UKIVUA MFUMO, UTABAKI NA NANI? Safari ya Kujitambua Katika Dunia Inayofundisha Kufanya Kazi Kuliko Kuishi...
Kuna muda huwa nawaambia wanafunzi wangu kitu kimoja cha msingi kabisa katika safari ya kujitambua: Vua kila kitu ulichovikwa kabla hujajaribu kujiona wewe ni nani.
Vua kile ambacho mfumo wa elimu umekufundisha kukiita “ukweli wa mwisho” kuhusu maisha yako.
Vua kile ambacho kazi yako imekufundisha kukiita thamani yako. Vua kile ambacho jamii imekufundisha kukiita mafanikio.
Na hata vua kile ambacho imani na mazingira yako ya kukulia yamekufundisha kukiona kama mipaka ya fikra zako.
Halafu kaa kimya kidogo ndani yako, si kimya cha nje tu bali kimya cha ndani kabisa ambacho hukusikii kelele za watu, wala hofu, wala matarajio ya wengine.
Hapo ndipo swali la kweli huanza kuuma taratibu: nikivua haya yote, nimebaki na nani?*
Wengi huogopa kufika hapo kwa sababu wanadhani watapotea. Lakini ukweli ni kwamba, hapo ndipo mtu huanza kupatikana.
Maisha yenyewe ni safari ya mwendelezo. Sisi hatujianzi leo, tunabeba historia ya vizazi vilivyopita na tunaendelea kuiandika kwa namna mpya.
Kila kizazi kimekuja na uelewa wake, changamoto zake, na njia zake za kuelewa dunia. Na kwa hiyo kila mmoja wetu amezaliwa ndani ya mfumo uliokwisha kuanza kabla yake, mfumo unaomfundisha jinsi ya kuishi, jinsi ya kufikiri, na mara nyingine hata jinsi ya kujiona.
Lakini ndani ya mfumo huo, jambo kubwa ambalo mara nyingi hupotea ni nafasi ya mtu kujitazama kama yeye mwenyewe, si kama bidhaa ya jamii, si kama matokeo ya shule, si kama kazi anayofanya, bali kama kiumbe kamili chenye uwezo wa kufikiri, kuhisi, kuchagua na kuelewa kwa kina kwa nini kipo hapa.
Kwa sababu ukweli ni huu: Mtu hujifunza mengi sana kuhusu “kufanya” kabla hajajifunza “kuwa”.
Tumejifunza kufanya kazi, kupata kipato, kutimiza wajibu, kufuata taratibu, na kuishi ndani ya mfumo uliowekwa.
Lakini mara chache sana tumejifunza kusimama na kujiuliza: kwa nini ninafanya ninachofanya, na je maisha ninayoishi yananiwakilisha kweli?
Hapo ndipo mgongano wa ndani huanza.
Mtu anaweza kuwa na kazi, elimu, na mafanikio ya nje, lakini bado akajihisi hayupo mahali pake. Kwa sababu mafanikio ya nje hayajibu kila mara swali la ndani la nafsi. Na hapo ndipo Mtu huanza kutafuta maana, si tu mafanikio.
Lakini maana haipatikani kwenye kelele za dunia, hupatikana kwenye ukimya wa kujitazama kwa uaminifu.
Pale mtu anapojipa ujasiri wa kuacha kujitetea na kuanza kujiuliza kwa ukweli: nini kinaniamsha asubuhi kwa hamasa, nini kinanifanya nijihisi hai, na ni wapi mchango wangu wa aina yake unaweza kuleta tofauti bila kunilazimisha niwe kama mtu mwingine.
Ndani ya kila mtu kuna kipaji, lakini kipaji pekee hakitoshi. Ndani yake kuna kitu kikubwa zaidi kinachoitwa mwelekeo wa maisha, ule msukumo wa ndani unaokuelekeza mahali ambapo uwepo wako unakuwa na maana zaidi.
Na mara nyingi mwelekeo huo huzikwa chini ya matarajio ya jamii, hofu ya kushindwa, na mazoea ya kufuata njia zilizokwisha kukanyagwa na wengine.
Ndiyo maana watu wengi huishi maisha ya kufanana, si kwa sababu hawana utofauti, bali kwa sababu hawajawahi kujipa nafasi ya kuusikia utofauti wao.
Na hili ni jambo muhimu kulielewa: si kila kitu unachofundishwa ndicho kinachokamilisha uhalisia wako.
Elimu, kazi, dini, jamii—vyote hivi ni mifumo ya kukuongoza, lakini havipaswi kuwa vifungo vya kukuamua kabisa wewe ni nani.
Mtu anapokosa nafasi ya kujitafakari nje ya mifumo hii, anaanza kuishi maisha ya kuiga badala ya maisha ya kuelewa.
Na maisha ya kuiga huleta uchovu wa ndani hata kama nje yanaonekana yamefanikiwa.
Kwa hiyo changamoto kubwa ya kizazi chochote si kukosa maarifa, bali ni kukosa nafasi ya kuyaunganisha maarifa hayo na uelewa wa kina wa nafsi zao. Kwa sababu maarifa bila uelewa hujenga watu wanaojua mengi lakini hawajielewi.
Na hapo ndipo dunia huanza kuonekana kama sehemu ya ushindani, badala ya nafasi ya kuchangia.
Watu huanza kujiona tofauti zaidi kuliko wanavyojiona kuwa sehemu ya mfumo mmoja wa maisha unaounganishwa na uhai wenyewe.
Lakini ukirudi ndani yako kwa uaminifu, bila kelele, bila kujilinganisha, bila hofu ya hukumu ya wengine, utaanza kugundua kitu cha ajabu sana: wewe si kosa la mfumo, wala si matokeo ya bahati tu, bali ni mchanganyiko wa uzoefu, uwezo na uwepo unaoweza kutoa mchango wa namna yake ambao hakuna mwingine anayeweza kuurudia kama wewe.
Na hapo ndipo kujitambua kunapokuwa si wazo tu, bali uzoefu wa ndani.
Hatimaye, maisha hayahitaji watu wengi wanaojua kufanya kazi pekee.
Yanahitaji watu wanaojua kwa nini wanaishi, wanaojua kwa nini wanafanya wanachofanya, na wanaojua jinsi ya kuunganisha ujuzi wao na maana ya uwepo wao.
Kwa sababu mtu anayejielewa, hata akifanya jambo dogo, huacha athari kubwa. Lakini mtu asiyejielewa, hata akifanya jambo kubwa, mara nyingi hubaki na pengo la ndani lisilojaa.
Na hivyo basi, safari ya kweli ya Mtu si kupata majibu yote ya maisha, bali ni kujifunza kuishi kwa maswali sahihi, kwa uaminifu, na kwa ujasiri wa kujiona upya kila siku bila hofu ya kubadilika.
Hapo ndipo mtu huanza kuishi, si kama anayefuata maisha, bali kama anayeyaelewa na kuyashiriki kwa makusudi.
Ninaitwa Mbulwa King'ung'e Founder King Mentorship Program.
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment