“Wewe Ni Nani? Mapinduzi ya Utambuzi Binafsi..."



Najua hakuna mtu aliyewahi kukuambia wewe ni nani. Labda ndiyo maana unajidharau, labda ndiyo maana unajiona hutoshi, labda ndiyo maana unajidunisha. 

Lakini jiulize: kwa nini unaishi kwa kuzingatia zaidi sauti za wengine kuliko sauti yako mwenyewe? 

Kwa nini unamzingatia rafiki kuliko nafsi yako?

Kwa nini unalipa uzito pendekezo la mwalimu, mchungaji, au mfanyakazi mwenzako kuliko msukumo wa ndani unaokujua zaidi? 

Kwa nini uzingatie maoni ya watu wasiojua hatima yako, ilhali wewe ndiye umebeba hatima ya maisha yako? 

Sisi Watu tunahitajiana, tunapaswa kusaidiana kwa mema, lakini msaada haupaswi kuwa minyororo na ushauri haupaswi kuwa kifungo. 

Swali si kama wewe ni mwema au mzuri; swali ni: unafanya nini kwa wengine na zaidi ya hapo, unafanya nini kwa nafsi yako? 

Mchango wako katika jamii umetosha, au bado una wajibu ambao hujauvaa kwa ujasiri? 

Kama unajua una wajibu wa kubadilisha jamii, kwa nini umeiruhusu jamii ikuamulie thamani yako? Kama jamii ni sababu ya wewe kudumaa, kwa nini bado unaipa mamlaka juu ya akili yako?

Sote tunazaliwa tukiwa huru, bila hofu, bila mashaka, bila mipaka, lakini dunia ikaanza kukuambia wewe ni nani na hatua kwa hatua ukaanza kuamini sauti za nje kuliko sauti yako ya ndani.

Ukawa unajiona kwa vioo vya watu wengine, ukiwa unapima thamani yako kwa mizani isiyokuwa yako, na hapo ndipo ulipoanza kupotea. 

Jamii si adui, lakini ina mifumo inayounda watu wanaofanana, si watu wanaojitambua. 

Tangu utotoni umefundishwa nini cha kuamini, nini cha kuogopa, nini cha kuchagua, na nini cha kuepuka, lakini hujawahi kufundishwa swali moja muhimu: wewe ni nani bila kelele za dunia? 

Mtu asipojitambua, hugeuzwa kuwa mtumwa wa fikra alizopewa; atapewa cheo lakini atakosa maamuzi, atalipwa mshahara lakini atakosa amani ya kuutumia, atapewa kazi lakini hataifurahia, kwa sababu anaishi kwa kuigiza, si kwa kujua.

Hakuna somo gumu kama kujitambua na hakuna somo muhimu kama utambuzi binafsi. 

Utambuzi binafsi si kujua jina lako, ni kujua misingi ya maamuzi yako, kujua kwa nini unaogopa, kujua kwa nini unachelewa kuchukua hatua, na kujua kwa nini unahitaji kuthibitishwa na wengine. 

Wengi hushindwa kwa sababu wanataka mafanikio bila kujijua, wanataka uhuru bila kuachana na utegemezi wa sauti za nje, wanataka kuthaminiwa bila kujithamini. 

Lakini ukweli unabaki: maisha ya mtu hubadilika pale anapoanza kujisikiliza kwa dhati. Kama mtu hawezi kujiamulia maisha yake, ataishi kama kioo kinachonyamaza, akirudia maoni ya wengine, akiruhusu hofu na hila kuunda hatima yake.

Kila kitu unachofanya kikiwa chini ya udhibiti wa wengine ni kazi ya mtu mwingine, si yako.

Swali si kama wewe ni mzuri, bali ni: je unafanya nini kwa ulimwengu huu na kwa nafsi yako? 

Je unachagua kuishi kwa nguvu yako, au unaendelea kuishi kwa maelekezo ya wengine? Hii si vita dhidi ya jamii, bali vita dhidi ya kutojitambua. 

Kuanzia leo, anza kujisikiliza. Wapuuze wanaokujaza hofu, wapuuze wanaokudharau, wapuuze wanaofikiri huwezi kuishi bila wao.

Jiweke kimawazo katika ulimwengu usio na kelele za hukumu. Sikiliza sauti ya ndani. Jione. Tambua uwezo wako. 

Sote tunazaliwa na vipaji na uwezo, lakini wachache wanachagua kuviendeleza; wengine wanavizika kwa hofu. 

Wakati unapoanza kujitambua, unapata ujasiri wa kuvunja vizuizi, kupata uhuru, na kuunda maisha yako kwa uwezo wa dhati uliopewa.

Mwisho wa yote, ni wewe kuamua: uishi maisha yako au uendelee kuishi maisha yaliyoandikwa na mfumo. 

Katika King Mentorship Program, tunafundisha Utambuzi Binafsi si kwa lengo la kumtoa mtu kwenye mfumo, bali kumpa mtu machaguo mengi ya kuishi. 

Mtu atambue kuwa asingekuwa yule aliyeundwa na mazingira, angekuwa nani? Angechagua nini? Angeishi vipi? Hili si jambo dogo; hili ni jambo la hatima. 

Uamuzi wako unaunda hatima yako, na kila hatua ya kujisikiliza ni hatua ya uhuru. 

Uamuzi ni wako, maisha yako ni yako, na leo ni siku ya kuanza kuishi kwa nguvu yako kamili.

Ndimi Mbulwa King'ung'e, Founder wa King Mentorship Program. 

Mawasiliano:0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...