Nilipitia Mahusiano 4 (2019–2024) Kabla Sijagundua Kwa Nini Mahusiano Mengi Yanavunjika...

Nilidhani mapenzi yanatosha kujenga mahusiano. Lakini baada ya kupitia mahusiano manne tofauti kuanzia 2019 hadi 2024, niligundua ukweli ambao watu wengi hawaufundishi — kwamba mahusiano hayaharibiki kwa kukosa mapenzi, bali kwa kukosa sababu za kuishi zinazofanana.

Kama uko kwenye mahusiano au unapanga kuingia kwenye ndoa, ujumbe huu unaweza kukuokoa na maumivu ambayo wengine tayari wanalia nayo.

Mara kadhaa nimesikika nikisema kwamba asilimia kubwa ya watu wanazungumza, lakini hawajui wanavyosema. 

Tuna wataalamu wengi, tuna wasomi wengi, tuna walimu wengi wa mahusiano, lakini bado kila siku tunasikia watu wakilia, ndoa zikivunjika, mahusiano yakiharibika, na wengine wakianza upya bila kuelewa walikosea wapi. 

Tatizo si kwamba watu hawafundishwi. Tatizo ni kwamba mara nyingi tunafundishwa namna ya kufurahia mapenzi, lakini hatufundishwi namna ya kujenga mahusiano. 

Tunafundishwa ladha, lakini si msingi. Tunafundishwa namna ya kuvutia, lakini si namna ya kudumu.

Kwa muda mrefu nimekuwa nikitazama haya kwa ukimya. Siyo ukimya wa kutokujua, bali ukimya wa kujaribu kuelewa. 

Nilianza kujiuliza swali moja ambalo wengi hawapendi kujiuliza: kwa nini ndoa za zamani zilidumu? Si kwamba watu wa zamani walikuwa wakamilifu. Hapana. Walikuwa na changamoto kama sisi. 

Lakini walikuwa na kitu ambacho sisi tunaanza kupoteza—walikuwa wanapima misingi kabla ya kuunganisha maisha yao. Walikuwa wanalinganisha maisha kabla ya kuunganisha mapenzi.

Naandika haya si kama mtu aliyesimama nje ya uwanja. Naandika kama mtu aliyewahi kuingia ndani ya uwanja, akaanguka, akaumia, na akaanza kujiuliza maswali mazito. 

Katika maisha yangu, nimewahi kuwa kwenye mahusiano manne tofauti. Mwaka 2019 niliingia kwenye mahusiano ambayo kwa nje yalionekana yana nafasi ya kufanikiwa, lakini mwisho wake haukuwa mzuri. It didn’t work out. 

Nilijaribu tena mwaka 2020 nikiwa na matumaini mapya, nikidhani labda safari hii mambo yatakuwa tofauti, lakini bado haikudumu. 

Mwaka 2022 nikajikuta tena kwenye mahusiano mengine, nikifikiri nimejifunza vya kutosha, lakini mwisho wake ulikuwa ule ule—kutengana. 

Na mwaka 2024 nikajaribu tena, lakini hapo ndipo nilipoanza kuacha kulaumu watu na kuanza kujiuliza swali gumu zaidi: je tatizo ni watu ninaokutana nao, au kuna kitu kikubwa zaidi ambacho sijakielewa kuhusu maisha na mahusiano?

Niliporudi nyuma kuangalia mahusiano haya manne, niligundua jambo moja ambalo lilinitikisa ndani kabisa: hatukukosa mapenzi. Mapenzi yalikuwepo. Hisia zilikuwepo. Lakini tulikosa kitu kikubwa zaidi — tulikosa kufanana kwa sababu za kuishi.

Hapo ndipo macho yangu yalifunguka. Nikaanza kuelewa kwamba mahusiano mengi hayaharibiki kwa sababu watu hawapendani, "bali kwa sababu hawajui sababu zao za kuishi.

Kila mtu hapa duniani ana sababu zake za kuishi. Siyo ajali kwamba ulizaliwa. Kuna jukumu, kuna wito, kuna mwelekeo ambao maisha yako yanapaswa kuufuata. 

Na kabla hujaungana na mtu mwingine, ni muhimu sana kujua sababu zako za kuishi, na pia kujua sababu za kuishi za yule unayetaka kuwa naye. 

Kadiri nilivyoendelea kuchunguza maisha yangu na ya wengine, niligundua kwamba sababu za kuishi mara nyingi zinahusiana sana na vitu vikubwa vitatu ambavyo wengi hawavizingatii.

Kwanza ni wito au jukumu la kuishi. Kila mtu ana kitu ambacho ameumbwa kukifanya hapa duniani. 

Wengine wameumbwa kufundisha, wengine kuongoza, wengine kujenga familia zenye misingi imara, wengine kuanzisha mifumo na kubadilisha maisha ya watu. 

Sasa fikiria mtu mwenye wito wa kujenga na kusaidia watu wengi akiungana na mtu ambaye hana kabisa mtazamo wa kuwajibika kwa wengine. 

Mapenzi yanaweza kuwepo, lakini maisha yatakuwa mapambano ya kila siku kwa sababu mwelekeo wa maisha hauendani.

Pili ni tabia za kimwili ambazo mtu huzaliwa nazo. Kuna watu ni wavumilivu kwa asili, wengine ni wakali kwa asili, wengine ni wapole, wengine ni wa haraka, wengine wanapenda kupanga kila kitu, wengine wanaishi kwa hisia zaidi. 

Tabia hizi zinaathiri sana namna mtu anavyoishi na anavyokabiliana na changamoto. Ukikutana na mtu ambaye tabia zake za msingi zinapingana kabisa na zako, mapenzi yanaweza kukuwepo, lakini amani haitakuwepo kwa urahisi.

Tatu ni season au majira ambayo mtu alizaliwa. Hili ni jambo ambalo wengi hulipuuza, lakini linaathiri sana nguvu za mtu, mtazamo wake, na namna anavyokabiliana na maisha. 

Kuna watu wana asili ya kuanza vitu, wengine wana asili ya kumaliza vitu, wengine wana nguvu ya kustahimili, wengine wana nguvu ya kubuni. 

Hivyo kama watu wawili hawako kwenye majira yanayofanana kiakili na kiutendaji, hata kama wanapendana, safari yao inaweza kuwa ngumu sana.

Nilipoanza kuelewa haya, ndipo nilipoanza kuona kwa nini ndoa nyingi za zamani zilidumu. 

Siyo kwa sababu kulikuwa hakuna matatizo, bali kwa sababu walikuwa wanachukua muda kupima maisha kabla ya kuunganisha maisha yao.

Walikuwa wanatazama familia, tabia, uwezo wa kustahimili maisha, na mwelekeo wa maisha kwa ujumla. Kwa lugha rahisi, walikuwa wanalinganisha sababu za kuishi kabla ya kuunganisha maisha yao.

Kama uko kwenye mahusiano leo, jiulize swali moja la msingi sana: je ninajua sababu zangu za kuishi, na je ninajua sababu za kuishi za yule niliye naye? Au tunaishi kwa hisia tu bila kuelewa tunakoenda? 

Na kama bado hujaingia kwenye ndoa, usikimbilie mapenzi kwa sababu mapenzi yapo kila mahali. Kuvutiwa kupo, hisia zipo, lakini msingi wa maisha ndiyo unaodumu.

Usikimbilie mtu kwa sababu anakufurahisha tu. Tafuta kwanza kuelewa wewe ni nani, umeumbwa kufanya nini, na maisha yako yanaelekea wapi. Ukijijua, utachagua vizuri. Na ukichagua vizuri, utaishi vizuri.

Msije mkafikiri Mungu aliwaumba ili mje mteseke kwenye mahusiano. Kuteseka mara nyingi si mpango wa Mungu, bali ni matokeo ya kukosa misingi. 

Mahusiano hayaharibiki kwa sababu mapenzi hayapo. Mahusiano yanaharibika kwa sababu msingi haukujengwa. Na msingi mkubwa wa mahusiano si mapenzi—ni sababu za kuishi zinazofanana.

Hujaingia kwenye ndoa? Tafuta sababu zako za kuishi. Uko kwenye mahusiano? Hakiki kama sababu zenu za kuishi zinafanana. Kwa sababu bila msingi, jengo haliwezi kusimama.

Ninaitwa Mbulwa King'ung'e. Siyo mshauri wa mahusiano. Mimi ni mwalimu wa maisha na mwalimu wa mambo ya Mungu, na pia ni founder wa King Mentorship Program

Kama unahisi ujumbe huu umefungua macho yako au umekugusa mahali fulani moyoni, basi usiuweke kimya—ushirikishe na mtu mwingine ambaye anaweza kuhitaji kusikia ukweli huu kabla hajafanya kosa ambalo wengine tayari wanalia nalo.

Mawasiliano: 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...