ADUI MKUBWA WA MAISHA YAKO SI TUKIO — BALI TAFSIRI YA FIKRA ZAKO MWENYEWEMaisha hayashindwi na tukio — bali na maana tunayochagua kulipa.
Adui mkubwa wa mtu si hali, si tukio, wala si mtu mwingine. Adui mkubwa wa mtu ni fikra zake mwenyewe.
Kuna tofauti kubwa sana kati ya wewe na tukio. Tukio ni jambo linalotokea katika maisha, lakini wewe ni mtu mwenye uwezo wa kuchagua maana ya tukio hilo.
Tatizo kubwa la watu wengi si tukio linalowapata, bali ni namna wanavyojipachika ndani ya tukio hilo na kujipa maana isiyowajenga.
Watu wengi hujikuta wakiumizwa si kwa sababu ya tukio lenyewe, bali kwa sababu ya tafsiri wanayoipa hali wanayokutana nayo.
Miaka michache iliyopita kulikuwa na vijana wawili waliokuwa wanafanya biashara ndogo ya kuuza nguo.
Walikuwa wakijitahidi kujenga maisha yao kwa juhudi kubwa sana. Siku moja walipata hasara kubwa isiyotarajiwa.
Mzigo wao uliungua moto ghafla usiku mmoja, na ndani ya muda mfupi wakapoteza kila kitu walichokuwa wamewekeza.
Hakukuwa na bima, hakukuwa na msaada wa haraka, na walibaki na deni pamoja na maumivu makubwa ya kupoteza walichokuwa wamejenga kwa muda mrefu.
Lakini kilichofuata baada ya tukio hilo ndicho kilichobadilisha maisha yao. Kijana wa kwanza alipoona hasara ile, alisema moyoni mwake kuwa maisha yamemchoka na dunia imemwonea.
Alijiona hana uwezo tena wa kusimama wala kuanza upya. Akaanza kuamini kwamba tukio lile lilikuwa mwisho wa ndoto zake.
Alikaa nyumbani kwa muda mrefu, akakata tamaa, akapoteza hamasa ya kufanya kazi, na polepole akaanza kuamini kuwa yeye si mtu wa mafanikio tena.
Lakini kijana wa pili alichagua tafsiri tofauti kabisa. Alijiambia, “Moto umeunguza mzigo wangu, lakini haujaunguza uwezo wangu.”
Ingawa alikuwa na maumivu na huzuni kama mwenzake, hakuruhusu tukio lile litafsiri utambulisho wake.
Alianza tena kwa hatua ndogo sana, akitumia mtaji mdogo alioupata kwa shida. Aliendelea kusonga mbele kwa uvumilivu na kujifunza kutokana na makosa yaliyotokea.
Miaka michache baadaye, kijana huyu alikuwa ameweza kujijenga upya na hata kuajiri watu kadhaa katika biashara yake, wakati yule wa kwanza bado alikuwa analalamika juu ya tukio lile lile lililotokea zamani.
Tukio lilikuwa moja, lakini tafsiri ilikuwa tofauti, na tafsiri ndiyo iliyoamua maisha yao.
Hili ndilo somo kubwa sana ambalo watu wengi wanapaswa kulielewa. Mahusiano ni tukio lililopo katika maisha ya binadamu.
Lakini mtu akisema kwamba anachukia mahusiano na kwamba hayana maana, haina maana kuwa mahusiano hayana maana, bali inaonyesha fikra zake kuhusu mahusiano ndizo zimetoa tafsiri hiyo.
Maisha yenyewe ni tukio lililopo kwa kila mtu. Lakini mtu akisema maisha hayana maana, haina maana kuwa maisha hayana maana, bali ina maana kuwa ameamua kutokuyapa maana katika mtazamo wake mwenyewe.
Kwa hiyo, wakati mwingine ni muhimu sana kujifunza kujitofautisha wewe na tukio.
Tukio ni jambo lililopo, lakini mtazamo wako kuhusu tukio hilo ndiyo huamua maisha yako yatakuwaje. Huwezi kudhibiti kila kitu kinachotokea duniani.
Moja ya busara kubwa maishani ni kutambua ni mambo gani unaweza kudhibiti na ni mambo gani huwezi kudhibiti.
Huwezi kudhibiti fikra za watu wengine kuhusu wewe, huwezi kudhibiti tabia zao, huwezi kudhibiti mifumo ya serikali, wala huwezi kudhibiti imani za watu wengine.
Kujaribu kudhibiti vitu hivyo ni kujichosha bure na kupoteza nguvu zako pasipo sababu.
Lakini kuna mambo muhimu sana ambayo unaweza kuyadhibiti. Unaweza kudhibiti mawazo yako, unaweza kudhibiti mtazamo wako, unaweza kudhibiti maamuzi yako, pamoja na maono na matarajio yako ya maisha.
Hapa ndipo nguvu yako ya kweli ilipo. Hapa ndipo unapopata uwezo wa kubadilisha maisha yako hata kama mazingira yako ni magumu.
Umaskini ni tukio, ni hali inayoweza kumpata mtu yeyote katika maisha. Lakini si lazima uwe utambulisho wako wa maisha yote.
Mama lishe anaweza kukosa mtaji leo, lakini akaamua kupambana na kujenga kesho yake.
Dereva bodaboda anaweza kuanza na pikipiki ya kukodi, lakini akaamua kuweka akiba kidogo kidogo hadi siku moja akawa mmiliki wa pikipiki yake mwenyewe.
Kwa maana hiyo, kupitia hali ya umaskini, unaweza kuchagua wewe ni nani. Unaweza kuchagua kusema kuwa wewe ni maskini na hutabadilika, au unaweza kusema kuwa hiyo ni hali tu ya muda na si mwisho wa safari yako.
Watu wengi hawafahamiki wao ni nani mpaka wanapokutana na tatizo.
Tatizo lina uwezo wa kukuuliza swali moja muhimu sana, nalo ni: “Wewe ni nani kweli?”
Jibu la swali hilo halitoki kwenye maneno matupu, bali linatoka kwenye matendo yako.
Jambo moja ulilochagua kukabiliana nalo ndilo linaanza kukutambulisha wewe ni nani katika maisha.
Ninaitwa Mbulwa King'ung'e, Founder wa King Mentorship Program.
Sikuzaliwa nikiwa mwalimu, wala sikuzaliwa nikiwa mentor au mwandishi. Nilijijenga hatua kwa hatua.
Nilipokutana na tatizo la ujinga katika jamii, nisingeweza kulikwepa wala kulikimbia.
Nilichagua kulikabili kwa nguvu zote nilizokuwa nazo. Leo ninatambulika kama mwalimu, mentor, mwandishi na consultant, si kwa sababu sikukutana na matatizo, bali kwa sababu nilibadilisha mtazamo wangu kuhusu matatizo niliyokutana nayo.
Watu wengi wanapoona kikwazo mbele yao, wanaona mwisho wa safari yao. Lakini ukweli ni huu: kikwazo si mwisho, bali ni njia mpya ya kutokea.
Ukiona njia moja imefungwa, badilisha mbinu. Ukiona mlango umefungwa, tafuta mlango mwingine.
Usibadilishe ndoto zako kwa sababu ya kikwazo, badilisha mbinu zako ili ndoto zako ziendelee kuishi.
Unapokutana na tatizo leo, jiulize swali moja muhimu sana: je, ninajipachika ndani ya tatizo na kujipa maana ya kushindwa, au ninajitofautisha na tatizo ili nilishinde?
Kwa sababu siku moja maisha yatakuuliza wewe ni nani. Na jibu lako halitatokana na tukio ulilokutana nalo, bali mtazamo uliouchagua mbele ya tukio hilo.
Ninaitwa Mbulwa King'ung'e
Founder — King Mentorship Program
Mawasiliano:0744284329
Comments
Post a Comment