Maumivu Yako Hayatoki Kwenye Dunia — Yanatoka Kwenye Matarajio Yako


Watu wengi wamevunjika moyo si kwa sababu maisha ni mabaya… bali kwa sababu matarajio yao yalitangulia mbele ya maandalizi yao.

Kuna siku mtu mmoja aliniambia maneno ambayo sitayasahau kirahisi. Aliniambia kwa sauti ya uchovu na huzuni, “Nilitarajia maisha yangu yatabadilika mwaka huu… nilipanga mengi sana. Nilijitahidi. Lakini leo sina hata mia mfukoni.” 

Nilimtazama kwa makini, nikagundua hakuwa tu amechoka kimwili—alikuwa amevunjika moyo kabisa.

Alikuwa amejaribu biashara mara kadhaa bila mafanikio. Alikuwa ameomba msaada kwa watu wake wa karibu lakini hakupata kile alichotarajia. 

Alikuwa ameomba kwa Mungu kila siku, lakini hali yake haikubadilika haraka kama alivyotarajia. 

Taratibu alianza kuamini kuwa labda dunia imeamua kuwa kinyume naye. Lakini kadri nilivyomsikiliza, niligundua jambo moja kubwa—maumivu yake mengi hayakutokana na dunia kuwa mbaya, bali kutokana na matarajio yake kukimbia mbele ya maandalizi yake.

Ukweli mchungu ambao watu wengi hawataki kuusikia ni huu: miongoni mwa sababu kubwa zinazochangia maumivu yetu ni matarajio yetu kwenda kinyume na hali halisi ya maisha.

Tunatarajia mambo mengi, mazuri, makubwa, ya haraka—lakini maisha hayatembei kwa kasi ya matarajio yetu. Na pale mambo yanapokwenda tofauti na tulivyopanga, tunaanza kuumia moyoni.

Tunatarajia wenzi wetu watupende kwa kiwango fulani. Tunatarajia watu watambue thamani yetu, watupongeze, watuone kuwa wa kipekee. 

Lakini pale wanaposhindwa kufanya hivyo, tunahisi hatuna maana. Tunaanza kujiona kama watu wasio na thamani. 

Tunajiuliza maswali mengi moyoni—kwa nini hawajali, kwa nini hawatambui juhudi zetu, kwa nini hawatuoneshi upendo tulioutarajia? Na polepole, maumivu yanaanza kuota mizizi ndani ya moyo wetu.

Kwa mtu aliyewahi kupenda na kuumizwa, anajua vizuri sana kuwa hakuna ridhisho kubwa kama lile linalotoka kwa mtu unayempenda. 

Na pale unapotarajia kupendwa lakini ukapata ukimya, au kupuuzwa, moyo huumia sana. Unaweza kuendelea kuishi, lakini ndani yako unahisi kuna kitu kimevunjika. 

Hapo ndipo wengi huanza kuhisi maisha hayana maana tena, si kwa sababu dunia imebadilika, bali kwa sababu matarajio yao hayakukutana na uhalisia.

Lakini si kwenye mapenzi tu ambapo matarajio hutuumiza. Wengi wetu pia tumeweka matarajio makubwa sana kwa Mungu tukasahau wajibu wetu binafsi. 

Tunaamini kila kitu kitafanywa na Mungu bila sisi kufanya sehemu yetu. Tunaomba sana, tunasali kila siku, tunaweka matumaini makubwa kwamba hali itabadilika ghafla. 

Lakini tunapokutana na magumu yanayoendelea kwa muda mrefu, tunaanza kukata tamaa. Tunaanza kujiuliza kama Mungu yupo kweli, au kama ametuacha peke yetu.

Kumbe ukweli ni kwamba Mungu hakutuumba bila uwezo. Alitupa akili, nguvu, na uwezo wa kutenda. 

Aliumba dunia ikiwa na neema na fursa nyingi, lakini akatuachia jukumu la kuzitafuta na kuzitumia. 

Tunapotarajia matokeo makubwa bila kuandaa uwezo wa kuyafikia, tunajiweka kwenye nafasi ya kuumia. Na pale tunapoumizwa, tunaanza kulaumu—tunalaumu hali, tunalaumu watu, tunalaumu hata Mungu.

Fedha pia ni chanzo kikubwa cha maumivu katika maisha ya watu wengi. Tunapanga mengi kwa matumaini ya kuwa na maisha bora. 

Tunafanya kazi, tunaanza biashara, tunajaribu njia mbalimbali za kuongeza kipato. Lakini pale fedha inapokosekana au kuchelewa kupatikana, moyo huanza kuumia. 

Kuna watu wanaamka kila siku wakiwa na matumaini mapya, lakini jioni wanarudi nyumbani wakiwa na huzuni ile ile. 

Wengine wamejaribu kuuza bidhaa nyingi lakini wateja hawaji kama walivyotarajia. Unataka kuuza bidhaa mia, lakini unapata mteja mmoja tu—na hapo ndipo maumivu huanza kujitokeza wazi.

Wakati mwingine tunajifariji kwa kusema kuwa fedha haiwezi kununua furaha. Usemi huu una ukweli wake, lakini pia una upande mwingine. 

Fedha inaweza kukupa mazingira ya kuishi kwa utulivu, inaweza kupunguza msongo wa mawazo, na inaweza kukupa nafasi ya kufurahia maisha kwa uhuru zaidi.

Ndiyo maana kukosa fedha mara nyingi huleta maumivu makubwa moyoni, si kwa sababu mtu anapenda mali kupita kiasi, bali kwa sababu anahitaji utulivu wa maisha.

Halafu kuna eneo lingine ambalo huumiza sana—eneo la malengo. Watu wengi huandika malengo yao kwa matumaini makubwa. 

Wanaota ndoto kubwa, wanaweka mipango mizuri, wanajiona wakifika mbali. Lakini pale wanapoanza safari na kuona matokeo hayaji haraka kama walivyotarajia, wanachoka. 

Unataka kuuza sana lakini hakuna wateja. Unataka kufanikiwa lakini kila hatua unayopiga inaonekana kurudi nyuma. 

Unaanza kukosa usingizi. Unaanza kukata tamaa. Matumaini yako yanaanza kuyeyuka taratibu kama barafu kwenye jua kali.

Katika hali hiyo, ni rahisi sana kuhisi kama dunia imekutenga. Ni rahisi kuhisi kama marafiki hawajali, ndugu hawajali, na hata Mungu amekuacha peke yako. 

Lakini ukweli ni huu: dunia haijakutenga. Marafiki hawajakutenga. Na si kwamba mafanikio hayakutaki. 

Mara nyingi kinachotokea ni kwamba matarajio yako yamekimbia mbele zaidi kuliko maandalizi yako ya sasa.

Hapa ndipo ninapopenda kusema jambo ambalo linaweza kubadilisha maisha yako ukilielewa vizuri: maumivu mengi tunayopitia hayaji kwa sababu dunia ni mbaya, bali kwa sababu matarajio yetu yamekimbia mbele ya uwezo wetu wa sasa. 

Tunataka kufika mbali haraka, lakini hatujajiandaa vya kutosha kufika huko. Tunataka matokeo makubwa, lakini bado hatujajenga msingi imara wa kuyabeba.

Leo sipo hapa kukutia hamasa ya muda mfupi. Sipo hapa kukuambia maneno matamu ya kukufanya ujisikie vizuri kwa dakika chache halafu kesho urudi kwenye maumivu yale yale. 

Nipo hapa kukuambia ukweli ambao unaweza kukuumiza kidogo, lakini ukakuponya kwa muda mrefu. 

Jitengeneze hadi uwezo wako ufanane na matarajio yako. Jijenge hadi uwe na nguvu ya kubeba kile unachokitaka.

Ndiyo maana huwa nafundisha kuhusu utambuzi binafsi. Kwa sababu mtu anapojielewa vizuri, anajua uwezo wake wa sasa uko wapi, na anajua hatua gani anahitaji kuchukua ili kufikia kile anachokitaka. 

Anajua kwamba mafanikio si jambo la bahati pekee, bali ni matokeo ya maandalizi ya muda mrefu.

Na kama wewe ni mmoja wa watu waliovunjika moyo leo, ninataka ujue jambo hili: kuvunjika moyo si mwisho wa safari yako. 

Labda matarajio yako yalitangulia mbele zaidi kuliko maandalizi yako ya sasa, lakini hiyo haimaanishi kuwa huwezi kufika unapotaka kufika. 

Inamaanisha tu kuwa kuna kazi ya kufanya, kuna uwezo wa kujenga, na kuna safari ya kuendelea.

Usikate tamaa kwa sababu mambo hayajaenda kama ulivyotarajia. Usijione umeshindwa kwa sababu matokeo yamechelewa. 

Badala yake, jenga uwezo wako. Jifunze. Endelea kupambana. Kwa sababu siku matarajio yako yatakapolingana na uwezo wako, maumivu yatapungua… na tumaini litarudi tena moyoni mwako.

Na siku hiyo itakapofika, utaelewa kwamba haukuwa umeachwa na dunia—ulikuwa unaandaliwa kuwa mtu mwenye nguvu zaidi kuliko ulivyokuwa mwanzo.

Mbulwa King'ung'e
Founder, King Mentorship Program
📞 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...