“Utakasirika… Lakini Maisha Unayoishi Ndicho Ulicholipia...”


Kuna ukweli mmoja ambao watu wengi wanaukwepa kimya kimya, si kwa sababu hawaujui… bali kwa sababu wanajua wakikaa nao, utawalazimisha kubadilika. 

Ukweli huo ni huu—maisha hayana huruma na mtu anayekwepa gharama. 

Unaweza kuomba, unaweza kutamani, unaweza hata kujifariji kwa maneno mazuri kila siku, lakini mwisho wa siku, maisha yatakupa kile ulicholipia, si kile ulichotamani. 

Hapo ndipo watu wengi wanapochanganyikiwa, kwa sababu wanajiona wanastahili mengi, lakini hawajiulizi wamewekeza nini ili kustahili hayo wanayotamani.

Tunaishi kwenye dunia ambayo kila mtu anataka matokeo mazuri, lakini wachache wako tayari kupitia mchakato unaozalisha matokeo hayo. 

Watu wanataka pesa, lakini hawataki nidhamu ya pesa. Wanataka mahusiano bora, lakini hawataki kujibadilisha ili wawe watu bora wa kuingia kwenye mahusiano hayo. 

Wanataka kuthaminiwa, lakini hawajajenga tabia zinazozalisha thamani. 

Na ukweli ni huu, huwezi kuwa na maisha ya kiwango fulani kama hujawa mtu wa kiwango hicho. 

Maisha hayadanganyiki. Hayashawishiki na maneno yako. Yanajibu kwa kile unachofanya, si kile unachosema.

Kitu ambacho watu wengi hawatakubali ni kwamba hakuna kitu cha maana kinachokuja bure. 

Kama si fedha, basi ni muda. Kama si muda, basi ni nguvu. Kama si nguvu, basi ni maumivu ya kujinyima na kukua. 

Na kama utaamua kukwepa gharama hizi leo, basi ujue unaingia kwenye deni la maisha ambalo utalilipa kesho kwa riba kubwa zaidi. 

Utakwepa kujifunza leo, kesho utalipa gharama ya ujinga. Utakwepa nidhamu leo, kesho utalipa kwa majuto. Utakwepa kujibadilisha leo, kesho maisha yatakulazimisha ubadilike kwa maumivu ambayo usingeyahitaji kama ungeanza mapema.

Watu wengi wanapenda vitu vya bure bila kuelewa kuwa “bure” mara nyingi ndiyo ghali zaidi mwishowe. 

Wanataka ushauri wa bure, wanataka mentorship ya bure, wanataka mtu awaonyeshe njia bila wao kujitoa. 

Lakini hawajiulizi, ni nani alilipa gharama ili hayo maarifa yawepo? Ni nani alipoteza muda wake, nguvu zake, na sehemu ya maisha yake ili wewe upate hiyo “bure” unayoitafuta? 

Ukweli ni kwamba hakuna mtu makini atakayewekeza kwako kwa kina bila kuona thamani yako katika mchakato huo. 

Na kama wewe mwenyewe hujaamua kujitolea kwa maisha yako, ni kwa nini mtu mwingine afanye hivyo kwa ajili yako?

Nimewahi kuwa upande huo. Nilikuwa naona kila anayetoa huduma anataka hela yangu. 

Nilijiona mjanja kwa kujifunza mwenyewe, kusoma hapa na pale, kusikiliza hiki na kile. Lakini miaka ilivyoenda, nilianza kuona kuna kitu hakiko sawa.

Nilikua najua vitu, lakini maisha yangu hayakuwa yanabadilika kwa kiwango kinachoendana na maarifa hayo. 

Hapo ndipo nilipoanza kujiuliza kama kweli tatizo langu ni kukosa taarifa… au kukosa mwongozo sahihi wa kunipeleka hatua inayofuata. 

Na hapo ndipo nilipobadilisha mchezo. Nikaanza kulipa gharama ambazo hapo awali nilikuwa nakimbia—gharama ya muda wangu, gharama ya kujinyima, gharama ya kukubali kusahihishwa, na ndiyo, hata gharama ya fedha.

Ndipo nikaanza kuona tofauti ambayo si ya kubahatisha. Nilianza kupunguza miaka ya kupotea. Nilianza kupata mwelekeo. Nilianza kuona vitu kwa uwazi ambao sikuwa nao kabla. 

Nikagundua kitu ambacho wengi hawakijui au wanakipuuza—mtu sahihi anaweza kubadilisha mwelekeo wa maisha yako ndani ya muda mfupi sana, lakini wewe unaweza kutumia miaka mingi ukizunguka sehemu ile ile ukidhani unaendelea mbele. 

Hapo ndipo nilielewa kuwa kulipa gharama si kupoteza, ni kubadilishana nishati.

Unatoa kitu chenye thamani ili upokee kitu chenye thamani kubwa zaidi—na hapo ndipo milango inaanza kufunguka.

Na bado, watu wengi watasoma haya na wataendelea vilevile. Si kwa sababu hawajaelewa, bali kwa sababu hawako tayari kubadilika. 

Ukweli mchungu ni huu—huwezi kuvuta maisha ambayo hujastahili kuwa nayo. Maisha yanakupa kile unachoweza kubeba, si kile unachotamani. 

Na kama hujalipa gharama ya kuwa mtu wa kiwango fulani, hata ukikipata hicho kiwango, hakitadumu mikononi mwako. 

VNdiyo maana unaona watu wanapata vitu halafu wanavirudisha chini bila kuelewa kwa nini. Hawakuwa tayari kuvimiliki.

Kwa hiyo mwisho wa siku, chaguo ni rahisi sana, hata kama si rahisi kulitekeleza. 

Unaweza kuchagua kulipa gharama ya mabadiliko kwa makusudi leo, au ukasubiri kulipa gharama ya majuto kesho. 

Hakuna njia ya katikati. Hakuna shortcut ya kweli. Na hakuna mtu atakayekuja kukuokoa kama wewe mwenyewe hujaamua kuchukua hatua. 

Lakini kama utaamua, kama utaacha kujidanganya, kama utaacha kukimbia kile unachojua kabisa unapaswa kufanya—basi hapo ndipo mambo yanabadilika.

Kwa sababu maisha hubadilika pale mtu anapoacha kutafuta njia rahisi… na kuanza kulipa gharama ya kuwa mtu anayestahili maisha anayoyataka.

Nitumie ujumbe neno GHARAMA Kwenda 0744284329 nikuonyeshe hatua inayofuata...

Ndimi Mbulwa King'ung'e Founder King Mentorship Program.

Mawasiliano: 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...