, ukapata majibu. Lakini inapofika kwenye maswali ya uwepo, wengi hukimbilia mafumbo.
Si kwa sababu majibu hayapo, bali kwa sababu akili haijazoeshwa kuyatafuta bila woga.
Maisha yalikuwepo kabla ya mifumo ya dini, kabla ya taasisi za elimu, kabla ya tafsiri za kifalsafa. MTU alikuja baadaye kujaribu kuyaelewa baada ya kupoteza ukweli wa kuishi.
Hivyo basi, kuishi si suala la kuiga maandishi; ni suala la kuelewa mfumo na kuchukua nafasi yako ndani yake.
Hebu fikiria mtu anayesema: “Niliandikiwa kupita katika mateso haya.” Lakini hapohapo anachukua hatua, anapambana, anatafuta suluhisho.
Hilo peke yake linathibitisha jambo moja — ndani yake kuna imani kwamba ana uwezo wa kubadilisha hali.
Na kama ana uwezo wa kubadilisha hali, basi hakuwa mfungwa wa maandishi; alikuwa mmiliki wa chaguo.
Tatizo si imani. Tatizo ni utegemezi wa kufikiri.
Ndiyo maana katika King Mentorship Program, iliyoanzishwa na Mbulwa King’ung’e, hatubomoi imani za watu.
Tunajenga misingi ya uwajibikaji. Tunamuuliza mtu maswali magumu ambayo wengi wamekwepa kwa miaka.
Tunamwongoza kuchunguza anajua nini, anaamini nini, na kwa nini anaamini hivyo. Si kwa lengo la kumbadilisha, bali kwa lengo la kumkomaza.
Tunamjenga mtu kiakili — ili ajifunze kufikiri kwa kina.
Tunamjenga kimwili — ili aishi kwa nidhamu na uthabiti.
Tunamjenga kiroho — si kwa utegemezi, bali kwa ufahamu.
Tunasisitiza kwamba wewe ndiye dereva wa maisha yako. Kukosea si laana ya mambo ya Mungu; ni sehemu ya kujifunza.
Maumivu si hukumu ya kiungu; mara nyingi ni matokeo ya maamuzi, au matokeo ya kutojua. Na kutojua si kosa la milele — ni hatua inayoweza kurekebishwa kwa maarifa.
Jamii iliyokomaa si ile inayotafuta wa kulaumiwa. Ni ile inayotafuta wa kuwajibika.
Tunataka kuunda kizazi kitakachojua kwamba kuishi si kusubiri kuongozwa, bali ni kuelewa na kuongoza.
Kizazi kitakachotambua kwamba mema tunayoyataka yanahitaji uwazi wa fikra, si visingizio vya kiimani.
Kaa chini ujiulize: je, maisha unayoishi sasa ni script isiyobadilika, au ni matokeo ya maamuzi yako yaliyokusanywa kwa muda?
Unapolaani ugumu wa maisha, je, unakosoa mfumo au unakwepa uwajibikaji wako ndani ya mfumo huo?
Ulipewa akili kwa sababu. Si kwa ajili ya kuitunza kwenye hifadhi ya hofu. Bali kwa ajili ya kuitumia, kuhoji, kuchambua, na kujenga.
Mwisho wa yote, safari ya ukomavu huanza pale unapokubali ukweli mmoja mgumu: hakuna anayekaa kwenye usukani wa maisha yako isipokuwa wewe.
Na siku utakapotambua hilo kwa kina, ndipo mapito yatakapogeuka kuwa maamuzi — na maamuzi kuwa mwelekeo.
Hiyo ndiyo falsafa tunayoisimamia. Hiyo ndiyo misingi ya King Mentorship Program.
Na hapo ndipo jamii ya kiutu yenye uelewa wa kweli huanzia.
Ndimi; Mbulwa King'ung'e, Founder King Mentorship Program.
Mawasiliano:0744284329
Comments
Post a Comment